Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nami napenda kuchangia kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ambayo ni muhimu sana.

Kabla sijaanza kuchangia, napenda kujua kwa kweli hatima ya vijana wawili; Wilson Thomas na Richard Kayanda ambao walipotea wakati wanatoka nyumbani kwangu; walikuwa kwenye timu yangu ya kampeni siku tarehe 26 mwezi wa Kumi, mpaka leo hawajulikani walipo. Hawa vijana wana wake zao, wana watoto wadogo na ndiyo walikuwa tegemeo kwenye familia. Mheshimiwa Waziri unalifahamu hili, IGP analifahamu, RPC analifahamu, OCD analifahamu, DC analifahamu; tungependa kujua hatima ya hawa ndugu, kama wameshafariki mtuambie tuweke matanga; na kama wapo gerezani tuweze kwenda kuwatembelea tuwaone. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee sasa. Ukisoma hotuba au ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu waliotoa Machi, 2021 wameonyesha ni jinsi gani Jeshi la Polisi linakiuka Haki za Binadamu na wakaainisha baadhi ya mambo ikiwepo raia kufia mikononi mwa Jeshi la Polisi, pia ukamataji usiokuwa na staha; na huu ninaweza nikakiri kwamba ni mimi mhanga mmojawapo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2020 mwezi wa Kumi nilivamiwa na Jeshi la Polisi, wakaja kunikamata na video ilizunguka sana. Tena Jeshi la Polisi wanaume, wakati mwanamke anatakiwa akamatwe na Polisi wa kike. Mbaya zaidi, kijana yule Polisi alionekana kabisa akinipapasa kwenye makalio. Kwa hiyo, ni wengi sana wanafanyiwa hii kero. Unapoenda kukamata una-harass kitu ambacho ni kinyume cha haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tunashuhudia watuhumiwa wanapokua kwenye Jeshi la Polisi vituoni wanapigwa na kuteswa. Kuna baadhi ya Polisi wanawatesa wakiwalazimisha wakiri makosa ambayo hawajayatenda na ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu imeainisha haya. Kwa hiyo, Waziri naomba myafanyie kazi ili sasa Jeshi la Polisi, isiwe Police Force kama ilivyo, liweze kuwa ni Jeshi ambalo linatoa huduma kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa spika, kitu kingine ni jinsi ambavyo watuhumiwa kwa maana ya wafungwa na mahabusu wanavyokaguliwa kwenye Magereza yetu. Juzi wakati Mheshimiwa Ole-Sendeka anaongea kwa machungu sana kuhusu Mererani, kwamba watu wanakaguliwa uchi, ikanikumbusha sana wakati niko Segerea. Mnavyoingia pale, mnavuliwa nguo zote, mnaambiwa mnakaguliwa na hata kama mama yuko kwenye siku zake, utaruka kichurachura ili waone kama una kitu umeficha huku chini. Mwaka 2020 nilizungumzia hili jambo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukipiga picha, siku hizi wanakamata hata familia. Leo unamkamata baba ana mkwelima wake, labda mkwelima ana shemeji yake pale, wakifika Gerezani wanavuliwa nguo zote wanabaki uchi wote! Uchi kabisa wa mnyama, anakalishwa kwenye ndoo analazimishwa kwamba ajisaidie haja kubwa ili waone kama kuna kitu ameingia nacho Gerezani. Nadhani hii ni kinyume kabisa na haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru Waziri Mkuu juzi alitoa kauli hapa kwamba wataenda kuangalia, ikiwezekana waweke mashine. Tuwe na modern tools za ku-screen, mahabusu akipita au akiingia anakuwa screened tu, kama kuna kitu ameweka tumboni kitaonekana, kuliko wanavyofanya sasa hivi. Ni udhalilishaji. Yaani kila unapotoka kwenda Mahakamani, ukirudi lazima uvue nguo zako zote, ukaguliwe, ni udhalilishaji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine kwenye NIDA, vitambulisho vya Taifa ni muhimu sana. Mosi, vingeweza kuwa ni pato hata kwa Taifa letu. Tunajua kwamba makampuni mbalimbali yanatumia kama data na wanalipa, bima, ukienda benki, ukienda kwenye simu, lakini pia hata Watanzania wengi hasa walivyosema ukiwa na simu ni lazima usajili kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa, wengi walihangaika sana. Utakuta hata mwingine anamsajilia ndugu yake.