Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipatia fursa hii kuchangia kwenye Wizara muhimu sana na mtambuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai, lakini zaidi maji ni uchumi. Bila maji hatutaweza kuwa na viwanda ambavyo tunaimba “Tanzania ya Viwanda.” Bila maji hatuwezi kuwa na kilimo chenye tija wala ufugaji; bila maji, wamesema wengi hapa kwamba, afya za Watanzania zitatetereka na itaenda kuigharimu Taifa kuweza kugharimia hawa Watanzania ambao watakuwa wameugua, lakini pia wataacha kufanya kazi za maendeleo kwenye nchi yetu. Bila maji pia tumeshuhudia ndoa nyingi zikiharibika na watu wetu wakiliwa na mamba, watoto wetu wa shule wakipoteza muda mwingi kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa ulijiwekea malengo ambayo yalikuwa kwamba kufikia mwaka 2021 kwa maana ya baada ya miaka mitano, maji vijijini yawe yamepatikana kwa asilimia 85 na maji mijini yawe yamepatikana kwa asilimia 90, lakini kwa taarifa ya Waziri ambayo ameitoa hapa ni kwamba maji sasa ni asilimia 72.3 vijijini ambapo pia siyo kiuhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mpango wameainisha, kwa kipindi chote cha miaka mitano kufikia Desemba, 2020 walikuwa wametekeleza miradi 1,423 ambayo ilikuwa na vituo au visima 131,370. Katika vituo hivyo au visima, ni 86,000 tu vilikuwa vinatoa maji na vituo au visima 44,590 havitoi maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hayo yote yanatokea mosi, fedha tunazopeleka hazina usimamizi na ufuatiliaji wa kina, unakuta fedha za Watanzania masikini zinapotea tu. Zaidi walishindwa kufikia malengo kwa kuwa bajeti tunazotenga haziendi kiuhalisia. Hata ukiangalia bajeti ya 2020/2021, tulitenga shilingi bilioni 705 hapa, lakini Waziri anakiri kwenye ibara ya 22 kwamba mpaka Aprili, 2021 zimeenda shilingi bilioni 376 tu, ambayo ni asilimia 53; ndani ya miezi kumi, bado miezi miwili tu utaona kabisa dhahiri kwamba hawataenda kutekeleza kama ambavyo wamepanga. Kwa hiyo, hata hapa tunaweza tukawa tunakaa, Wabunge tunafurahia tumepewa miradi kadhaa kwenye maeneo yetu, lakini kiuhalisia haitaenda kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo kwenye ubadhilifu wa miradi yetu hii ya maji; na tumekuwa tukiongea hapa kwa kweli, kuanzia Bunge la Kumi, Bunge la Kumi na Moja na Bunge hili la Kumi na Mbili Wabunge wanasimama wanalalamika fedha zinazopotea. Mheshimiwa Waziri


ameainisha hapa kwamba kuna miradi 85 ilibidi irudiwe tena. Nitachukua michache tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye Kiambatanisho Na. 2, mfano ameainisha Mradi wa Ntomoko, Kondoa huko Dodoma zilitumika shilingi bilioni 2.2, lakini tena kuuhuisha, wametumia shilingi bilioni 2.2 na kitu, asilimia 100. Ukienda kule Mombo, Mbuyuni kuna mradi ulikuwa umeshatumia shilingi milioni 400 ukawa haufanyi kazi. Ili kuuhuisha, imebidi tena watumie shilingi milioni 300, asilimia 85.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Arusha huko Karatu Remote, kulikuwa na bwawa linajengwa huko, lilitumia shilingi milioni 124 likawa halijafikia kufanya kazi. Ili kulihuisha lifanye kazi, ikabidi watumie tena shilingi milioni 204, asilimia 165. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujua, hawa watu waliofanya huu ubadhirifu wamechukuliwa hatua gani? Tumeshaomba hapa, Wizara ifanye ukaguzi wa kina kwenye miradi yote ili tuweze kujua ni miradi mingapi imetumia kiasi gani cha fedha ya Watanzania masikini na haifanyi kazi na hao watu wamechukuliwa hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, naenda kwenye miji 28 ambayo na Tarime ilikuwemo. Ni dhahiri hii miji 28 ingekuja ingeweza kutusaidia sana. Kuna fununu kwamba kuna baadhi ya miji itaenda kuondolewa ikiwepo Tarime, Mafinga, Songea na kwingine. Zile dola 460, mwaka 2020 aliongea Mheshimiwa Kitwanga hapa kwa machungu sana, akaelezea kwamba hizi dola 460 zingeweza kutosha miji hata 54; na akaelezea kwamba kuna harufu harufu ya upotevu wa fedha kwenye hii kitu. Sasa badala ya 28, wanataka wapunguze irudi 24.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa DPR ya sasa hivi; kwa maana ya mapitio ya kina ya mradi huu kwa sasa, wanaonyesha kwamba hata mtandao wa maji wanaenda kuupunguza kutoka kilometa 5,751 kwenda 711. Capacity wanaipunguza kutoka 98,450 wanapeleka 48,150. Sasa unajiuliza, kama wanapunguza haya yote, tulitarajia basi gharama ingeenda kuwa kinyume na hapo, badala ya dola 460, ziwe dola 225. Tujiulize nyingine zinaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Tarime mathalani, ukisema ugawanye tu, huwezi ukatumia dola milioni 16.2 ambayo ni shilingi bilioni 38. Tarime pale; kutoka Rorya kuja Tarime ambao watanufaika na wananchi wa Rorya karibia zaidi ya Kata 11, siyo zaidi ya shilingi bilioni 16 tu. Kwa hiyo, tunaomba sana. Kila nikiongea namkumbuka Mheshimiwa Kitwanga mwaka 2020 alivyokuwa akilalamika. Tuna wataalam wetu, tuna ma-engineer wetu, tuna technician wetu hapa hapa Tanzania. Kama WAPCOS tunaona ni shida, basi ufanyike uchunguzi wa kina tena. Hata Bunge lako kupitia hii Kamati ya Maji, muunde Tume ipitie huu mradi. Hizi hela ni nyingi sana. Ni mkopo ambao Watanzania masikini wataenda kuulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuhakikishe kwamba, tunaenda na ile review ya mwanzo na siyo ya sasa hivi ambayo wanasema wanaenda kupunguza baadhi ya miji ili iweze kutumika effectively kuhakikisha kwamba siyo tu miji 28, ikiwezekana na miji mpaka 54. Hata hii 28 yenyewe, 24 ambayo itabahatika kupata, mtandao wa maji nao wameupunguza sana. Kama ilikuwa wakamilishe kwa Tarime nzima Kata nane, sasa hivi watajikuta labda wanakamilisha Kata mbili au tatu. Haiwezekani kabisa, kuna harufu ile ile ya uendelevu wa ubadhilifu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anajitahidi sana, anapita huko kuhakikisha kwamba miradi inahuishwa, lakini sasa bila kung’oa mizizi ya ubadhirifu wa fedha kwenye Wizara hii, tutaendelea kulia na fedha za Watanzania masikini zitaendelea kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa Tarime, vile visima 23 mmechimba visima vinane lakini maji yanatoka kwenye visima sita. Mradi wa Gibaso hautoi maji kule Tarime Vijijini na mradi wa Mwema hautoi maji ambao ulitumia fedha nyingi sana. Tunaomba sana, sana uweze kupitiwa na hawa ambao wanawajibika kupoteza hizi fedha waweze kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)