Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia hii bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Nianze kwa kuwashukuru watumishi, hawa watumishi wa Umma. Watumishi wa umma ndiyo wapishi wakuu, ndiyo wapishi wakuu wanaofanya mambo haya tunayoyaona. Mafanikio yote yanayosemwa sisi wanasiasa tunakuwa juu na bendera, lakini mpishi mkuu ni mtumishi wa umma. Nimewashukuru watumishi wa umma kama vile nilivyowashukuru wakulima na wafanyakazi waliotuwezesha kupata chakula cha kutosha kwa miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, utawala bora na utumishi ni sekta muhimu, ni sekta muhimu kama ambavyo zimeanishwa katika Mpango wa Tatu wa Dira ya Taifa na Lengo la Taifa la 2025. Katika Dira ya Taifa 2025 tunazungumzia utawala bora, lakini tunazungumzia amani, utulivu na mshikamano. Huwezi kuwa na utulivu na amani kama hauna utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo wananchi wanapoona amani na mshikamano ina maana nchi hii ina utawala bora. Sitachukua muda kuzungumzia suala la utawala bora kwa sababu kila mtu anafaidi amani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie utumishi, ninayo mapendekezo, mtumishi ukitaka kumpa motisha ili aweze kufanya kazi vizuri kuna mambo muhimu ya kuongelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mapendekezo, naiomba Wizara hii ibaini mahitaji ya watendaji ya watumishi tujue tunahitaji watumishi kiasi gani; sekta ya afya, watumishi kiasi gani; sekta ya elimu, kiasi gani; ugavi wa kila namna ili tukiwa tunajua watu tunaowahitaji basi tujue mapungufu yetu ni kiasi gani ili nchi hii tuweze kuwa na walimu wanaotakiwa, waganga wanaotakiwa ili wale waliopo waweze kupata motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shule yenye mahitaji ya walimu kumi ukitaka kuwa-demotivate waliopo wapange wawili. Ni kama timu ya mpira, timu ya mpira ya watu kumi na mmoja ukitaka kuwa-demotivate weka wacheza mpira saba hawatafanya kazi. Kwa hiyo, pamoja na miradi yetu ambayo lazima iendelee, mradi kielelezo mwingine ni kuajiri wafanyakazi wanaotakiwa kila sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta za uzalishaji (the productive sectors) hatutaweza kuzalisha kwa tija kama hatutakuwa na wagani wanaotakiwa. Kumbe Wizara hii ndiyo inahusika na kutoa na kutoa vibali, Wizara hii ndiyo inachakata, inachakata, inachakata ule mchakato mzima wa kuajiri kwa maneno mengine ndiyo waajiri wenyewe. Kwa hiyo, katika sehemu nzuri tunayopaswa kuingalia ni hii ya watumishi na imeandikwa wala sio mjadala.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yoyote ili iendelee inahitaji watu. Unaweza kuwa na madini, unaweza kuwa maji na usiendelee, lakini ukiwa na watu mfano wa Japan, Japan hawana migodi lakini wameendelea kwa sababu wana watu. Ndiyo maana katika Dira ya Taifa ya 2025 lengo letu ni kuwa na watu walioelimika na wenye uchu wa kujifunza ambayo ni kazi ya ofisi hii ambayo tunajadili bajeti yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna mambo madogo ya kuangalia ni msingi, kuna suala ambalo naungana na TAMISEMI wanaposema kwamba watakapoajiri watakuwa wanawapanga watu kwenye mikoa ambako wataweza kutumika na hawataondoka mpaka baada ya miaka mitatu.

Mimi nashauri kwamba kila mkoa upangiwe quota yake; wafanyakazi wangapi waende kule na mtu akubali kuwa anakwenda Rukwa, anakwenda Kagera, anakwenda Dodoma, anakwenda Dar es Salaam na hatatoka si pungufu ya miaka mitano. Hii itatuondolea hii kadhia waliyoisema watu wanakwenda kuchukua check number.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hilo nitoe angalizo kuna haja ya kujenga jamii, hapa nazungumzia ndoa changa, haja ya kujenga jamii si busara wanandoa wachanga wenye miaka miwili/mitatu mpaka kumi bwana kukaa Tabora na bibi akakaa Tanga, hii itakuja kutuletea kujenga jamii ya ajabu ajabu. Kwa hiyo pamoja na kupanga watalaam zingatia msiwape kadhia hawa wanandoa, otherwise tutakuja kuzaa watoto, unakuja mtoto unarudi nyumbani mtoto anakuita mjomba. Sasa ina maana nyumbani kila siku walikuwa wanakuja wajomba. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ustawi; ustawi wa nchi unapaswa kuwa na nguvu kazi…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwijage hebu subiri kidogo. Walikuwa wanakuja wajomba, kwa hiyo ni upande mmoja tu ambao unahusika au hebu weka vizuri hilo eneo kidogo. (Kicheko)

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kinyume cha mjomba ni nini? Napenda nikiri kwamba kwetu ni kilometa 1,600 kutoka Pwani kwa hiyo Kiswahili kilichelewa kufika. Mimi najua madhara ya wajomba. Naomba kwa ruhusa yako hilo swali linishinde, nizungumze…(Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Aah, ngoja ngoja, ngoja inabidi tuweke vizuri, labda, lazima uwelewe Malkia wa Nguvu siku hizi tunatunza umalkia kwa wivu kabisa. Eeh ukituambia sisi ndiyo tunaoleta wajomba na ninyi mnaleta mashangazi kwa hiyo lazima sentensi ziwe zinanyooka vizuri. Mama pia anaweza akarudi nyumbani akaitwa shangazi. (Makofi)

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunifundisha msamiati, kumbe kinyume cha mjomba ni shangazi. Napenda ni kiri tena kwamba Kiswahili mimi kwangu ni tatizo, kwa hiyo hoja yangu iko palepale, kwa hawa watu wenye ndoa changa ni vizuri wakakaa pale na sasa hivi kwa hali tuliyonayo Tanzania tunao wataalam wa kutosha.

Nizungumze kuimarisha sekta ya umma, jambo ninalopendekeza kwa Serikali; watumishi wa umma wanapoanza kazi day one ni muhimu Serikali kuwajengea mazingira na kuwaaminisha kwamba leo ni watumishi wa umma, kesho watakuwa watamishi au wadau wa sekta nyingine. Unapokuwa wewe ni mtumishi wa umma, ujue kesho utakuwa kwenye sekta nyingine ambayo ni sekta binafsi ukiwa mwajiri au mwajiriwa; kwa hiyo mazingira yako sasa uweze kujiandaa kwa kwenda sekta nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lengo langu ni nini! Kama sekta ya umma itastawi watu waliopo nje sekta ya umma watajenga wivu wa kuingia katika sekta ya umma, lakini na wa sekta umma sasa watajenga wivu na wataitendea sawia sekta binafsi. Watumishi wa umma wasiojua kwamba siku nyingine watakuwa watumishi wa sekta binafsi huwaangalia kwa jicho baya watu ambao ni wa sekta binafsi. Kwa hiyo, ukiwa umekaa kwenye sekta ya umma ujue ipo siku na wewe utakwenda kwenye sekta binafsi ukiwa mwajiriwa au ukiwa mwajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)