Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kuunga mkono hoja hii na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Aweso na Naibu wake pamoja na wafanyakazi wa Wizara ya Maji kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya.

Mheshimiwa Spika, maji ni uhai, maji ni kila kitu. Sisi Tanzania tumejaaliwa kuwa na vyanzo vingi vya maji; bahari, maziwa, mito mikubwa na midogo, lakini kwa kiasi kikubwa maji haya hayajaweza kuwafikia wananchi. Kwa hiyo, naomba kutokana na bahati tuliyopata Watanzania kwa kupata vyanzo hivyo, basi viweze kumaliza tatizo la maji vijijini. Tusitumie kuchimba visima tu, lakini pale ambapo ipo mito mikubwa, maji yatolewe kwenye ile mito mikubwa yapelekwe kwenda kusambazwa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna Mto Malagarasi una maji mengi sana. Tulikuwa tunaomba kupitia mto huo, vijiji vile ambavyo vimekaribiana na mto huo viweze kunufaika kwa kupitia maji yanayotoka katika Mto Malagarasi. Vile vile zipo Halmashauri ambazo zinayo miradi ilianzishwa kwa muda mrefu, lakini haijaweza kukamilika. Naiomba Serikali iweze kupeleka pesa ili ile miradi ambayo tayari ilishaanzishwa kwa muda mrefu iweze kukamilika na wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanawake wengi wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji na wanashindwa kufanya shughuli za kuzalisha mali. Kwa hiyo, wananchi wakipatiwa maji, wanawake wataweza kutumia muda mwingi kwenda kuzalisha mali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Sp[ika, vile vile ukosefu wa maji unasababisha milipuko ya magonjwa mengi ikiwemo kipindupindu na kuhara, kama wenzangu walivyosema, fedha nyingi zinaenda kutumika kwa ajili ya ununuzi wa madawa. Pia naomba shule za msingi na sekondari zipelekewe maji. Zipo shule nyingine hazina maji kabisa. Watoto wanapata shida na hasa watoto wa kike, wanapata shida kutokana na maumbile yao. Mtoto wa kike anatakiwa kupata maji kila wakati. Kwa hiyo, naomba maji yapelekwe shuleni; katika shule za msingi na sekondari ili watoto waweze kuondokana na adha hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia karibia kila mwezi Watoto wa kike, wapo ambao wanapoteza siku tano hawaendi shuleni kabisa kutokana na maumbile yao, wanashindwa kwenda shule. Matokeo yake, zile siku tano ambazo mtoto anakuwa hakwenda shule, anapoteza muda wa kusoma, hawezi kufanya shughuli zake za masomo vizuri. Sasa siku tano hizo za kila mwezi, ukizidisha kwa mwaka mzima, mtoto wa kike amepoteza siku ngapi? Ni siku nyingi kabisa. Matokeo yake baadhi ya watoto wanaathirika na kutokufanya vizuri kwa sababu ya ukosefu wa maji mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kasulu una tatizo kubwa la maji, iwe kiangazi iwe masika, mji ule maji yanayotoka ni machafu. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali itusaidie kututengenezea kichujio ili maji yanayotoka katika Mji ule yaweze kuwa masafi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika eneo la Mwandiga nalo bado kuna shida ya maji. Mabomba yametandikwa, miundombinu imesambazwa lakini bado maji hayajafika katika Mji wa Mwandiga; na Mji huo kwa muda mrefu sana, wanapata shida ya maji. Kwa hiyo, naomba kwa sababu miundombinu imeshasambazwa, mabomba yaweze kuletwa kusudi maji yaweze kupatikana katika Mji wa Mwandiga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika katika Mji wa Kibondo tulipatiwa shilingi milioni 700, lakini bado maji hayajawafikia wananchi. Nilikuwa naomba basi, Serikali iweze kupeleka fedha hizo haraka iwezekanavyo ili kuweza kukamilisha miundombinu hiyo wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)