Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie katika Wizara hii ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya yote, kwanza naomba nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi kwa kunipigia kura nyingi sana katika kugombea nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC). Nawashukuru sana kwa kunipa kura nyingi na naahidi nitawafanyia kazi, sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nichukue nafasi hii kwa ufupi nimpongeze mama yangu, Mheshimiwa Margaret Sitta kwa kazi nzuri aliyoifanya. Kwa kweli inadhihirisha wazi kwamba tunapokuwa na watu wazima basi mambo hayaharibiki. Tunamshukuru sana mama na akinamama wote kwa juhudi mlizozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea labda nirekebishe wasemaji wenzangu waliomaliza kuongea sasa hivi, Mheshimiwa Anatropia aliyekaa sasa hivi alikuwa anajaribu kuongea kuhusu deni la EPZA. Ni kweli EPZA wanadaiwa kutoka shilingi bilioni 60 kwenda shilingi bilioni 190, ongezeko la deni hili si kama anavyosema ni kwa sababu ya inflation, hapana! Deni limepanda kwa sababu interest rate imepanda siyo inflation rate. Kutokulipa deni hili kunafanya interest inapanda matokeo yake ni kwamba leo EPZA wanashindwa kulipa deni hilo kwa sababu ya ucheleweshaji wa kupeleka pesa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali na mimi niungane naye, ipeleke pesa ilipe madeni ya EPZA waendelee ku-facilitate yale maeneo na wawekezaji waje wawekeze pale. Wananchi wanadai fidia zao mpaka leo hawajapewa pesa, deni linabaki kwa wale wenye maeneo wanadai, Serikali na yenyewe ongezeko la deni linaongezeka kutokana na interest rate. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ifanye juhudi maalum kwa ajili ya kwenda kulipa deni hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kuchangia siku za nyuma kuhusu maendeleo ya viwanda lakini naendelea kusisitiza. Upande wa viwanda na hasa viwanda vidogo-vidogo, tunaomba Serikali iweke mkakati wa kutosha, tuna vijana wengi nchini wanamaliza vyuo, wanamaliza shule lakini hawana mitaji, wana ujuzi mbalimbali, hawana pa kuanzia! Wakienda benki interest inayotolewa ni kubwa ni more than 25%, ni 17% mpaka 25%! Ukienda kwenye commercial bank kwa mtu wa kawaida hawezi akakopesheka na hasa vijana wetu kwa sababu kwanza wanakosa collateral, inakuwa ni vigumu wao kupata mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Serikali ije na mkakati maalum kwa vijana, iweze kutoa mikopo kupitia dirisha la TIB, mikopo maalum kwa ajili ya vijana, ikiwezekana wapunguziwe interest rate, yaani ile pesa ya riba, kutoka 25% inayotolewa na mabenki wapewe upendeleo maalum. Ikiwezekana wapewe 1% - 3% ili wakopesheke waweze kufanya kazi ya kuanzisha viwanda vidogovidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwenye masuala ya agro processing, tumezungumza vitu vingi sana kwamba tutaanzia na mazao yanayozalishwa na wakulima. Ni kweli, tuanze huko lakini kuna tatizo la kodi kero. Nami na-declare interest, tumezunguka kama Kamati ya Viwanda na Biashara tumekuta mfano, ukinunua alizeti kutoka Bariadi, Mkoa wa Simiyu kupeleka Singida kwa ajili ya kukamua pale Mkoa wa Simiyu anakutana na geti anatoa ushuru. Akifika Maswa anakutana na geti anatoa ushuru. Akifika Shinyanga anakutana na geti anatoa ushuru. Akifika Singida anakutana na geti anatoa ushuru, ndipo anapofikisha kwenye kiwanda. Huu ushuru mdogo mdogo unafanya production inakuwa ina-high cost, matokeo yake bidhaa unapoipeleka sokoni huwezi ku-compete na mtu anayeingiza mafuta ya kupikia kutoka nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbuka mafuta yanayoletwa hapa kutoka nchi za nje (crude oil) ina kodi ndogo sana. Sasa huyu mtu anayemnunua alizeti kwa ajili ya kukamua anakuwa ameingia gharama kubwa ya kulipa