Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. TAUHIDA C. GALLOS Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuweza kunipatia fursa hii ya kuweza kuchangia Wizara hii ya TAMISEMI. Nichukue fursa hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake. Mheshimiwa Waziri dada yetu dada Ummy Mwalimu nikupongeze kwa nafasi hii uliyopewa ya Wizara hii ya TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa tunakufahamu hatuna mashaka na uwezo wako tunaamini kwenye Wizara hii utatuvusha vizuri. Hatuna mashaka kwasababu hufanyi majaribio juu ya kazi hii tunajua umekuja kufanya kazi na utachapa kazi. Ikiwa sisi kama wenzio kuna baadhi ya mambo tukwambie ili uweze kuyafanyia kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri pamoja na pongezi lakini kwa sehemu lazima tukupe pole, pamoja na pongezi zote zilizo toka hapa kwa Wizara hii tukupe pole.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunaendelea kukuombea unajua kwa sehemu kubwa wanawake wenzio ndani ya Bunge tunavyokuunga mkono. Tutaendelea kukuombea Mwenyezi Mungu akujalie, akutie nguvu, akupe ujasiri, uweze kuisaidia Taifa letu. Uweze kutuvusha kama wanawake, uweze kutuvusha kama wabunge wenzio tuweze kwenda salama kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya TAMISEMI ni kubwa na ina mambo mengi. Mheshimiwa Waziri kwanza kabisa nianze kwa kusema wizara hii pamoja na kazi nyingi inayofanya tunaomba mpate muda wa kufanya vipindi kwenye TV hususani wa kutoa elimu kwa wananchi. Wananchi wengi hawafahamu tafsiri ya Hati Chafu na Hati Safi, wengi wao wanatafsiri tofauti na ilivyo ndani ya tafsiri ya Hati Chafu na Hati Safi. Niombe ukipata fursa kama kutakuwa na vipindi andaeni vipindi vya kuwaelewesha wananchi tafsiri za Hati Safi na Hati Chafu. Kwasababu tafsiri hii inaenda ni kitaalam zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi wanaposikia Halmashauri nyingine imepata Hati Chafu wakiamini kwamba kuna mambo mabaya, mabaya yaliyopitiliza lakini kuna baadhi ya Halmashauri zinapata Hati Safi iwaje ndani ya halmashauri hizo zina upigaji na miradi mibovu ambayo tunaishuhudia ndani ya macho yetu. Fursa hiyo tumeipata Wabunge kwasababu tunaenda kukagua miradi, wakati tunakwenda kukagua miradi tunakutana na Hati Safi ingawa halmashauri hiyo ina miradi mibovu na utekelezaji wa miradi ya wananchi ipo sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mheshimiwa Waziri takribani wapigaji wote wana utalaamu wa kutengeneza hati safi kwasababu wanazifahamu zinapatikana vipi. Mheshimiwa Waziri tunaomba kwenye haya yafanyanyieni uchunguzi wa kina lakini wapeni taaluma ya kutosha wananchi wapate kujua tafsiri za Hati Safi na Hati Chafu. Watu ambao wanapata Hati Chafu wanakuaje na wanaopata Hati Safi inakuaje wakapata zile Hati. Hata sisi tunavyopangiwa Kamati kuna muda zilikuwa zinatupa shida kutafsiri hizi Hati, lakini kwa kuwa tunapewa elimu na taaluma ya kutafsiri hizi Hati huwa tunaelewa kazi zinakwendaje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la asilimia 10 ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Mheshimiwa Waziri tunakuomba shughulika na hizi asilimia 10 za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hili ndiyo jibu la Watanzania. Kama mikopo itatolewa ipasavyo, kama wanawake, vijana na wenye mahitaji maalum watawezeshwa ipasavyo, Tanzania tutapiga hatua, Halmashauri zitasaidia viongozi wetu kufanya kazi vizuri. Mheshimiwa Waziri ana