Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika mada hii ya viwanda. Kwanza, niwashukuru sana wananchi wangu wa Kibiti kwa kunipa kura nyingi sana na nawaahidi sitowaangusha. Pili, napenda kuwashukuru na kuwapongeza akinamama wote kwani tunafahamu bila ya mama tusingekuwa hapa duniani, kwa hiyo, hakuna mtu kama mama. Napenda pia kuunga mkono hoja hii mia kwa mia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakwenda kujielekeza katika mada hii ya viwanda. Mada hii ya viwanda ni muhimu sana kwani inagusa sana maisha ya mwanadamu hususani vijana katika soko la ajira. Angalizo langu ningeanza kwa kusema kwamba Waziri mwenye dhamana aangalie ni maeneo gani ya kuanzisha viwanda kutokana na malighafi zinavyotoka sehemu husika. Mfano katika Jimbo langu la Rufiji, tunalima sana mananasi, mpunga, mihogo na korosho. Kwa hiyo, tuna kila sababu lazima tupate viwanda sambamba na mazao hayo. Atakapotuletea viwanda hivyo naamini wakulima wetu sasa watapata soko lenye tija sasa hivi soko la mazao ya matunda ni moja tu kwa Bakharesa, wananchi wetu wakipeleka mazao yao wanakaa foleni kubwa matokeo yake mazao yao yanaharibika na mkulima anapata short. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rufiji tuna Kiwanda cha Kusindika Samaki Nyamisati, lakini kiwanda hiki hakifanyi kazi. Naomba Waziri mwenye dhamana tukutane naye ili tuangalie changamoto ni nini ili kiwanda hicho kianze kufanya kazi. Unapozungumzia prawns lazima utaigusa Rufiji kwani prawns wengi wanapatikana Nyamisati na kiwanda hiki kipo sehemu yenye kina kirefu cha maji. Unapozungumzia kiwanda huna budi urekebishe na uboreshe maeneo ya kufanyia kazi ikiwemo kupeleka maji, umeme na barabara ili mwekezaji anapokuja apate urahisi wa kuwekeza katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kutoa ushauri kwa Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kwamba hivi viwanda vinavyoagiza mitambo kutoka nje iangalie ni jinsi gani ya kupunguza kodi. Kwani kodi mkiweka kubwa, hawa jamaa watakaokuja kuwekeza katika viwanda hivi wataona kama mzigo mkubwa ambapo wataona haina tija kuwekeza katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rufiji tuna Bonde la Mto Rufiji lakini naliona kwamba halina tija yoyote. Sasa hivi tuna uhaba wa sukari, lakini katika bonde hili tungelima miwa na kuweka viwanda vya sukari hata hii shida ya sukari hapa nchini naamini ingeepukika kabisa au kupungua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia viwanda lazima uboreshe mazingira ili yawe rafiki kwa watu watakaokuja kuwekeza katika maeneo husika. Angalizo langu ni kwamba wawekezaji wa nje wanapokuja ni lazima wananchi wa maeneo au wazawa wa maeneo yale wafaidike. Tunachoogopa wasije wawekezaji kutoka nje wakafikia mjini wakachukuliwa na master plan wale wananchi wanaozunguka maeneo yale wakawa hawafaidiki na sekta hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa kuzungumzia mikopo katika taasisi za kibenki, naomba wazawa wapewe elimu ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri wao wenyewe. Katika elimu hii ni vema tukaboresha vyuo yetu vya VETA na viwanda vyetu vidogo vidogo (SIDO) ili wananchi wapate jinsi ya kujifunza ili waweze kujiajiri wenyewe na kujitegemea katika sekta hii ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nipende kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa utendaji wake wa kutumbua majipu. Wadengereko wote wa Rufiji wanasema wako pamoja naye na wanamuunga mkono kwamba aendelee kutumbua majipu ya nchi hii kwa sababu wananchi sasa wanahitaji maendeleo hawataki maneno. Wameona utendaji wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwamba unaleta tija kwa nchi hii. Nasi tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu apate afya njema aendelee kutumbua majipu ili kila mmoja afuate taratibu zinazotakiwa katika utendaji wake wa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia viwanda lazima unagusa maisha ya watu wa hali ya chini. Kwa hiyo, bajeti hii naiunga mkono mia kwa mia, ahsante.