Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Ameir Abdalla Ameir

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametukutanisha hapa leo. Zaidi napenda kuwapongeza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambao wamenipa imani kubwa na kunichagua kuweza kuliwakilisha Baraza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nitakuwa mtovu wa nidhamu kama sitawashukuru wananchi wa Jimbo langu walionichagua wa Jimbo la Mwanakwerekwe. Ni mara yangu ya kwanza kuchangia humu ndani ndiyo maana natoa shukrani hizo.

Mheshimiwa Spika, niende katika mchango wangu na nitagusa mambo matatu. Kwanza nitagusia suala zima la historia ili watu wajue ni kwa kiasi gani huu Muungano una umuhimu katika maisha ya Watanzania kwa ujumla. Katika kipengele cha pili nitajaribu kueleza angalau mafanikio yaliyopatikana katika kila awamu; kuanzia awamu ya kwanza mpaka awamu ya tano ili pia tuone kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika suala zima la maendeleo ya kiuchumi linakua kwa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, katika historia mimi ni muumini wa faida kubwa zinazopatikana kutokana na Muungano huu. Naomba nitamke hilo wazi na sitatafuna maneno kwamba naziona faida kubwa zaidi na changamoto ambazo zinaelekea ukingoni katika kukamilishwa, kuratibiwa na kuondolewa kabisa. Nikianza katika historia yetu kidogo tu ni kwamba mahusiano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hayakuanza tarehe 26 Aprili, 1964 bali yalikuwa yameshajengeka tangu siku za nyuma. Kilele kile ilikuwa ni kuhitimisha tu lakini mahusiano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yalianza mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nieleze katika karne ya pili ambapo tulishuhudia biashara (commercial contact) ikifanyika baina ya Zanzibar na nchi zile za Uajemi kama Syria, Iraq, Iran ambao hawa sasa walileta bidhaa zao Zanzibar lakini zikifika Zanzibar zilikuwa zikiletwa maeneo ya ndani kwa Ndugu zetu huku Tanganyika tukishirikiana nao kwa pamoja. Kwa hiyo, hata suala la uchumi halikuanza leo; mashirikiano ya uchumi yalianza kipindi kirefu tangu siku za nyuma.

Mheshimiwa Spika, vilevile Profesa Felix Chami, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati anafanya utafiti wake wa ecological excavation katika eneo maarufu Zanzibar, Mkoa wa Kusini linaitwa Kuumbi Cave, naomba mnisikilize kwa makini sana Waheshimiwa Wabunge kuna jambo la msingi sana nataka kusema hapa; katika hili pango Profesa aliweza kugundua kwamba binadamu pale aliishi miaka 30,000 iliyopita.

Vilevile iliweza kugundulika mifupa ya wanyama kama twiga, pundamilia na nyati. Sasa kwa akili ya kawaida unajiuliza wanyama hawa wanapatikana Tanzania Mainland tu imekuwaje leo Profesa Chami katika utafiti wake akagundua wanyama wakubwa wakubwa walikuwa wanaishi maeneo ya Zanzibar. Hii ni kutokana na ile theory kwamba eneo lote hili lilikuwa moja lakini baadaye likatawanyika na likagawa visiwa vidogo vidogo vikiwemo vikubwa Zanzibar na vingine, nadhani jamani tumefahamiana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Muungano huu wa Tanzanyika na Zanzibar naomba tuelewe kwamba ni wa kipekee sana ambapo ni nadra duniani kukuta Muungano umefanyika kwa siku 100 lakini Muungano wetu ulifanyika kwa siku 100 kama na siku 12 hivi kuonesha kwamba ulikuwa ni wa ridhaa, wa damu na wa udugu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yalianza mashirikiano ya udugu, damu baadaye tukaja tukamalizia na suala la documentation. Msingi wa Muungano huu ni maridhiano na ridhaa na hiyari, kwa hiyo, ni vigumu sana kuona kwamba kuna siku Muungano huu utaweza kuvunjika, hilo jambo haliwezekani. Ni sawasawa na kusema mgonjwa wa akili achukue bunduki halafu apige mbu itawezekana wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nachotaka kuzungumza ni kwamba tumepata baraka kubwa kutokana na Muungano huu, tumepata heshima kubwa duniani kutokana na Muungano huu, miungano mingi imeshavunjika lakini huu bado unadumu na unaendelea na utaendelea. Tumeona mfano Muungano wa Syria na Misri, tumeona Sudan ambayo imekatika na kuwa na Sudan ya Kusini na Sudan ya Kaskazini; tuna mifano mingi kama hiyo. Mfano mdogo tu East Africa Community tulianza nayo lakini baada ya muda ili- collapse kidogo kwa changamoto mbili, tatu ambazo hazikuwa-handled vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba wanausimamia Muungano huu kidhati kabisa na tuna imani kubwa utadumu kwa maslahi ya pande zote mbili. Hakuna sababu hata moja ya mtu ambaye anatoka Tanganyika au Tanzania Mainland akamdharau mtu anayetoka Zanzibar Visiwani wala Zanzibar Visiwani akamdharau mtu ambaye anatoka Tanzania Mainland sote ni kitu kimoja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umeisha.

MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)