kodi ndogo ndogo. Hizo kodi wakati mwingine zinapokusanywa hazifiki mahali husika. Kwa hiyo, ni bora kodi hizi zingefutwa ikawezekana huyu mzalishaji ukampa kodi moja kubwa ya mapato kuliko kuingia gharama ya kulipa kodi ndogo ndogo na kero. Tunaomba hili suala lifanyiwe kazi kwa haraka kwa kweli ni kero kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine niliwahi kuongea nalisisitiza tena, tutafute mbegu bora, mbegu za kisasa ambazo zina mazao mengi. Kwa mfano, alizeti tunapata 70% tu ya ku-extract mafuta kama ukikamua, tunaomba mbegu bora. Ufanyike utafiti maalum kwa kuleta mbegu bora za uzalishaji kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Ufugaji. Mbegu zenyewe siyo za mazao tu, hata za mifugo, tunataka mbegu bora ili tuweze kuvuna mavuno bora. Tunasisitiza tena na hili liingie kwenye kumbukumbu na Serikali ifanye juhudi maalum kwa kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la viwanda vinavyoajiri watu wengi na hasa viwanda vya nguo (textile). Ningekuwa naongea na Mheshimiwa John Pombe Magufuli leo ningemwambia katika mambo ambayo unatakiwa uyaanzishie Wizara ni Wizara ya Textile. Tungeanzisha Wizara au Idara Maalum kwa ajili ya Textile maana kwenye textile kuna mambo mengi, huwezi ku-produce shati bila kuweka vifungo. Huwezi ku-produce shati bila kuwa na material ya plastic, kuna vitu vidogovidogo vingi ambavyo vinaweza kwenda kutoa shati na suruali na vitu vingine. Tukiwa na Idara Maalum au Wizara Maalum basi itahakikisha sisi Tanzania tuna-specialise kwenye masuala ya textile tu. Pamba tunayo, watu tunao, maeneo tunayo, tuna uwezo wa kufanya production ya nguo kuliko nchi nyingine yoyote kwa East Africa na Bara zima la Afrika. Tunaomba hilo nalo lifanyiwe uangalizo maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni Kiwanda cha Urafiki. Tulitembelea kiwanda hiki, 51% inakuwa owned na China na 49% ni Tanzania tunamiliki. Wachina hawafanyi production, capacity ya Urafiki ni kuzalisha mita za nguo milioni 30 kwa mwaka lakini production ya leo ni milioni tano kwa mwaka. Ukienda kwenye store ya Urafiki nje kuna magari yanasubiri production iishe ili wapakie kanga wapeleke Kariakoo. Ina maana demand is high, production is low. Wachina mkakati walionao siyo ku-modernize tena kile kiwanda, wanachotaka wao kufanya ni kuondoa kiwanda na kufanya iwe ni shopping mall, waweze ku-import product kutoka China, wapeleke ajira China, Tanzania tumelala. Mheshimiwa Waziri naomba kwa suala la Urafiki mtoe mkakati tusaidiane, nunueni hizo 2% za Urafiki ownership irudi Tanzania tuendeleze kile kiwanda tufanye production inayoeleweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la TANALEC, mwenzangu Mheshimiwa Anatropia kaliongea. Ukienda Kenya tulisoma tenda document za Kenya TANALEC wanafanya production ya transfoma lakini hakuna upendeleo wa nchi yetu kufanya TANALEC iweze ku-supply transfoma Tanzania. Wenzetu wa Kenya niliona tender form wanazotoa, wanatoa tenda za transfoma kwa vifaa vya umeme na wanatoa elekezo kwamba hii itajazwa na local manufacture tu. Sisi Sheria yetu ya PPRA inaangalia bei, turekebishe, TANALEC imekosa kazi kwa sababu ya sheria hii. Tulimwita Director General wa TANESCO akatuambia tunashindwa kununua TANALEC kwa sababu ya Sheria ya PPRA. Tunaomba sheria hii iletwe mapema tuirekebishe, tu-favor viwanda vyetu. Tunazungumzia viwanda halafu tenda tunapeleka India maana yake nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la uwekezaji, tunaomba zitoke special incentives kwa wawekezaji wanaokwenda kuwekeza mikoani. Sasa hivi eneo zuri la kuwekeza ni Dar es Salaam lakini limejaa, hakuna nafasi. Tunaomba watu wapewe incentive wakawekeze nje ya Dar es Salaam, wapewe special incentive.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.