Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika Wizara hii Wizara ya Ulinzi. Kwanza nimpongeza kaka yangu, ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Kwandikwa, Waziri wa Wizara hii na hoja yake nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani ilikuwa nafikiri jeshi lolote duniani kazi yake ni kupigana tu au kulinda mipaka peke yake ya nchi husika. Lakini nimekuja kujifunza Jeshi ndio nchi na nchi ndio Jeshi. Nimpongeze sana General Mabeyo na timu yake yote, wakati wa msiba wa aliyekuwa Rais wetu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Msiba ule waliubeba ilikuwa natazama mimi TV nikasema kumbe jeshi ni nchi na nchi ni jeshi kuanzia hatua ya mwanzo mpaka walipokwenda kumpumzisha aliyekuwa Rais wetu John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ile sio ndogo na ni kazi moja kubwa sana. Kwa hiyo, mimi nampongeza sana, sana, sana pamoja na jeshi lote kwa ujumla wake walivyosimamia msiba wenyewe, walivyosimamia amani ya nchi, walivyosimamia maeneo yote, ilikuwa naona maeneo tu kule mipakani, kwamba sasa pasitokee na taharuki yoyote katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania. Jeshi letu linafanya kazi kubwa, yako mambo hata kwenye hotuba hawawezi wakayasema. Mipaka yetu inalindwa na jeshi twenty-four seven. Kuna watu pale hawalali saa 24 wanatazama mipaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilikuwa nasikiliza taarifa ya habari kuna baadhi ya wakimbizi wanatoka nchi jirani kule wanaanza kukimbilia huku. Kazi kubwa hiyo inayofanywa na Jeshi letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapo pale. Jeshi wanafanya kazi ya kulinda mipaka yetu, Jeshi wanafanya kazi ya kulinda maeneo mengi, Jeshi wanafanya kazi yanapotokea mafuriko ndani ya nchi yetu hii, kwa mfano, kuna wakati meli ilipunduka katika Ziwa Victoria, walitumwa vijana wa Jeshi kwenda pale, lakini kwa bahati mbaya kwa sababu ya vifaa walikuwa hawana sana, walikuwa na vifaa vichache walichukua zaidi ya siku saba mpaka siku kumi kuokoa ile hali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hoja yangu hapa Mheshimiwa Waziri pamoja na Jeshi yaani uone namna ya kuongeza fedha zaidi za kutosha kwenye eneo hili la kuokoa maeneo ya hatari au kwenye mafuriko kwenye maeneo yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ikitokea kwa mfano sasa hivi treni imepundika, barabara kubwa imekatika, daraja kubwa limekatika, kimbilio letu ni Jeshi. (Makofi)

Sasa hoja yangu hapa, fedha hizi tunapitisha leo trilioni 2.35 na ngapi zisipungue. Ziende kama walivyojipangia wenyewe ili wakajipange sasa waweze kuweka mambo yao vizuri kwa ajili ya Nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya nilisikia wameanza kutengeneza risasi na baada ya mwaka mmoja wataanza kuuza. Sisi tuna karakana kubwa ya Nyumbu alivyosema Mheshimiwa Mwijage pale kubwa mno ile inaweza kuwa ya tatu Afrika au duniani ikawa moja katika sehemu moja kubwa. Hivi tunashindwaje sisi kama Jeshi wakawa na mipango ya kutengeneza risasi na silaha ndogo ndogo. Leo JKT waliwahi ku-assemble matrekta haya wakauza na ikafanya kazi kubwa mno na wakulima wengi wamefanikiwa kutokana na zile treka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Nyumbu karakana ile inaweza wakaagiza engine tu peke yake wana karakana wanaweza kufyatua ma-mudguard, wakafyatua chassis, wakafyatua mambo mengi pale tukaagiza vitu vichache mno vikawa-assembled ndani ya karakana ya Nyumbu. Nyumbu pale tunaweza tukatengeneza risasi, Nyumbu pale wanaweza wakatengeneza silaha ndogo ndogo hizi ambayo kwa