Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

Hon. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia. Awali ya yote nampongeza sana Waziri Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri anayoifanya kwenye Wizara hii. Mheshimiwa Aweso ni mmoja katika Mawaziri ambao wanawafahamu wananchi wa Madaba na anafahamika na wananchi wa Madaba. Ametutembelea na kuangalia changamoto zetu katika Kijiji cha Mtyangimbole, lakini pia amekuja Mdaba Mjini Lituta, ameenda pia Kijiji cha Mtepa, Wino na pia amechangia fedha zake kuwezesha miradi ya maji ya wananchi. Ni mmoja katika Mawaziri wa kupigiwa mfano. Kwa niaba ya wananchi wa Madaba namshukuru sana sana Waziri Aweso kwa ushirikiano mzuri anaowapa wananchi wa Madaba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kupitia Wizara ya Maji kwa kufanikisha miradi ya Madaba Mjini, tumefaulu kwa kiwango kizuri lakini bado hatujamaliza ule mradi kwa asilimia mia moja. Nimwombe Mheshimiwa Aweso kwamba eneo la Mtepa, Lituta na Kipingo maeneo ambayo tayari amekwishatembelea yamepata maji kwa kiwango, lakini kwa sehemu kubwa bado hatujamaliza usambazaji. Tunaomba Waziri aendelee kutupa support kwa kupitia timu yake ya mkoa na wilaya ambao kwa sasa wamefanya kazi nzuri sana, tunaomba aendelee kuwatia nguvu wafanikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri yetu ya Madaba tunao mradi mmoja mkubwa sana wa vijiji nane na Mheshimiwa Waziri anavifahamu. Vijiji hivyo nane, ni Rutukira, Ndelenyuma, Bangamawe, Ngadinda, Ngumbiro, Mtyangimbole, Ruhimba na Likarangiro. Vijiji hivi havikuwa na maji kabisa, tulianza mchakato na Mheshimiwa Waziri kutafuta fedha bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa utakaotoa maji Mgombezi kupeleka kwenye vijiji hivi nane. Hata hivyo ilionekana hizi fedha ni nyingi na haziwezi kupatikana kwa mara moja. Ushauri wa Wizara na wataalam ulikuwa twende kwa vipande vipande.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Serikali imeshatenga fedha milioni 350 kwa ajili ya Mradi wa Maji Rutukila na Ndelenyuma, lakini tayari imetenga fedha milioni 300 kwa Kijiji cha Mbangamawe kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi, lakini pia Kijiji cha Mahanje milioni 250. Jumla ya fedha iliyotengwa ni bilioni moja na milioni mia moja na tisa (Sh.1,109,000,000) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa vijiji vinne; kati hivyo vijiji vitatu vinatoka katika vile vijiji nane nilivyokwishavitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapompongeza Waziri kwa kukubali kutenga fedha hii na Serikali kufanya hivyo, ninao ushauri wa kuhakikisha namna gani tunatekeleza miradi hii kikamilifu. Uzoefu unaonyesha mifumo ya utekelezaji ndio iliyoikwamisha Wizara hii kuwafikishia maji watanzania. Moja kati ya mambo ambayo napendekeza, eneo la kwanza utamaduni umekuwa kuunda kamati za utekelezaji wa miradi hii baada ya miradi kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kamati ziundwe kabla ya mradi haujaanza, kamati zishiriki kwenye utekelezaji wa mradi ili wanapokabidhiwa mradi wajue changamoto za mradi. RUWASA watekeleze miradi yote kwa kushirikiana na Kamati za Maji tangu day one hii itasaidia sustainability.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na ushauri wa maeneo mengine matatu, lakini nimesikia kengele imepiga, nataka niongeze umuhimu wa kuhakikisha kwamba mifumo ya kuingiza maji kwenye nyumba, pale Madaba tuna shida, tunawataka wanaotaka kuingiza maji kwenye nyumba waje wanunue mabomba RUWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, inatosha kutoa viwango vya ubora vya mabomba yanayotakiwa, mteja akanunue mwenyewe vifaa vyote, RUWASA wakague wamsaidie mteja. Mfumo tulioweka sasa Mheshimiwa Waziri wananchi wanaamini kwamba ni mfumo unaowezesha watu kupiga fedha, hatutaki kuwapa wananchi fursa ya kutafsiri vibaya nia njema ya Serikali ya kuwawezesha, tuwaachie wananchi wakanunue vifaa. RUWASA wakague vifaa hivi vimefikia viwango viwekwe, sio wananchi wanunue kupitia RUWASA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa RUWASA kununua vifaa vya miradi kwa kutumia mfumo ambao ni centralized unachelewesha sana utekelezaji wa miradi maeneo ya miradi, waandae utaratibu mpya utakaowawezesha wilaya, halmashauri au RUWASA katika ngazi ya wilaya na mkoa kununua vifaa wenyewe moja kwa moja kwa sababu hiyo centralized system ni nzuri lakini inachukua miezi sita mpaka saba kupata vifaa tunavyotaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wanapata maji, Mheshimiwa Aweso amekuwa makini na Naibu wake Waziri, hawajatukatisha tamaa, nasi tunawatia moyo wanaweza, tuhakikishe kwamba Watanzania wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)