Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Alice Karungi Kaijage

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nianze kwa kumpongeza Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote ambao Wizara zao ziko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Watendaji na Wajumbe wa Kamati wote wanaohusika na Wizara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Serikali, kwa maana ya kupambana na masuala ya HIV/AIDS mahali pa kazi, pia kuna mipango mingi sana ambayo imeendelea kutekelezwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuendelea kupambana na masuala haya sehemu za kazi. Kuna mpango unaoitwa Mpango wa Utatu unaoshughulikia masuala ya HIV/ AIDS mahali pa kazi. Mpango huu umekuwepo toka mwaka 2008. Kwa hiyo, nashauri kama inawezekana, mpango huu ufanyiwe tathmini kwa jinsi ambavyo umefanya kazi kwa nia njema tu ya kuuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala zima la zile Kamati za UKIMWI mahali pa kazi pamoja na elimisharika. Naishauri Serikali ifanye usimamizi mzuri, Kamati ziwe active mahali pa kazi. Zitasaidia wale waathirika watoe hali zao za afya yao kwa waajiri wao wawe wawazi wapate huduma, lishe, wapunguziwe majukumu ya kiutendaji mahali pa kazi kama ambavyo Mwongozo wa Utumishi wa Umma Namba 2 wa 2006 unavyoelekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ila suala la saratani ya mlango wa uzazi, linahusiana sana na suala la HIV/AIDS kwa akina mama. Kwa sababu, ugonjwa huu asilimia 70 unasababishwa na mdudu anaitwa Papillomavirus 15 and 16. Pia sababu kubwa sana ya ugonjwa huu au virus hao kuambukiza ni kwa kujamiiana kwa njia ambayo siyo salama kama ambavyo UKIMWI kwa asilimia kubwa unaambukiza. Tumeona katika kituo cha huduma kule Tunduma, wanawake wamefanyiwa vipimo hivi 2900, kati yao 70 wamekutwa na viashiria vya saratani ya mlango wa uzazi na kati yao 43 wamepelekwa kabisa kwa maana ya rufaa kupimwa.

Mheshimiwa Spika, pia pale Mbeya kati ya wagonjwa nane waliopimwa saratani ya mlango wa uzazi ambao ni waathirika na wasio waathirika, sita wamekutwa ni wale waathirika, kabisa wana saratani ya malngo wa uzazi, wawili ndio sio waathirika. Kwa hiyo, unaona jinsi ambavyo hivi vitu vinaoana. Tunashauri Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hivi vituo vyetu vinavyohusika na masuala ya HIV/AIDS waongezewe sehemu ya kufanyia upembuzi wa saratani. Najua Serikali inafanya sehemu nyingine, lakini pia huku tunawapata wagonjwa mapema. Hawa wamama wakipatikana mapema, tiba yao ikiwa mapema wanapona kabisa.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu Tume ya Udhibiti wa Biashara na Matumizi ya Dawa za Kulevya. Chombo hiki kimeendelea kutoa elimu ya biashara ya dawa za kulevya kama ambavyo inaonekana katika sheria yake Na. 5 ya Mwaka 2015. Naungana na wenzangu wengi ambao wamesema jamani chombo hiki kitengewe fungu la maendeleo. Kwa nini? Kitengo hiki, mbali ya uraibu, hawa sasa hivi wana changamoto kubwa sana ya kupata magonjwa ya afya ya akili yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, tumeona pale Gereza la Ruanga, Mbeya, wametenga wodi moja kabisa kwa ajili ya wafungwa na mahabusu ambao wamepata magonjwa ya afya ya akili kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, ninasema waongezewe fungu la maendeleo Na. 2 kwa sababu gani? Wanakuwa na wigo mdogo sana kwa ajili ya huduma ya utengamano wa tiba kwa hawa waraibu. Hii inaathiri sana kasi yao ya matibabu. Pia, nasema watengewe kwa sababu kiliniki za urahibu ambazo ziko mpaka sasa hivi ni chache kutokana na fungu dogo kwenye chombo hiki cha kudhibiti UKIMWI, lakini imeonesha matokeo chanya sana. Kwa sababu hawa waraibu wameimarika, wamekuwa na afya bora na pia wanapata huduma ya magonjwa ambatana, kama vile magonjwa ya UKIMWI, magonjwa mbalimbali ya zinaa na TB. Hawa waraibu ambao wana-attend kliniki ambazo ni chache, haya matatizo yamepungua miongoni mwao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nakushukuru.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Alice Kaijage. Kabla hujakaa, Mheshimiwa unajua Kiswahili kigumu; waraibu ni watu gani?

MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, waraibu ni wale ambao wameathirika na madawa ya kulevya ambao wako kwenye matibabu ya Methadone. Ahsante. (Makofi)