nchi kama nchi tunaweza tuka-export kwa nchi jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nyumbu ni kitu kikubwa sana wewe ukienda pale ndio unajua hapa kweli nchi ipo hapa. Ni suala la kukaa kuwekwa teknolojia, kuona bajeti yake, kuhuisha mashine zile wakakaa kama Jeshi, mimi naamini jeshi ni watu wakubwa mno na wanaelimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Jeshi kuna watu wamesoma kwelikweli, juzi tu pale kwenye msiba wa aliyekuwa Rais wetu zilivyopita zile ndege uliamini kama kuna ma-pilot wa aina hiyo. Ndege inaenda inabinuka inarudi namna hii. Kwa hiyo, utaona jeshi lipo vizuri na wanaweza wakafanya kazi vizuri, yaani mimi sasa hivi nimeona jeshi la umuhimu hapa tunatembea kwa amani tu, kumbe kuna watu kule wamekaa wanatulinda. Huwezi kujua wamekaa kwa muda gani, tunafanya kazi zetu vizuri, tunafanya mambo yetu vizuri, tunafanya biashara vizuri, tunafanya vitu vyetu vizuri, nchi leo ya Tanzania hii ni nchi katika nchi tatu Afrika ambazo mpaka leo hazijawahi kuingia kwenye misukosuko ya mapinduzi kwa sababu ya jeshi letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, historia ya Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni pamoja na Afrika Kusini, huwezi kusema Uhuru wa Afrika Kusini waliopata kule bila kuwataja Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Huwezi kusema Zimbabwe bila kuwataja Jeshi la Wananchi wa Tanzania, huwezi kusema leo Congo kuna vijana wetu wapo Congo, vijana wetu wapo Central Africa, vijana wetu wapo Lebanon, bila ya kuwataja Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo ni kazi kubwa mno wanaifanya kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi nilikuwa nataka watoke hapo tuingie, tuiboreshe Nyumbu iweze kuzalisha magari kwa ajili ya matumizi ya kijeshi, wazalishe risasi kwa ajili ya matumizi ya jeshi, waweze kuzalisha bunduki kwa ajili ya matumizi ya jeshi ndani ya nchi na kuweza kuuza ikiwezekana hata kuingia partnership na mashirika mengine ya private.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Urusi, risasi hizi na silaha zao zinatengenezwa na private sekta lakini chini ya ulinzi wa Serikali ya Urusi. Ukienda China hizi hizi risasi, hizi hizi silaha na mabomu mengine madogo madogo yanatengenezwa na private sekta lakini chini ya usimamizi wa jeshi la nchi husika na hiyo inawezekana tu, ni suala la kukaa, kupanga, kuona tutoke hapa sasa jeshi letu tuliwezeshe kuwa katika jeshi moja bora katika Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maslahi ya wanajeshi; wanajeshi tuwatizamie maslahi yao. Mheshimiwa Msukuma alisema nyumba bora, ni kweli, tuwatengenezee namna ambavyo watakavyoweza kuishi vizuri wanajeshi wetu. Ikiwezekana hata kuwaongezea maslahi bora kidogo. Wanajeshi wanavyofanya kazi, yaani wanakuwa na mazingira, unaweza kukuta mwanajeshi mmoja yuko sehemu huku mke wake labda yuko huku, akihamishwa huku, anatafuta ka-chance kadogo tu, Jumamosi, Jumapili anakwenda kumuona mke wake anarudi kwa ajili ya ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wako katika mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama kuna namna yoyote ya kuweza kuona maslahi yao, tuweze kuona maslahi yao hata kuwaongeze posho au mishahara au kuwatengenezea malazi mazuri na makazi mazuri, wahisi kwamba wao wapo kwa ajili ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nimpongeze tena General Mabeyo kwa kazi kubwa anayoifanya mungu akubariki sana, tuko pamoja sana, tutasaidiana sana, sisi kama Bunge wala hatua wasiwasi na naunga hoja mkono. Ahsante sana. (Makofi)