Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Bakar Hamad Bakar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, kwa kutuamsha na kutufikisha hapa na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia kwa vile, ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako hili, naomba nichukue fursa hii kuishukuru Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, kwa kunipigia kura za kishindo na kushinda kuja kuliwakilisha Baraza hapa kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije kwenye kuchangia Hotuba hii ya Wizara ya Muungano na Mazingira. Kwanza nianze kuwapongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kuwasilisha Hotuba yao hii. Hotuba ambayo imesheheni mambo mazuri kwa mustakabali wa mazingira lakini kwa muungano wetu tukufu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye hoja moja kwa moja kwenye masuala haya ya Muungano. Tarehe 17 Oktoba, 2020 Kamati zetu zile za Muungano kwa maana ya SMT na SMZ zilitiana saini kuziondoa hoja (5) za Muungano.

Mheshimiwa Spika, hoja hizi ya kwanza ilikuwa ni ushirikishwaji wa Serikali ya Zanzibar kwenye masuala ya Kimataifa na Kikanda. Lakini ushiriki wa Zanzibar kwenye masuala ya Afrika Mashariki, lakini pia ni uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi asilia. Lakini pia, kuna jambo kubwa la gharama za mizigo kwa mizigo ile inayotokea Zanzibar kutua katika Bandari ya Dar es Salaam. Mambo haya ni mambo mema sana lakini yanabakia kwenye makaratasi. Kwa nini tunaona aibu, tunaona haya kuweza kuwaelimisha wananchi kufahamu mambo haya? Kufahamu kwanza, kabla ya kuondolewa changamoto hii ilikuwaje? Na baada ya kuondolewa kuna umuhimu gani na changamoto hii sasa ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la gharama za mizigo inayotoka bandari ya Zanzibar kuja bandari ya Dar es Salaam bado kwenye jambo hili kuna changamoto. Pamoja na kuondolewa hoja hii, hatujui kwamba, labda pengine ni suala la elimu, ama ni jambo gani hasa? Lakini kuna changamoto kubwa ambayo inasababishwa, inawezekana na TRA au sijui ni Taasisi gani pale ambayo inahusika na mambo hayo lakini sana sana nadhani ni TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwananchi mmoja mmoja anaondoka na mzigo wake mmoja pengine ni TV moja, anatoka nayo Zanzibar anakuja nayo Dar es Salaam akifika pale baada ya kutoa kodi Zanzibar anakuja tena kutoa kodi nyingine pale. Jambo hili naomba liangaliwe tena upya, kama ni jambo ambalo limeshaondolewa kwenye changamoto kwenye hoja hizi za Muungano lielimishwe limeondolewaje? Likoje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunavyofahamu sisi ni kwamba, kwa mizigo ile inayotoka nje kwa mfano, labda magari Zanzibar ikifika inachajiwa asilimia 40 ya Tax. Lakini yanaposafirishwa huku Bara yanamaliziwa difference ambayo ni asilimia 60 lakini je. kwa mizigo hii midogo midogo hali ikoje? Naomba sana Waziri na Naibu Waziri waelimishe jamii, wawaelimishe watanzania kuhusu masuala haya, bado kuna changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni ucheleweshwaji wa kuwekwa saini mikataba ya Kimataifa ambayo sana sana inahusu Zanzibar. Kwa mfano, ujenzi na ukarabati, kwanza kuna ukarabati wa Hospitali ya Mnazimmoja kule Unguja. Jambo hili limefadhiliwa na Saudia Fund, lakini mpaka leo bado haujulikani mustakabali wa jambo hili ukoje? Lakini kuna ujenzi wa barabara kubwa ambayo inatoka Chakechake-Pemba mpaka Wete, mpaka leo kila siku tunaambiwa tu kesho, kesho! Jambo hili kwa kweli linanisononesha. Nakuomba sana, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze jambo hili limefikia wapi? Na ni lini hasa jambo hili litaondolewa, litatatuliwa na barabara ile ya Chakechake-Uwete itapata ufumbuzi na kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie jambo moja. Kuuenzi, kuutunza na kuuthamini Muungano wetu ni pamoja na kuwathamini viongozi wa Muungano huu. Dkt. Omar Ali Juma alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ukienda katika Kijiji chake kinasikitisha. Kwanza, kwenye kaburi lake ambalo amelazwa pale, utasikitika sana. Barabara ambayo inaunganisha kutoka barabara kubwa mpaka kufika kwenye kaburi lake ambayo pia barabara hiyo inaunganisha kwenda kwenye shule ambayo ipo kwa jina lake yeye Dkt. Omar Ali Juma barabara hiyo ni chakavu haipitiki. Tunaomba Serikali ilione jambo hili na ithamini kiongozi huyu amefanya kazi kubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namuomba sana Waziri atakapokuja hapa aeleze ni mpango gani uliopo kwenye kuthamini mchango wa Dkt. Omar Ali Juma nakushukuru sana. Ahsante sana.