Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kukushukuru wewe mwenyewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia leo katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye ameniwezesha leo nami niweze kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; nampongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu; nampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na timu yake yote ya Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo wanatukonga nyoyo zetu Watanzania, wametuonesha umahiri wao na kwamba wana ari kubwa ya kulitumikia Taifa na wananchi wote wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna moja au nyingine, naitumia nafasi hii pia kuwashukuru wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia mimi uwepo wangu au wamerahisisha mimi Zainab Mwamwindi kuwepo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Nawashukuru kwa namna ya pekee na nasema Mungu awabariki sana, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inahitaji kwenda kwa kasi na ari kubwa. Tunasema tunahitaji Tanzania yenye viwanda. Kilimo kinatajwa kama uti wa mgongo wa nchi yetu na kinatajwa kwa sababu ya kwamba hakuna hata mmoja kati yetu Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambaye hatujui kwamba bila kilimo nchi haitasonga mbele. Ni lazima tulime na tuweze kupata mafanikio mazuri, lakini pia ndoto yetu ya kuwa na viwanda vingi itatokana na uzalishaji mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa kuna Kiwanda kikubwa cha Karatasi cha Mgololo. Kiwanda kile kinazalisha karatasi, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho yake, atueleze au awaeleze wananchi wa Tanzania kwamba ni kwa nini Kiwanda cha Mgololo kinachotengeneza karatasi soko lake halipo lakini pia karatasi zake hazipatikani sokoni na hata kama zitapatikana, karatasi zake huwa ghali sana? Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage naomba atusaidie sisi wananchi, ni kwa nini Tanzania hii tunatengeneza karatasi lakini kwa bahati mbaya sana karatasi zile zikipatikana bei inakuwa ghali kuliko zile ambazo zinaingizwa kutoka nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la kinu cha kusindika au kusaga sembe kilichoko Manispaa ya Iringa. Ni kiwanda ambacho kinasaga sembe. Inawezekana kikawa ni kiwanda pacha, kinahusiana na kilimo vile vile. Kiwanda kile kilikuwa kinafanya kazi vizuri sana huko nyuma wakati wa NMC lakini mara baada ya Shirika la NMC kufa, kiwanda kile sasa kimekuwa hakifanyi kazi kama ambavyo inatakiwa. Pia kuna vijana wetu na akinamama pia wapo ambao nao walikuwa wanapata ajira na wengi wao wakiwa ni akinamama ambao ndio wanaotunza familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, naomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie katika kiwanda hiki, Serikali iweke mkono wake kwa asilimia mia moja ili iweze kuwakomboa wananchi wa Mkoa wa Iringa ambapo wananchi wa Mkoa wa Iringa hasa ni wakulima wa mazao ya mahindi, wanazalisha mahindi kwa kiwango kikubwa sana, lakini mara nyingine tunakosa soko la kupeleka mahindi, tukauze wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, Serikali itie mkono wake kwa asilimia mia moja katika kiwanda kile ili tuweze kukuza ajira kwa vijana wetu, lakini pia wakulima wa Mkoa wa Iringa na mikoa jirani waweze kunufaika na kiwanda kile kwa kuuza mahindi yao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mama. Vazi la mwanamke yeyote wa Kitanzania ni Kanga. Namwomba Waziri wa Viwanda atusaidie sisi wanawake wenye maumbile kama mimi, tumekuwa sasa hatuvai kanga, kwa sababu Kanga zinazidi kuwa ndogo siku hadi siku na akinamama wamenituma nije niseme katika Bunge lako hili. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, kanga zilizopo sasa zinatosha kuvaa wasichana wadogo na Tanzania hii wanawake wameshiba, wako vizuri, wanahitaji kuvaa kanga wapendeze watoke katika shughuli mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, hilo aliwekee kipaumbele sana maana wanawake ndiyo jeshi kubwa na tegemeo la Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza leo kuchangia, naomba kusema naunga mkono hoja ya Waziri wa Viwanda na Biashara. Nasema ahsante sana kwa kunipa nafasi.