Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Mwanakhamis Kassim Said

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mimi leo sitawapongeza, nitawaombea, namuombea Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mwenyezi Mungu awape nguvu na afya kwa kuwatetea wananchi wa Tanzania. Pia nichukue nafasi hii kumuombea Mheshimiwa Sirro na Kamishna wa Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kuwatetea wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, askari wetu wanafanya kazi ngumu sana, kwa kweli ni kazi ya kusikitisha. Asilimia kubwa ya Askari wa Jeshi la Polisi wanaostaafu ni nadra kuwakuta ni wazima. Askari wetu hawa wanafanya kazi ngumu wakistaafu wengi wana- paralyze. Hawa watu wanafanya kazi kubwa sana na ngumu na maeneo yao ya kazi siyo rafiki.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye vituo vya polisi Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza vipo kwenye hali ngumu lakini hata mazingira yao ya kazi wanapokuwa barabarani ni magumu. Wewe ni shuhuda leo ukiondoka kuanzia Dodoma kufika Dar es Salaam ni askari lakini jua, mvua wanapigwa askari wetu. Kazi yao ni ngumu sana, tutakaa tutawalaumu lakini askari wetu wanafanya kazi ngumu na kipato chao ni kigumu sana. Wapo askari siyo wazuri lakini kuna askari ni wazuri sana akiwemo Kamanda Sirro na Kamishna wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushahidi tosha ni wakati tunapofanya chaguzi. Askari wetu wanafanya kazi ngumu sana ya kudhalilishwa, kutukanwa, ni nusu kujuta kufanya kazi hii lakini hawana lingine la kufanya kwa sababu waliiomba kazi hii. Namuomba Mheshimiwa Waziri wawaone askari wetu kwa posho zao lakini na vitendea kazi. Sasa hivi unakwenda kwenye vituo kuripoti kesi ya ubakaji lakini unaambiwa hakuna gari wala hakuna askari kutoka pale kwenye kituo akamfuata mtuhumiwa, unaambiwa wewe kama unayo pesa utoe mafuta upeleke kule akachukuliwe mtuhumiwa. Mimi nahisi yote haya ni kwa sababu bajeti ni ndogo. Sababu ya vituo vyetu kuwa chakavu bajeti ni ndogo kwa sababu polisi si maskini wa wafanyakazi; wana wajenzi, watu wa umeme, nafikiri wana kila design ya mafundi, kwa nini wasipewe bajeti kubwa ya kufanya kazi zao wanakuwa ni watu wanyonge sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, turudi katika wale wanaostaafu, askari wetu wengi wanastaafu hawapati haki zao mapema. Unakuta askari kastaafu kama mwaka au miezi sita unamkuta ni omba omba. Haipendezi, inakera, inauma na wao ni binadamu kama sisi na wao ni wafanyakazi kama sisi, lazima askari wetu watunzwe wana kazi ngumu kutulinda sisi na mali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bora aombe kuliko kuiba. Wengi tunasema askari wanapenda rushwa lakini mimi nasema wasiombe rushwa ila kuomba ni haki kwa sababu hawaibi. Wanaomba kwa sababu wapo kwenye hali ngumu lazima tuungane bajeti ya watu hawa iwe kubwa, ni haki yao. Mimi nasema pesa hizi angekuwa nazo Sirro angewapa askari wote wakaneemeka au angekuwa Kamishna wa Zanzibar anazo pesa hizi angewapa askari wake wote wakaneemeka kwa sababu hataki waombeombe wala waombe rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini leo unawakuta askari wapo kwenye …

T A A R I F A

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, taarifa

SPIKA: Taarifa, endelea

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mchangiaji anayeendelea kuchangia kwamba kuomba ama kutoa rushwa ni mwiko na ni kinyume kabisa cha sheria bila kujali mazingira uliyopo. Naomba Mheshimiwa mzungumzaji awatetee askari lakini asitee rushwa. (Makofi)

SPIKA: Pokea hiyo taarifa Mheshimiwa Mwanakhamis.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, sitetei rushwa, natetea askari wetu. Wengi tumezungumza hapa, wamesemwa wana vitendo vibaya, wanabaka, wanakera, wanaudhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri ni mwaka wa ishirini au na zaidi nipo kwenye siasa lakini sijawahi kukamatwa kupelekwa kituo cha polisi wala sijapelekwa magereza. Suala la magereza mimi sijui najua utendaji wa kazi wa askari wetu, kwa sababu sote humu tunapogombea anatulinda askari polisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana muda umeisha.

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)