Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Deogratius John Ndejembi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chamwino

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake nyingi ambazo anaendelea kutujalia sisi waja wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kwa sababu ndiyo mara yangu ya kwanza kuzungumza tangu Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, afanye mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kunibakisha mimi katika nafasi yangu nikiwa nahudumu katika ofisi yake, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru sana na kumuahidi sitomuangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushukuru sana wanajimbo wa Jimbo langu la Chamwino ambao wameendelea kuwa na imani nami na tumeendelea kuwa wote pamoja katika kutatua changamoto mbalimbali za Wanachamwino. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa lakini siyo kwa umuhimu, naomba niwashukuru Wabunge wote 19 ambao wamechangia katika hotuba yetu iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri hapa ya bajeti yetu ya Ofisi yetu ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja mbalimbali ambazo zimeletwa na Wabunge hapa tumezipokea na nyingi ni hoja ambazo zimejikita katika kuboresha maslahi ya watumishi wetu wa umma ambao ndio engine ya Serikali yetu, watumishi wa umma ndio ambao wanatoa huduma kwa wananchi wetu ambao wengi wao ni maskini katika Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutambua hilo, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 imeboresha maslahi ya watumishi wa Serikali kwa kulipa malimbikizo ya madeni ya mishahara kwa watumishi zaidi ya 34,676 ambayo yana jumla ya thamani ya shilingi 69,077,261,014 katika mwaka wa fedha huu 2020/2021. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako kwamba madeni ya arrears za mishahara yapo ambayo yalifanyiwa uhakiki na yamelipwa mwezi Novemba, 2020 na kuna madeni vilevile ya arrears ambayo yalifanyiwa uhakiki na yamelipwa mwezi uliopita, mwezi Machi, 2021na hivi tunavyozungumza kuna madeni mengine ambayo tayari yanafanyiwa uchambuzi na uhakiki na yatakwenda kulipwa muda si mrefu tayari yakimaliza uhakiki katika Ofisi ya Utumishi na kupelekwa kwa wenzetu kule Hazina yataweza kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna hoja ambazo zimeletwa hapa na Waheshimiwa Wabunge ya kuzungumzia masuala ya OPRAS ambayo ni Open Performance Appraisal System ambayo ipo kwa watumishi wa umma. Huu ni mkataba wa ufanyaji kazi baina ya mtumishi na mwajiri wake. Sasa hapa kumekuwa kuna changamoto kidogo, na kama mlivyomsikia Mheshimiwa Rais jana, naye alilizungumzia. Changamoto ni kwamba watumishi wetu wengi wamekuwa wakifanya udanganyifu katika mfumo huu. Kwa maana taarifa za mwaka juzi, mwaka jana, ndizo hizo hizo ata-copy na ku-paste na kubadili tu tarehe bila hata ya kujipima.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukimuuliza mtumishi huyu kwamba hivi wewe kuanzia Januari mwaka jana mpaka Januari, 2021, kuna kipi ulichochangia katika eneo lako la kazi cha kuweza kuleta matokeo chanya ambayo ni faida kwa wananchi wetu wa Tanzania? Ukiuliza swali hilo unaweza ukakuta majibu hayaeleweki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunakwenda kubadili mfumo huu na kuweka utaratibu ambao utakuwa ni rahisi sana kwa mtumishi tangu anaingia katika utumishi wa umma na anapoendelea katika ukuaji wake wa utumishi, basi tuweze ku-evaluate performance yake kwa njia rahisi zaidi kwa maana immediate supervisor awe ana uwezo wa kuweka comment, lakini vilevile mwajiri mkuu awe ana uwezo wa kuweka comment katika performance ya mtumishi huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhakikisha ya kwamba hakuna udanganyifu. Kuwe kuna utaratibu wa kuwa na work plan ambayo itatoholewa kutoka kwenye strategic plan ya taasisi yenyewe ili tuweze kujua huyu mtendaji ametusaidia vipi kuweza kufikia malengo yaliyowekwa na taasisi husika, ndipo tutaweza kujua pia kwamba hawa watumishi, je, anastahili kupanda daraja, je, anastahili kupanda mshahara, je, kile anacholipwa na Serikali ni sahihi au amepunjwa au anatakiwa kuongezwa kwa sababu ya tija ya kazi yake anayoifanya?