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Pili wa Maendeleo uliainisha kwamba kufikia Juni, 2021 tutakuwa tumeandikisha na kutoa vitambulisho kwa Watanzania milioni 21, kitu ambacho kimekuwa kinyume. Hata leo hapa Mheshimiwa Waziri anakiri tumeshamaliza Mpango wa Pili, kwamba ni milioni saba tu ndiyo wana vitambulisho. Pamoja na kwamba kulikuwa na kanuni ya 7(1) inaelekeza wale Maafisa Uandikishaji wanapoandikisha wahakikishe wanatoa vitambulisho ndani ya miezi sita. Mheshimiwa Waziri amesema hapa kuna watu wana namba, ambao ni zaidi ya milioni 18. Hao kwa mujibu wa hii Kanuni walitakiwa wawe na vitambulisho, lakini hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, ukisoma ripoti ya CAG amesema haya yote yamefanyika kwa sababu ya upungufu wa rasilimaliwatu na fedha. Ukiangalia mwaka wa fedha 2016/2017 waliweza kuandikisha 4% tu ya lengo ambalo lilikuwa limewekwa. Kwa hiyo, utaona kwamba hatutoi kipaumbele. Hii inasikitisha. Kama tunaweza tukahuisha na wapiga kura wakapata kadi zao, tunashindwa nini kwenye hiki kitu muhimu sana ambapo Kitambulisho cha Taifa unatembea nacho kila sehemu! Nimesema, kwa hicho kitambulisho unapata mapato kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine CAG ripoti imeonyesha kulikuwa hakuna viashiria ambavyo vingeweza kufuatilia ufanisi wa hii kazi, lakini mbaya zaidi kadi zaidi ya 427,000 ziliweza kuharibika ambazo is worth shilingi bilioni 3,400. Sasa shilingi bilioni 3,400 zimeharibika ambazo hata ukisema ujenge madarasa ya shilingi milioni ishirini ishirini ni zaidi ya madarasa 170 watoto wetu wangeacha kukaa kwenye miti, lakini
zimeharibika. Kwa hiyo, naomba sana tuone umuhimu wa NIDA, watu wapewe Vitambulisho vyao vya Taifa. Kwanza hata inaweza kupunguza uhalifu, maana unaweza uka-m- trace mtu popote pale. Pia hata kwenye haya mambo ya Loan Board wanaweza waka-trace wakajua ni vipi watakupata; na sehemu nyingine zote Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, kingine, napenda kuongelea kuhusu maslahi ya hawa Askari Magereza na Askari wengine kwa kweli. Hawa watu wanafanya kazi. Mimi nazungumzia Magereza kwa sababu nimeishi nao. Namshukuru Mungu nilivyoenda Gerezani miezi minne ile, nimeweza kujifunza mengi sana. Askari Magereza leo, mwenye degree analipwa shilingi 770,000/= lakini hapewi asilimia 15 za taaluma kama wanavyopewa wenzao Askari Polisi. Kwa mfano, Askari Polisi mwenye degree analipwa shilingi 860,000/=, anapewa asilimia 15 ya taaluma ambayo ni shilingi 129,000/=, anapewa shilingi 61,000/= ya pango, lakini wenzao huku hawapati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi hawa watu hawajapandishwa vyeo kwa takribani ya miaka sita. Hakuna ajira ambazo zimefanyika kwenye Jeshi la Magereza na kwingine kote. Tunajua kuna watu wanakufa, watu wanaacha kazi, kuna watu wanalemaa na mambo mengine mengi, sasa tusipoajiri kwenye hii kada tunasababisha utendaji kazi kuwa na udumavu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, uniform, nimelipigia sana kelele hili. Hawa maaskari wanajinunulia wenyewe. Fedha zilitoka mathalani, naambiwa fedha zilitoka kidogo wakaambiwa wanunue baret, lakini ni wajibu wa Serikali kuhakikisha yule Askari anapewa kama ni baret, anapewa shati, anapewa mkanda, suruali, sketi, kiatu everything! Sasa wamekuwa wakijinunulia muda wote. Sasa kama ni hivyo kwamba Serikali inashindwa kuwanunulia, basi waweke package kwenye mshahara wao ili wakiwa wanapata na wawaelekeze ni wapi wanaenda kununua. Ukiwa-align hapa utakuta kila Askari ana-uniform yake tofauti tofauti. Huu pia ni udhalilishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho ni kwenye zimamoto. Lazima tujue kama Taifa majanga ya moto yameongezeka. Umeme wenyewe unakatikakatika kila mara, mengine yanatokea ni hitilafu tu; mtoto amewasha kiberiti, pasi ya umeme na nini; lakini ukiangalia kiuhalisia, hatuna magari ya zimamoto kwenye Majimbo na Wilaya, achilia mbali ofisi. Hapa Mheshimiwa Waziri amesema anajenga Chamwino, kwa sababu hapa kuna Ikulu, lakini huko ukienda wilayani ukikuta gari, ni lile dogo ambalo halina capacity. Kwa mfano, lile gari lililoko Tarime, ikitokea dharura yoyote haliwezi kwenda Mori ichote maji irudi. Kwa hiyo, badala ya kununua magari ya washa washa, tununue magari ya zimamoto.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana (Makofi)