Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Elimu. Kwanza niipongeze Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa nzuri sana ya kuratibu na kusimamia elimu nchini, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia hotuba yake ya juzi katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi aliweza kuondoa kwenye asilimia ile inatozwa kwa wafaidika wa mkopo, asilimia sita, tunapongeza sana kwamba hiyo alizingatia na kuiondoa. Vile vile nimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuratibu mafunzo kwa vijana wetu waliomaliza darasa la saba na kidato cha nne ambayo utekelezaji wake unaendelea sasa.

Mheshimiwa Spika, elimu bora ni ile inayotoa maarifa stadi na ujuzi kwa yule anayejifunza ili yamsaidie kukabili Maisha. Sasa kwa upande wa mtaala wa elimu katika nchi yetu mtaala uko vizuri, upungufu wake ni kumwongea maarifa stadi yule anayemaliza ili aweze kukabili maisha. Wapo vijana wamemaliza darasa la saba, wapo vijana wamemaliza kidato cha nne, wapo waliomaliza kidato cha sita, wapo waliomaliza degree na tunao mfano Walimu wako mitaani, wapo Madaktari wapo mitaani, muda huu wana maarifa ya ziada ya kuweza kuyakabili maisha wanaposubiri kuajiriwa. Kinachotokea hapo ni kwamba hapana, ndicho hicho ambacho sasa tunashauri kwamba Wizara iangalie katika mtaala wake waongeze maarifa hayo yatakayokuja kuwasaidia vijana wetu katika maisha.

Mheshimiwa Spika, nilifanikiwa kuwepo Uganda na Kenya kule kwa upande wa shule ya msingi wana somo linaitwa uchumi. Hilo wanasoma kuanzia Shule ya Msingi lakini kwa wale wanaosoma kwa hatua ya cheti au degree na kadhalika, huyo ambaye anategemea kusoma hawezi akapewa degree yake bila kusoma somo la ujasiriamali au entrepreneurship. Kwa hiyo, kwa maana ile asipopata yale maarifa hawezi akapewa degree yake. Ninachoomba kiongezwe hicho katika mitaala yetu, anapokuwa chuoni anasoma Ualimu au anasoma Udaktari aongezewe maarifa hayo ili yamsaidie, anapokosa kwenye ile kozi iweze kumsaidia kwenye maisha yake.

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa wale wanaomaliza kwenye kidato cha nne au kidato cha sita, wengi wamezungumza masuala ya VETA. Niombe sana VETA ziongezwe kila wilaya kwa makusudi ya kwamba yeyote ambaye hakufanikiwa kwenda kidato cha sita, amemaliza kidato cha nne au amemaliza darasa la saba hakufanikiwa kwenda kidato cha kwanza mpaka cha nne, basi aweze kupata maarifa chuoni. Inaweza ikawa kwenye ufundi ujenzi, ufundi mbao au kilimo, hayo yatamsaidia.

Mheshimiwa Spika, katika hilo kuna mkopo unaotolewa kwenye vyuo vikuu, naona haja ya kushauri Serikali iweke mikopo kwa wanafunzi ambao wana soma kwenye vyuo hivi vya kati. Kuna nchi kama Uchina…

SPIKA: Mheshimiwa Kamamba sikukatizi, lakini kwa nini tunajenga hii concept ya kwamba VETA ni kwa wale wasiofanikiwa yaani hiyo inajenga kama kitu fulani inferior hivi. Endelea tu na mchango wako Makamu Mwenyekiti.

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, nazungumza hivi kwa sababu hilo kundi ambalo linakuwa limeachwa, lakini vilevile kwetu kwa sababu mimi ni Mwalimu kutokana na uelekeo wa mwanafunzi, huwa tunawashauri kwamba, kwa uelekeo huu anaweza akaenda akasoma kozi hizo, lakini yule ambaye anafanikiwa kwenda moja kwa moja sawa, lakini kwa yule ambaye anakuwa ameshindwa kupata nafasi ndio nawaangalia zaidi katika hoja yangu ambayo naijenga sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe waweke mkopo nao; kwanza wanatoka katika jamii yetu ni wanafunzi wa kawaidakawaida, lakini anapomaliza masomo yake, tuna hakika anaajiriwa moja kwa moja, anajiajiri, lakini pia huyu anakopesha kwa sababu akimaliza mafunzo yake, atakwenda kujiajiri na kwake anapata nafuu ya kuweza kurejesha mkopo huo kwa wakati, tofauti na huyu ambaye tunampeleka kwenye chuo kikuu, anasoma kwa miaka mitatu ama minne, anarudi mitaani, hana ajira, kwa hiyo si rahisi hata kurudisha ule mkopo anaokuwa amekopeshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa hawa ambao wanakwenda kwenye vyuo wanasomea kazi tena kwa muda mfupi na ni wengi na anamaliza moja kwa moja anakwenda kupata kazi yake, ni rahisi kurudisha huo mkopo. Kwa hiyo, niombe katika mikopo ambayo inatolewa kwenye vyuo vikuu vilevile mkopo uweze kupolekwa kwenye vyuo vya kati.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye upande wa ukaguzi au udhibiti ubora wa shule. Wadhibiti Ubora wa shule ndio jicho la Serikali katika kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa usahihi. Bahati mbaya hawawezeshwi vya kutosha kuweza kusimamia na kuratibu elimu nchini. Niombe wapewe fedha za kutosha waweze kusimamia elimu ya nchi yetu waweze kufanya ufuatiliaji waweze kushauri kwa wakati ili zile changamoto zilizopo katika shule zetu ziweze kurekebishwa, ziweze kusimamiwa na hatimaye elimu iweze kutolewa vizuri kupitia Wadhibiti Ubora. Kwa hiyo, naomba sana Wadhibiti Ubora ambao wapo katika halmashauri zetu zote wawezeshwe ili kuweza kusimamia.

Mheshimiwa Spika, hii inakwenda sambasamba na kuwapa stahili zao. Wadhibiti Ubora wa Wilaya wapo ambao wanasimamia idara. Kuna waraka ulishatolewa wa wao kupewa stahili za Ukuu wa Idara, lakini hawajaweza kupewa stahili hizo. Niombe wapewe hili ziwasaidie katika kusimamia elimu hiyo kupitia ukaguzi ambao wanaufanya.

Mheshimiwa Spika, wapo vijana ambao ni wabunifu, tunawaona kila siku na juzi nimemwona kijana mmoja amebuni mashine ya kukamua muwa kupata juisi. Wapo wengi, niombe Wizara iwachukue hao kwa sababu tayari wameshakuwa wabunifu, lakini wanachoeleza hawana fedha za kuweza kuwasaidia kuendeleza ule ubunifu. Naomba watafutwe, wafuatiliwe wapewe fedha, waendelezwe na hatimaye naamini kwamba wakiendelezwa kwenye ule ubunifu ambao wameshaanzisha, utawasaidia sana kujiongezea kipato lakini itasaidia kuweza kuongeza wabunifu wengi katika nchi hii na kuweza kuboresha miundombinu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kuna mmoja alitengeza mashine ya kutengeneza juisi, lakini yupo mwingine alitengeneza mashine kubwa ya kuchambua nyuzi za katani, niliona Tanga. Kwa kuanzia hawa wafuatiliwe, washauriwe na wawezeshwe ili waweze kuingizwa katika mfumo rasmi na hatimaye waweze kupata fedha za kuweza kusaidia katika kuendeleza ujuzi wao.

Mheshimiwa Spika, kwa leo naomba kuchangia hayo tu. Ahsante sana. (Makofi)