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tunakwenda kulifanyia kazi na kuhakikisha kwamba OPRAS hii inabadilika na kuwa yenye tija katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi pia wamezungumzia suala la kuwawezesha watumishi wetu kwa kuwafanyia training mbalimbali na kuwapa mafunzo kuweza kujua kazi zao ziko vipi na mafunzo mengine ambayo ni ya on the job training.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili tumegundua kwamba kuna changamoto moja; tuna Chuo cha Utumishi wa Umma, lakini chuo hiki waajiri wengi wamekuwa hawatengi mafungu au fedha za kuweza kupeleka watumishi wao kuweza kufanyiwa mafunzo ya utumishi wa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mtu ametoka chuo fulani lakini akiingia kwenye utumishi wa umma lazima afunzwe apewe etiquette za utumishi wa umma na aweze kuendana nao katika miaka yake yote ya utumishi. Hili ninaamini muda si mrefu Waheshimiwa Wabunge mtaona mabadiliko makubwa sana kwenye hili. Tunataka kuwe na uniformity katika utumishi wa umma, kwamba watu wanavyo- behave akiwa mtaani na akiwa kazini, basi mtu akimuangalia aweze kufahamu kwamba huyu ni mtumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge ambao wamezungumzia suala zima la Uwezeshaji wa Kaya Maskini (TASAF). Mpango huu kiukweli umesadia watu wengi, kaya nyingi ambazo hazikuwa na uhakika wa mlo hata mmoja katika kaya zao, lakini leo hii zimekuwa zina uhakika wa milo mitatu na kaya nyingine zimekwenda hata kuboresha maisha ya kuwa na biashara, kuwa na mifugo, kulima kilimo kilicho bora na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwahakikishie Wabunge, kaya zilizokuwepo kwenye TASAF III, Phase One zilikuwa ni kaya milioni moja Tanzania nzima. Sasa tunakwenda kuwa na kaya 1,400,000 katika nchi nzima, ambapo vijiji vilivyoachwa mpaka ifikapo mwezi Julai, 2021, vijiji vyote katika nchi yetu vitakuwa vinapokea TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika suala hili ninaomba sana ushirikishwaji wa Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani, mshiriki sana katika kutoa elimu kwa wnanachi wetu kwamba TASAF si jambo endelevu, TASAF imekuja kwa sababu ya kukuwezesha wewe kukutoa katika hali moja na kukuweka katika hali nyingine ya maisha yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumekuwa na upotoshwaji unaendelea, wanaelezana watu huko kwamba ukiboresha maisha yako watakutoa kwenye Mpango wa TASAF. Lengo la TASAF ndiyo wakutoe, lakini ukiwa umeboresha maisha yako. Kama walikukuta huna mbuzi basi uwe una mbuzi watano, una kuku kumi, una bata ishirini na una nyumba bora, ndilo lengo la Mpango wa TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mwisho wa siku ukibaki kwenye mpango huu kwa muda mrefu, siku mpango huu unapokuja kuisha tutakuwa tumetengeneza tatizo kubwa zaidi badala ya mpango huu ulipofika. Mpango huu lazima Waheshimiwa Wabunge twende majimboni mwetu tutoe elimu kwamba umekuja kuwasaidia kuboresha maisha yao na siyo kuwa tegemezi wa mpango huu katika maisha yao yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, ndugu yangu, kaka yangu, Mheshimiwa Malima, ametoka kumalizia hapa na amezungumzia utaratibu wa kupata kaya hizi maskini. Nilifahamishe Bunge lako Tukufu kuwa utaratibu ni kwamba unakwenda kwenye mkutano wa kijiji na mkutano wa kijiji ndiyo unatambua kaya zile maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa changamoto imekuwa kwamba katika wale wananchi wa eneo husika kuna watu ambao wana status fulani katika kijiji. Wale watu wanaogopeka na wanawekwa kwenye mpango na wakiwa kwenye mpango watu wanaogopa kusema kwa kuogopa akisema anaweza akachukuliwa hatua mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine nyingi tumezichukua na Mheshimiwa Waziri wangu, Mheshimiwa Mchengerwa naye atazizungumzia. Lakini nyingi tulizozichukua tutazitafutia majibu na kuzijibu kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)