Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ya kuweza kutoa mchango katika hoja ambayo iko mbele ya Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Ummy Ali Mwalimu ambaye hapo nyuma alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga na sasa tumemkabidhi Jimbo la Tanga Mjini na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze rafiki yangu Mheshimiwa Silinde na Ndugu yangu Dugange kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, lakini kipekee nimpongeze sana Katibu Mkuu Profesa Riziki Shemdoe. Huyu ni kijana wangu anatoka kabisa pale Mlalo, kwa hiyo, hayo ni matunda ya Mlalo. Pia niwapongeze Ndugu Magembe na Ndugu Gerald Mweri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mchango wangu ujikite sana kwenye eneo zima la elimu na nitaanza katika ngazi ya Halmashauri ya Lushoto ambayo ni halmashauri ya nne nchini kwa kuwa na shule nyingi za msingi. Halmashauri ya Lushoto ina shule za msingi 168, shule hizi ni nyingi sana ambazo nadiriki kusema kwamba kwa ngazi ya Halmashauri tunashindwa kuziendesha sisi wenyewe, hivyo, tunaiomba Wizara na Mheshimiwa Ummy yeye alikuwa Mbunge wa Viti Maalum anajua, watusaidie tutengeneze Kanda Maalum ya Kielimu ya Lushoto, vinginevyo mara zote mtatuona shule za Lushoto zikiwa za mwisho katika mitihani mbalimbali kwa ngazi zote kuanzia msingi mpaka sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Lushoto imetawanyika sana kwa sababu ya safu ya Milima ya Usambara, kwa hiyo, hata jiografia yake ni ngumu sana kufikika kila mahali na hiyo pia inachagiza hata watumishi mara zote wanapoletwa Lushoto, hasa Wlimu, wanahama na kuhamia Wilaya nyingine za bondeni ama mkoani kwa ujumla. Kwa hiyo, tatizo kubwa ni jiografia ambayo sasa inaathiri utoaji wa elimu na upatikanaji wa elimu bora, kwa hiyo, niombe sana, ukiangalia mgawanyo wa baadhi ya halmashauri, kwa mfano nitasema Mafinga Mjini kwa ndugu yangu, shemeji yangu, Mheshimiwa Chumi, shule za msingi katika Halmashauri ya Mafinga ni 28, ukienda pale Korogwe Mji ni 36, ukienda Pangani ni 36, lakini ukienda Mlele kwa Mheshimiwa Kamwelwe pale wana shule 13 katika halmashauri nzima, utawezaje kutoa mgao sawa na halmashauri yenye 168? Hii kwa kweli ni dhahiri kwamba, jambo hili lazima liratibiwe upya na tuweze kuwa na mgawanyo ambao unaeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye Walimu; Walimu waliokutwa na vyeti fake katika Halmashauri ya Lushoto walikuwa 216, lakini hatujarejeshewa idadi hiyo, isipokuwa tulikuwa tunapata tu mgawo huu wa kawaida wa Walimu 16, Walimu 24, Walimu 60 na katika awamu hizi zote tatu za nyongeza ya Walimu. Kwa hiyo, niombe sana kwamba, wale ambao wametoka kwa sababu ya vyeti fake 2016 tungepata idadi kamili ile irudi ili iweze kusaidia katika eneo hilo. Hivi ninavyozungumza tuna uhaba wa Walimu 1,274 katika Halmashauri ya Lushoto kwa hiyo, utaona kwamba ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie katika eneo lingine ambalo hili ni la kitaifa. Kuna tatizo kubwa ambalo tunalo katika mgawanyo wa hizi fedha ambazo zinakwenda kwenye capitation. Serikali imeweka utaratibu mzuri tu ambao tangu mwaka 2016/2017 tulitenga zaidi ya shilingi bilioni 219, lakini mwaka 2017/2018 bilioni 220, mwaka 2018/2019 shilingi bilioni 286, mwaka 2019/2020 shilingi bilioni 288 na mwaka 2020/2021 shilingi bilioni 298. Ni jambo jema kabisa kila mwanafunzi kati ya wanafunzi milioni kumi n amia tano wa shule za msingi wanapata Sh.10,000, lakini pia wanafunzi milioni 2,200,000 wa shule za sekondari pia wanapata shilingi 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja iko pale kwenye ile pesa kuna shilingi 4,000 hii