mambo na kazi nyingi, namshauri atenge vipaumbele aone ataivusha vipi Tanzania, afanye kazi kwa kumsaidia Rais wetu. Nashauri Waziri aweke vipaumbele kwamba ndani ya mwaka mmoja au miwili vitu gani anaweza akavifanyia kazi na vikaleta jibu ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote nilizokaa ndani ya Bunge hili nimekuwa mjumbe wa Kamati ya LAAC, sikuwahi kuona kuna jibu sahihi kuhusiana na asilimia 10. Pamoja na sheria tuliyoipitisha kwamba lazima kila halmashauri watenge fedha lakini bado jibu halipo. Halmashauri hazifikishi fedha kwa walengwa, fedha za mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum haziendi ipasavyo. Naomba Wizara walichukue na waliangalie kwa jicho la kipekee ili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna jambo tofauti, kuna baadhi ya Wakuu wa Mikoa wanashindwa kuelewa kwamba wao ni sehemu ya zile halmalshauri, wanadhani halmashauri ipo peke yake na wao wako peke yao. Kuna muda wanapoitwa utashangaa Mkuu wa Mkoa anawaambia halmashauri wajibikeni wakati ule ni uwajibikaji wa pamoja, wanajihisi wao siyo sehemu ya zile Halmashauri. Kuna baadhi ya Wakuu wa Mikoa wanafurahi wanapoziona halmashauri zinafanya vibaya na kuzitia madoa wakati wao ni sehemu ya halmashauri zile kufanya vibaya. Kama utapata muda itisha mkutano wa pamoja, Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi, wajue wanaisimamia Serikali ndani ya mkoa wanapaswa kwenda pamoja kwa faida ya wananchi na siyo kujinufaisha wao na kutengeneza migogoro ndani ya mikoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie suala zima la elimu, Wabunge wengi wamechangia, liangalie lilivyokuwa la pekee, kila Mbunge anayesimama kwa namna yoyote ile lazima ataigusa elimu. Kuna shule ndani ya Tanzania hii mwalimu yupo mmoja na tatizo ni dogo tu linaweza likapata ufumbuzi, kuna njia rahisi za kupata ufumbuzi. Kuna walimu unawapeleka Liwale, mwaka juzi nilichangia na hili nililizungumza, unamchukua mwalimu wa Dar es Salaam, mtoto aliyezaliwa Dar es Salaam unampeleka Liwale anashindwa kufanya kazi lakini Liwale ileile kuna walimu wanaomba nafasi zile hawapewi nafasi za kufanya kazi na wapo tayari kuisaidia Liwale, wapo tayari kusaidia eneo lao. Unamchukua mtoto wa Kahama unaenda kumpeleka Tanga akafanye kazi, uwezo wa kusema tunamtafutia nyumba hatuna, uwezo wa kusema tunamtafutia usafiri hatuna, unapomuacha kwao Shinyanga afanye kazi atakaa kwa mzee wake na kula ataisaidia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri Wizara itengeneze njia mbadala za kusaidia Serikali. Mheshimiwa Ummy Mwalimu kati ya watu niliofurahishwa na hii nafasi uliyopewa mmoja mimi, naamini utachukua maoni yetu na kuyafanyia kazi. Suala la kuwapangia walimu waende kwenye sehemu sahihi halihitaji fedha wala bajeti bali linahitaji mpango na mpango wenyewe ni rahisi. Mchukue watoto ndani ya mkoa husika wanaotaka kufanya kazi sehemu ile wapeni nafasi wafanye kazi, tuache mambo haya yanayoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la elimu, kero yangu nyingine kubwa inayonisumbua ni kuhusu vibali. Nadhani halmashauri ndizo zinazotoa vibali kwa nini mpaka leo Tanzania tunatoa vibali vya kuanzisha bar na shule iko hapo hapo? Tunatengeneza nini? Tuangalie hatuwajengi watoto wa Tanzania bali tunawabomoa. Unapotaka kutoa kibali cha bar angalia mazingira husika, unampelekeaje mtoto bar na shule ipo hapo hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi/Vigelegele)