Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Maji. Na nimshukuru Mungu sana kwa ajili ya zawadi ya uhai pamoja na afya njema aliyonipatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Aweso, pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Eng. Maryprisca Mahundi na Katibu Mkuu, Eng. Sanga, kwa namna ambavyo Rais amewaamini kuendelea kuhudumu katika Wizara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama namna ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amepanga uongozi kwenye Wizara hii utagundua kwamba ana matarajio makubwa sana ya safu yake hii kumletea ushindi katika mapambano ya kumtua ndoo mama kichwani. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwaamini hawa na kwa ajili ya msukumo anaoufanya ili wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji ni Wizara mtambuka, ni Wizara ambayo ikifanya vizuri inaweza kupunguza bajeti ya Wizara ya Afya kwa kiwango kikubwa sana. Kwasababu Wizara ya Afya wakati mwingine magonjwa mengi yaliyopo ni ya mlipuko yanayosababishwa na watu kukosa maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Wizara ya Maji mkijitahidi mkafikia tu malengo yenu, bajeti ya Wizara ya Afya itashuka chini badala ya kuendelea kupanda. Sio jambo zuri sana kuona kila mwaka Wizara ya Afya bajeti inapanda, maana yake ni kwamba matatizo ni mengi kuliko mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya Wizara ya Maji ni ya zamani, ni chakavu. Kwa hiyo, tunahitaji nguvu kubwa sana kuweza kuifufua hii miradi na kutengeneza mipya. Mheshimiwa Aweso, wakati mwingine nasema wazi; nchi yetu tusiijenge yote kwa mara moja. Kuna majimbo hayana barabara wala zahanati na maji hakuna, sasa tuwe tunaangalia basi, tufanye sensa ya kutosha tuone hivi maji yako mengi upande gani na upande gani unahitaji, unaweza kuona namna nzuri kabisa ya ku-solve tatizo la maji vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Aweso, sisi Wabunge wa vijijini tuna matatizo makubwa sana ya maji. Visima vyetu vimekuwa visima chakavu, lakini nenda uangalie, hata ongezeko la watu limeongezeka. Chukulia Jimbo la Mvumi; tuna Tarafa tatu za Makang’wa, Mvumi na Mkwayungu. Hizi tarafa zimekuwa miji mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashauri tu hata kama tutakwenda kila mwaka, mwaka mmoja Tarafa ya Mvumi tujenge tanki kubwa la lita laki mbili, mwaka unafuata Tarafa ya Makang’wa tujenge tanki kubwa la lita laki mbili, mwaka unaofuata tumalizie Mkwayungu tanki kubwa la lita laki mbili. Tutakuwa tayari tumeondoa matatizo makubwa sana ya namna ya kupata maji. Kwasababu matanki yetu ni ya zamani mno, yana lita 40,000, lita 50,000; hazitoshelezi kutokana na ongezeko kubwa la watu katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambali ninataka kuishauri Wizara; hivi vile visima kumi vifuatilieni; vimefikia wapi? Maana mwanzoni tulikuwa na visima kumi, pesa zikatolewa visima vikachimbwa baadhi ya maeneo maji yakapatikana, vimefukiwa. Kwa hiyo, wananchi wanaambiwa tu kuna kisima pale lakini maji hakuna. Twende tuwaondolee matatizo kwa sababu kama visima vimechimbwa kusambaza maji kuna gharama gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna baadhi ya maeneo yana maji machungu, yana maji ya chumvi nyingi. Chukua maeneo kama Mlodaa, pale kila tukichimba kisima lazima tukute maji makali sana; Manzase; hivi kama tumeweza kutoa maji Ziwa Victoria tunashindwa nini kuchukua maji Mlowa barabarani kuyapeleka Mlodaa ambapo ni kilometa saba tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mlowa barabarani ina maji mengi, tumechimba Ng’wenda tumekosa maji, tumekwenda hadi mita 150 tumekosa maji, tunashindwa nini kuchukua maji Lowa barabarani au Mlowa bwawani kuyapeleka Ng’wenda, mahali ambapo ni karibu? Tunashindwaje kuchimba maji katika Kata ya Nini kupeleka Ng’wenda; tunashindwaje kutoa maji katika Kata ya Mlowa kuyapeleka Manzase na barabara ni ileile moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo lazima watu wanywe maji ya palepale, maji yatoke sehemu nyingine, yaende yahudumie wananchi sehemu nyingine ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora ya maji safi na salama.


Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna sababu kama sehemu hiyo tuna-drill tunakuta maji ya chumvi, tunaendelea kuchimba tena eneo lilelile; ni kupoteza resources. Tuangalie kijiji gani kiko Jirani kina maji safi na salama tuchimbe halafu tuyapeleke kwa wale wananchi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Aweso, kwa hiyo, nakushukuru sana. Najua mmejipanga vizuri na mnafanya kazi vizuri na Wizara yako itakuwa Wizara ya kelele kwa sababu hakuna mbadala wa maji, maji ni ibada, maji ni afya, maji ni kila kitu. Kwa hiyo tutaendelea kukuhimiza lakini lengo letu ni kukushauri na sisi Wabunge tutakuunga mkono kuhakikisha kwamba unafanya kazi vizuri, wale wezi wa maji tunayo kazi ya kuhakikisha nao vilevile wanapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, upotevu wa maji; tuweke utaratibu mzuri wa kutoa taarifa. Hivi bomba linavuja kutwa nzima na Watanzania wanapita eneo hilo; hii si sawa. Kwa hiyo endeleeni kuzitangaza namba zile za kutoa taarifa za uvujifu a maji, lakini vilevile raia wema watoe taarifa kwa wizi wa maji ili wananchi wote waweze kupata huduma hii ambayo wote tunaitarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja; ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)