Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi angalau kwa muda huu mfupi ili niweze kuchangia machache niliyonayo katika hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la elimu ambapo nitaongelea kuhusu ajira za walimu. Tunatambua na Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema hapa kwamba kuna uhaba mkubwa sana wa walimu katika shule zetu. Jambo ambalo nataka kuongelea ni namna ajira za walimu zinavyotolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ajira za walimu hazizingatii mwaka wa kuhitimu. Inashangaza wakati mwingine mwalimu amemaliza chuo mwaka 2015 lakini anaajiriwa mwalimu aliyemaliza mwaka 2019. Kwa hiyo, kuna gap kubwa hapa na linafanya walimu wengine wakae mpaka wazeeke wafike miaka 45, kwa hiyo hawataajiriwa tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali kwamba katika kuajiri walimu, mwaka wa kuhitimu uzingatiwe; na ikiwezekana Wizara ya Elimu au kama ni TAMISEMI wafanye research waone ni walimu wangapi ambao wataajiriwa kutokana na mwaka wao wa kuhitimu. Wako waalimu ambao wana vigezo, maana mwalimu aliyemaliza mwaka 2015, ametoka chuo na yule aliyemaliza mwaka 2019 wana vigezo sawa, wametoka vyuoni. Kwa hiyo, unapoajiri wa mwaka 2019 na ukamwacha wa mwaka 2015 kwa mfano;Je, huyo ataajiriwa lini? Kwa umri wake, anaendelea kukua na mwisho atashindwa kuajirika kwa sababu atakuwa amevuka miaka 45.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili ni kuhusu afya. Ni kweli mimi sijakataa, hata kwenye kampeni zangu sijakataa majengo ya hayakujengwa. Majengo ya zahanati yapo, tunachopaswa kuangalia ni je, katika majengo yale kuna nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule kwetu na hasa kwenye Jimbo la Bukoba Vijiji; nita-cite Bukoba Vijijini kwa sababu ndiyo kule kule ambako nimegombea mimi. Unapogombea, inakupa nafasi ya kujua watu wale ambao unataka kuwaongoza wamekaa namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukosefu wa madawa upo, ukosefu wa wafanyakazi upo, lakini mimi nataka kujua hizi gharama za wananchi wanazolipia wanapokwenda kwenye matibabu katika zahanati hizi, ndiyo hoja yangu ya msingi. Napenda kujua haya maelekezo ya hivi viwango ambavyo nitavitaja saa hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke anapopata mimba, nasemea Bukoba Vijijini na mahali pengine kama mpo mnasikia, kwamba ili uweze kuandikishwa siku ya kwanza ya kuanza clinic, unapaswa ulipe shilingi 10,000/= na ulipie shilingi 2,000/= ya daftari. Maana yake Serikali hii wameshindwa hata kile cheti cha clinic cha mwanamke cha kwenda nacho. Kwa hiyo, unapaswa ulipe shilingi 12,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, wanawake wanapokwenda kujifungua wanalipa kuanzia shilingi 30,000/= na kuendelea. Kwa hiyo, nataka kujua, hivi vigezo au hizi gharama nani alizipitisha? Maana yake ukienda ndani ya Halmashauri wanakwambia kuna Waraka. Ukiomba Waraka, wanasema hatutoi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu maana hili jambo msilifanyie mzaha linaumiza watu huko vijijini, wanawake wanajifungua ndani ya nyumba zao, wanakwepa hiyo 30,000/= kwani ni pesa nyingi. Ina maana tunataka kuwaambia watu waache kuzaana na dunia isiongeze, kwa sababu unapomchaji siku ya kwanza kwenda kliniki, huwa najiuliza hayo malipo ni kiingilio? Sasa nataka kujua hivi vigezo nani aliviweka na ni Wizara ipi, ni TAMISEMI au ni Wizara ya Afya? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimesikia kengele imegongwa, mambo mengine tutakutana huko TAMISEMI. (Makofi)