Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Latifa Khamis Juwakali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira). Nami niungane na wenzangu kwa kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya.

Mheshimiwa Spika, pia naomba nichukuwe nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusema kwamba ataendelea kuulinda na kuutetea Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nami nataka niseme nasi vijana tuko nyuma yako mama, tutaendelea kuulinda, kuutetea kuupigania Muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kusema Muungano wetu huu ni tunu na tunasema tunu hulindwa, tunu hutetewa, tunu hupiganiwa; kwa hiyo, nasi kama Watanzania maana yake ni kwamba wajibu wetu ni kuendelea kuulinda kutetea na kupigania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ninukuu maneno ya Rais wetu kipenzi chetu Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alivyokuja kuliutubia Bunge letu hili la Kumi na Mbili. Alisema; “Muungano wa Tanzania ni Muungano wa hiari na umetokana na mambo makuu manne.” Jambo la kwanza alisema, maono ya waasisi wa Taifa letu, ambaye ni Hayati Abeid Amani Karume pamoja na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; jambo la pili, alisema Muungano huu ulisababishwa na utengamano na ukaribu wa kijiografia kwa Tanzania Bara yaani Tanganyika na Tanzania Zanzibar na kwa sasa tunaita Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sipendi sana kuita Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, napenda nitumie Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

SPIKA: Kazi iendelee. (Kicheko)

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, jambo la tatu alisema kwamba uhusiano wa kidugu na urafiki baina na wananchi wa Zanzibar na Tanganyika. Sote tunaona, anayeishi Tanzania Bara na anayeishi Tanzania Zanzibar, karibu sote ni ndugu. Kama huna udugu wa kidamu, basi hata udugu wa kuoana.

Waheshimiwa Wabunge, waliotangulia humu, wengi wamejinasibu, wamesema, wapo ambao wanatoka Zanzibar, lakini wana wake Ukerewe, wameoa wengine Kigoma na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne lilikuwa ni uhusiano wa kirafiki na ukaribu uliokuwepo...

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, anayeongea sasa hivi, Mheshimiwa Latifa Juwakali ni Mbunge wa Viti Maalum, ambaye ameshawahi kukimbiza Mwenge wa Uhuru. Kwa hiyo, anajua vizuri majimbo yenu yote na hata kule Kongwa alifika. (Makofi)

Endelea kuchangia Mheshimiwa Latifa. Anaelewa maana ya Muungano ni nini?

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jambo la nne ni uhusiano wa kirafiki na ukaribu uliopo kati ya vyama vya TANU kwa upande wa Tanganyika na ACP kwa upande wa Zanzibar. Kwa mantiki hiyo, inaonyesha ni jinsi gani huu Muungano ulikuwa ni Muungano wa hiari na Muungano ambao umeweza kuwaunganisha baina ya pande mbili; Zanzibar na Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, nimeanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana tulikuwa tuna kongamano pale na kongamano hili lilikuwa ni kuadhimisha miaka 57 ya Muungano, lakini yeye mwenyewe alikuwa ni shahidi, siyo matarajio kwamba wazee ndiyo watatangulia sisi vijana tutabakia, lakini hata hilo linawezekana, wazee wanaweza wakatangulia, vijana tukabakia au vijana tukatangulia na wazee wakabakia.

Mheshimiwa Spika, kuna kitu ambacho kinanisikitisha sana; leo nchi hii vijana wako wengi sana, lakini kama utakwenda katika vijana kumi uwasimamishe vijana watano wakuelezee historia au wakuambie wanaufahamu vipi Muungano, it is so bad, hawawezi kukuelezea historia ya Muungano. Kwa mantiki hii sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, naomba uniongezee dakika moja.

SPIKA: Endelea.

MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI: Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hii, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, mbali ya kazi nyingi ambazo anaendelea kuzifanya, waandae mpango maalum wa kuweza kuwasaidia vijana wetu ili waweze kuufahamu Muungano vizuri. Waswahili wanasema unachokijua ndicho unachoweza kukifafanua na ndiyo maana minong’ono mingi inakuwa huku, muda mwingine watu wanafuata mkumbo, vijana wanafuata mkumbo, maana yake kuna kero za Muungano, kuna faida za Muungano, hawaelewi. Kero zilikuwepo lakini nyingine zilishachanganuliwa.

Mheshimiwa Spika, hawa watu au vijana kama watakuwa wana uelewa wa kutosha itawasaidia wao sasa kusimama na kuweza kujenga hoja; kweli tuna Muungano, lakini kero zilikuwa hizi na faida ziko hizi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kama vijana wanasimamishwa kule shuleni, tunafanya debates za mada nyingine, hata na hii iwe miongoni mwa ajenda ya kuipeleka katika shule ili iweze kuwasaidia vijana wetu waweze kujua Muungano ni nini na kuweza kuusimamia na kuulinda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)