Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, na nitumie nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi walao niseme kidogo juu ya Wizara ya Maji kwasababu, ninaamini ili wananchi wetu waweze kufanikiwa kwenye mahitaji yao mengi wanahitaji maji safi salama na maji kwa wingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba, Wizara ya Maji imefanya kazi kubwa sana, sana kabisa, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima pamoja na Wizara kwa Ujumla, chini ya Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu muda wetu ni mchache sana na kwa hizi dakika tano niseme walao mambo matatu; la kwanza Mheshimiwa Kiswaga amezungumza ni vyema sana Wizara ikaendelea kutusaidia katika wakandarasi ambao tumeshawapata kwenye miradi yetu. Kwa mfano mradi wa chanzo kipya cha maji pale Mwanza, mradi ambao ni mradi bora na utakaosaidia sana Jiji la Mwanza kupata maji. Mkandarasi inawezekana akakwama kwa sababu hajapata msamaha wa vifaa vinavyotoka nje ambako alikuwa anafanya kazi nyingine. Ninaamini mkandarasi akipata vifaa hivi kwa wakati tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, ninaendelea sana kuishukuru Wizara kwasababu ya kazi kubwa iliyofanya. Tunao mradi unaoendelea huu wa chanzo kipya cha maji na usambazaji wa bomba kutoka kule Lwanima kwenda Butimba kupitia Sawa kwenda Kanindo kwenda Igoma kwenda Kishiri utakaosaidia mpaka watu wa Buhongwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko tatizo na inawezekana sio la Wizara likawa linaunganisha na Wizara ya Fedha. Tunapompa mkandarasi kazi kuna kitu kinaitwa GN – Government Note; Government Note inatoka ya mwaka mmoja-mmoja. Tunapotoa Government Note ya mwaka mmoja wakati mkandarasi ana mkataba wa miaka miwili au miaka miwili na nusu tafsiri yake ni kwamba, atakapokuwa ameanza ujenzi wa mradi ile GN unakuta imeshaisha muda wake analazimika kusubiri tena miezi mitatu mpaka miezi sita. Hii inafanya tunachelewesha sana wakandarasi tuliowapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ili twende vizuri ninadhani Wizara ya Fedha ikubaliane na Serikali na Wizara ya Maji inapotoa GN itoe GN ya uhai wa mkataba, lakini ikiwa imeongeza miezi 12 itakayoisadia Wizara kumsimamia mkandarasi vizuri na kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na la tatu na la mwisho, ninafahamu Mji wetu wa Mwanza unakuwa kwa kasi. Mpaka sasa tunacho chanzo cha maji kinachozalisha zaidi ya lita milioni 90. Mahitaji ya Jiji la Mwanza, Nyamagana, Ilemela, Magu mpaka Misungwi ni zaidi ya lita milioni 160 na hizi milioni 90 tunazitumia sote kwenye hizi wilaya takribani tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe. Tunao mradi wa Mwanza South tunautegemea sana na sasa tuko kwenye hatua za mwisho. Wataalamu wanasema wanasubiri no objection, Serikali iongeze nguvu ili tupate huu mradi ambao sina shaka utasaidia sana kwenye maeneo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatarajia tukipata fedha hizi tutajenga tenki la lita milioni sita kule Nyamazobe litakalowasaidia sana watu wa Malimbe, watu wa Luchelele, pamoja na Chuo Kikuu cha SAUT ambacho kiko Nayamagana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hiyo tu maeneo yote ya kwenda Igoma, maeneo yote ya Buhongwa. Maji haya yatakwenda mpaka Kisesa kule kwa Mheshimiwa Kiswaga, yatakwenda mpaka kule kwa Mheshimiwa Pastory Mnyeti kule Usagara na kwa kufanya hivi yatakwenda mpaka Ilemela. Hapo tutakuwa tumekidhi walao mahitaji kwa asilimia 98 ya watu wa Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zaidi ya yote nikupongeze sana Mheshimiwa Aweso na msaidizi wako, ndugu katibu na timu nzima mnafanya kazi nzuri, mnakwenda kila mahali na kwa kweli mnaitembelea miradi yenu. Mungu awabariki sana na sina shaka kazi tuliyobakisha ni kusema ndio na shilingi yako mzee upambane kuhakikisha maji yanatufikia. Bwana awabariki sana, ahsanteni. (Makofi)