inakatwa kwa ajili ya vitabu, inayokwenda shuleni ni shilingi 6,000 ambayo na yenyewe ina mgawanyo wake; kuna ambazo zinakwenda matumizi ya ofisi asilimia 35 kwenye ile shilingi 6,000; taaluma asilimia 30 kwenye shilingi 6,000; mitihani asilimia 15 kwenye shilingi 6,000; huduma ya kwanza asilimia 10 na ukarabati asilimia 10 ambapo ukiangalia asilimia 10 hizi ni kama shilingi 600. Sasa sijui ukarabati wa Sh.600 tunakarabati nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hoja yangu iko kwenye zile shilingi 4,000 ambazo zinakuwa retained kwa ajili ya ununuzi wa vitabu. Ni masikitiko makubwa kwamba, ndani ya kipindi cha miaka hii mitano vitabu vimeanza kusambazwa takribani miezi mitatu iliyopita, mimi ndio nimeona vitabu kwenye Halmashauri ya Lushoto. Bahati mbaya sana vitabu vyenyewe vimekuja kwa ratio ya wanafunzi watatu kwa kitabu kimoja. Sasa ninajiuliza kwamba, hizi hela zote zilizotengwa kwa miaka mitano ambazo ni takribani shilingi 200,000,000,000, zimefanya kazi gani na zilikuwa zimewekwa kwenye akaunti gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama vitabu vimechapishwa kwa mara moja tu, tutaona kabisa kwamba hapa kwenye Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuna tatizo, lakini pia kwenye Wizara inayosimamia sera, kwa maana ya Wizara ya Elimu, kuna tatizo. Tukumbuke kwa mara ya kwanza walichapa vitabu vya shilingi 144,000,000,000 ambavyo vilikuwa vimekosewa na vikaondolewa kwenye mzunguko. Hatujawahi kuambiwa ndani ya Bunge hili kwamba, wale waliotia ile hasara wamechukuliwa hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali huko za watu, wahujumu uchumi na kadhalika, lakini katika eneo hili hatujawahi kuona shilingi 144,000,000,000 ambazo vitabu vimechapishwa havina ubora, lakini pia vimekosewa, havikuwa na maudhui, wala havikuwa vinafuata hata mtaala husika, vimeondolewa katika mzunguko kimya kimya na vimewekwa kwenye maboksi vimeachwa huko huko kwenye shule wala hawajavikusanya, hatuambiwi hasara hii ambayo Taifa tumeipata ni watu wangapi wamewajibika kwa kosa hili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana hizi ni zama za kuambiana ukweli. Tunaomba kabisa kwamba tusicheze na elimu, kwa sababu haya matatizo yote tunayoyaona sasa hivi ni kwa sababu tulikuwa tunaifanya elimu kama ni jambo ambalo sio la msingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana tupate majibu na hizi ni takwimu sahihi kabisa kutoka Serikalini huko. Watueleze pesa zetu hizi za vitabu kwa miaka mitano na vitabu vimepelekwa katika awamu hii, tena miezi mitatu iliyopita na bado vimepelekwa kwa ratio ya watoto watatu kwa kitabu kimoja kwa mujibu wa halmashauri yangu. Ningependa sana kuona kwamba kama tunasema kila mwanafunzi anapata Sh.4,000 kwenye capitation, tulitaka kuona kwamba wanafunzi nchi nzima wanapata vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwa kuwa sasa tunakwenda katika ulimwengu wa TEHAMA ningeomba sana kwamba kwenye capitation hii tuangalie sasa uwezekano wa kuanza kwenda kupeleka ipad ama computer mpakato kwa wanafunzi ili waanze kusoma kwa kujifunza mambo ambayo yanabadilika katika dunia hii ya leo. Tunakwenda katika artificial technology ambayo TEHAMA ndio inayotawala ulimwengu sasa tutakapokuwa tunaendelea kupeleka hela za vitabu, lakini tuone pia umuhimu wa kuangalia eneo zima hili la teknolojia kwa sababu sasa hivi umeme vijijini umeendelea kwenda na maeneo mbalimbali sasa umeme upo. Kwa hiyo, naamini kabisa kwamba, tukiweka hivyo tutawasaidia hawa vijana wetu kujifunza kwa vitendo kwenye dunia ambayo wanakuja kuitawala siku za usoni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)