Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia katika Ofisi hii ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kabla ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye ametujalia uzima hata leo tukawa kwenye Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze sana, nikianza na Mheshimiwa Waziri mwenyewe, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii ya TAMISEMI, kwa sababu wanaitendea haki Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengi wamezungumza habari za TARURA. Ni kweli TARURA ndiye mkombozi mkubwa kwa sekta ya uchukuzi na mawasiliano katika maeneo yote vijijini na asilimia kubwa ya Waheshimiwa Wabunge hapa tunatoka majimbo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie kuhusu TARURA kwa sababu kwanza kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amesema TARURA ina kilometa 108,946, lakini fedha wanayopata TARURA kwa mwaka wa 2021 ni shilingi bilioni 275.03, sawasawa na asilimia 35 tu ya uhitaji wa bajeti nzima ya TARURA. Ili TARURA iweze kusimama, lazima iwe na zaidi ya shilingi bilioni 700 ambapo tunaweza tukakarabati kilometa hizi 108,946. Kwa bahati mbaya sana, fedha zinazotolewa hadi sasa zimetolewa bilioni 172.85, sawa na asilimia 63 ya fedha zote bilioni 275 na bado kuna utofauti wa bilioni 102.8. Kwa vyovyote vile kwa hali ilivyo katika majimbo yetu mengi vijijini hayapitiki na ni mvua zinaponyesha sana kila sehemu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niiombe sana Wizara, Mheshimiwa Waziri pamoja na Serikali nzima, ione umuhimu wa kuongeza fedha katika sekta hii ya TARURA. Watendaji wake wote wanafanya kazi nzuri sana akiwemo CEO wao pamoja na watendaji wengine, licha ya kwamba kuna upungufu mdogomdogo ambayo mimi naweza nikayasema. Kwa mfano, maamuzi mengi yanafanyika mikoani, tunatamani ifanyike transformation TARURA, kwamba badala ya maamuzi mengi kufanyika mikoani, basi yafanyike ngazi ya halmashauri, ngazi ya wilaya ambako ndiko wataalam wapo. Kwa sababu sasa hivi barabara nyingi zinaharibika vijijini, lakini anayefanya maamuzi yuko mkoani ambapo mkoani kule barabara ni nzuri. Kwa hiyo kunakuwa kuna delaying technique ya kufanya barabara hizi zisitengenezeke kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano rahisi tu ni Jimbo langu la Busokelo. Busokelo kule mvua tunapata kwa mwaka mzima, zaidi ya milimita 2,000 kila mwaka, tunapumzika mwezi Septemba pekee. Ukipumzika mwezi Septemba tafsiri yake bajeti tunazopitisha hapa Bungeni, tarehe Mosi, Julai zinatakiwa zianze kutangazwa tenda, lakini zinakuja kutangazwa mpaka mwezi Novemba ama Desemba. Kwa hiyo utakuta kipindi cha kufanya procurement system zozote zinakuwa ni muda mrefu sana na wakati utekelezaji wake unakuwa kipindi cha masika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana mara tu Bunge likipitisha fedha za Serikali, manunuzi yaanze mara moja badala ya kusubiri kufikia mwezi Desemba ama Januari ambapo barabara nyingi zinakuwa zimeharibika na zinakuwa zimekata mawasiliano katika kata mbalimbali, kitu ambacho hakikubaliki kwa ulimwengu wa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizungumzia TARURA unazungumzia pia mifumo inayotumika katika manunuzi. Kuna Mfumo mmoja unaitwa TANePS, huu mfumo umekuwa ni changamoto kubwa sana, unasimamiwa na TCRA. Unaweza ukasajili wewe mkandarasi ama Engineers ambao wanakuwa kwenye huo mfumo, lakini matokeo yake baadhi ya passwords, tenda na documents kwenye huo mfumo, zinapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo utakuta inachukua muda mrefu sana mpaka tena huo mfumo usimame ili kuweza ku-process manunuzi hayo. Kwa hiyo nitoe wito na ushauri kwa Serikali kwamba kama inawezekana huu mfumo uweze kuwa revised badala ya jinsi ulivyo hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara moja kwa wastani ni kati ya shilingi milioni 25 mpaka milioni 30, lakini kwa sasa barabara moja ya TARURA inatengenezwa kwa shilingi 2,524,461 kwa kilometa, hiyo ni shilingi lakini kwa kilometa moja. Wakati wenzetu wa Road Fund kupitia TANROADS wao ni zaidi ya fedha hizi. Kwa vyovyote barabara zetu hazitaweza kutengenezeka vyema kwa uwiano huu ambao tuko nao mpaka leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa lililopo hapa tuna kitu tunaita data backlog maintenance, maana yake inahitaji barabara nyingi zitengenezwe kipindi cha mvua, kitu ambacho siyo rahisi. Kwa hiyo inabidi zitengenezwe kipindi ambacho siyo cha mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kupitia TARURA hii kuna asilimia 30 ambazo Waheshimiwa Wabunge inawezekana wengi tunafahamu, wengine hatufahamu, ambazo ni maalum kwa vikundi, tunaita special groups, maana yake vijana, wenye ulemavu, wazee na wanawake ambayo kila bajeti ya TARURA lazima kuwe na asilimia hizo 30, lakini ni halmashauri chache sana zinazotenga fedha hizi ili kuviwezesha hivyo vikundi kupata fedha, lakini si tu kupata fedha, vifanye kazi za TARURA kwa asilimia 30. Kwa hiyo nisisitize kwa Mheshimiwa Waziri kwamba hili pia ni muhimu kulisimamia katika Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TAMISEMI ina mifumo mingi sana. Nilikuwa naorodhesha mifumo hapa, iko zaidi ya mifumo 14 na mifumo yote hii inaisaidia TAMISEMI. Hata hivyo, mifumo hii haitakuwa na maana sana kama gharama za kiuendeshaji zinakuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niishauri Wizara kwamba kuna haja ya kupunguza mifumo ambayo iko TAMISEMI na wakati mwingine inakuwa ni redundant kwa maana kwamba mingine haifanyi kazi ipasavyo. Kuna kila sababu ya kuanzisha mfumo ambao uta-integrate na hii mifumo iongee, iwasiliane, ndipo tutakapoona haja ya kuwa na mifumo hii. Kwa hivi sasa ilivyo ni mifumo mingi sana na inatengeneza gharama kubwa kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza habari za TARURA, wamezungumza habari za malipo kuchelewa, wamezungumza habari nyingi, lakini tukiwa na mfumo mmoja ambao huo utakuwa chini ya Kitengo cha Monitoring and Evaluation, maana yake M&E ambao kila bajeti tunazopitisha hapa utakuwa na component ya kila mradi.

Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge popote utakapokuwa, awe kiongozi yeyote ngazi ya wilaya ama mkoa ama Taifa, una uwezo wa ku-trace back mradi wako na hata ukajua progress, ukajua kama bajeti imetolewa ama haijatolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii hatuna mifumo hii ndiyo maana CAG anapokuja na taarifa zake utakuta fedha nyingi zimeshapotea wakati tulikuwa na uwezo wa kufanya monitoring and evaluation kwa maana ya ufuatiliaji na tathmini kabla fedha hizi hazijatolewa. Nitoe wito, kwa sababu monitoring and evaluation kila mradi ukiwa nayo, hakika tutafikia malengo yetu kama Wabunge. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)