Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika mada hii muhimu ya Mpango uliopo mbele yetu. Kwanza napenda nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Mipango kwa kutuletea Mpango huu mzuri sana. Wapo wachangiaji takriban 10 waliochangia eneo hili, lakini kwa sababu ya muda, nitaeleza kwa ufupi maeneo machache sana.

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla tumeamua kujenga uchumi wa viwanda. Ili tuelekee kwenye uchumi wa viwanda, jambo muhimu sana ni kuwa na umeme wa kutosha, unaotabirika na wa gharama nafuu. Nimeanza na jambo hili tuone ili tunapoelekea tuko namna gani. Nianze na suala la kuzalisha umeme mchanganyiko ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumza kwa kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, hoja iliyoko mbele yetu hapa tunaweka kipaumbele gani. Mpango wa Serikali yetu ni kuzalisha umeme mchanganyiko na ndio mpango tulionao kwa kutumia vyanzo vyote tulivyonavyo ili kujiridhisha tunapata umeme wa kutosha, unaotabirika, wa uhakika na wa gharama nafuu.

Mheshimiwa Spika, tumeanza kuzalisha umeme hapa nchi toka mwaka 1964 katika mtambo uliopo Hale-Tanga wa megawatts 21.5. Tukaja Mradi wa Nyumba ya Mungu, nao bahati nzuri upo Tanga, maporomoko ya maji wa megawatts nane; baadaye tukaja Mtera karibu na hapa Dodoma, megawatts 80 mwaka 1980. Kwa hiyo, toka miaka hiyo, toka ukoloni mpaka mwaka wa 2000 tulikuwa tunatumia umeme wa maji. Baadaye miaka ya 2000 tulianza kutumia umeme wa rasilimali ya gesi asilia. Hapo kwa umeme tulionao hapa nchi ambao ni zaidi ya megawatts zaidi ya 1,601 asilimia 62 ya umeme tulionao kwa sasa unatokana na rasilimali ya gesi. Kwa hiyo tunaitumia gesi kwa sasa kwa kiasi kikubwa kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hoja ya kwamba pengine hatufuati sana vyanzo vingine haipo. Tunazingatia vyanzo vyote kuzalisha umeme ilimradi uwe umeme wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu. Kwenye rekodi tulizonazo umeme wa gharama nafuu kabisa kuliko vyote ni wa rasilimali ya maji. Ili uzalishe megawatts moja ya umeme wa maji unahitaji Shilingi 36 tu basi, fedha ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeme wa pili unaofuata kwa gharama nafuu, ni umeme wa nyuklia Shilingi 65 peke yake unapata unit moja ya umeme. Unaofuata kwa bei ya chini ni umeme wa solar pamoja na upepo unaohitaji Shilingi 103 kuzalisha unit moja. Umeme unaofuata kwa bei ya chini naomba mnifuatilie vizuri unafuata pia umeme makaa ya mawe ambao ni Shilingi 118 kwa unit. Umeme unaofuata ni umeme wa joto ardhi ni Shilingi 119 hadi 120. Umeme unafuata ni Shilingi 147, umeme wa rasilimali ya gesi Shilingi 147 kwa unit; na umeme wa mwisho ni wa mafuta mazito Shilingi 546 kwa unit. Nimalizie kusema, lazima mwisho wa siku umlegezee mzigo mwananchi wa kawaida na huu ni umeme wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nilipongeze Bunge lako Tukufu,mwaka jana, mwaka juzi na mwaka huu kwa kukubali kutekeleza Mradi mkubwa wa Julius Nyerere utakaozalisha megawatts 2,115. Hata hivyo, haina maana kwamba hatuzalishi miradi mingine, tunaendelea kuzalisha umeme wa gesi na hivi sasa tuna mpango wa kuzalisha megawatts 300 kule Mtwara; megawatts 330 kule Somanga Fungu na tunaendelea kuzalisha megawatts 185 Kinyerezi one extension na miradi mingine.

Mheshimiwa Spika, kwa Mradi huu wa Julius Nyerere ambao utatupa megawatts 2,115 ambao kama nilivyoeleza gharama yake ya kuujenga ni nafuu kuliko miradi mingine, maana yake tunakwenda kupunguza gharama ya umeme kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze jambo moja; kwanza napenda nitoe taarifa, mradi unaendelea vizuri na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu juzi aliutembelea, nisingependa kumsemea lakini aliona mradi unakwenda vizuri na sisi tutaendelea kutembelea hadi ukamilike.

Mheshimiwa Spika, China ambayo ndio anaongoza kuwa na mradi wa kuzalisha umeme duniani, kuna mradi mkubwa wa maji unaozalisha megawatts 22,160, mradi mmoja. Kwa hiyo naomba nisisitize kwamba pamoja na mambo mengine, pamoja na kuzingatia umeme mchanganyiko, lakini pia twende kwa vipaumbele vinavyolenga kweli kujenga uchumi wa viwanda wenye gharama nafuu. Bado narudia, tunatumia vyanzo vyote ndio maana nimesema kwamba rasilimali ya gesi tutaendelea kuzalisha miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo matumizi mengine mazuri sana kwa miradi ya gesi pamoja na kuzalisha umeme katika mradi wa gesi, gesi pia inaweza ikatumika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vingine; kutengeneza mbolea, kujenga viwanda vya Ngozi, viwanda vya vyuma na kadhalika. Kwa hiyo matumizi ya rasilimali ya gesi bado yapo palepale. Sio rasilimali ya gesi tu nimetaja vyanzo vingine ndio maana tunakwenda kuzalisha umeme wa upepo na jua na uko mpango wa kukamilisha mradi huo mwakani Julai utakaozalisha megawatts 1,100 kwa hiyo vyanzo vingine tutaendelea kuvitumia. Langu la msingi hapo kutoa taarifa hii Bungeni, nitaeleza kwenye mpango na bajeti yetu muda utakapofika, lakini leo nimeona niliweke jambo hili sawa ili Watanzania tujue tunakoelekea.

Mheshimiwa Spika, katika miradi hii ambayo nimeitaja hapa, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba, vyanzo vyote ambavyo viko kwenye mpango wetu vinatumika kuzalisha umeme kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, tutakapozalisha mradi huu wa Julius Nyerere tutakuwa na takribani megawatts 4,887 hapo mwakani mwezi Juni. Kwa hiyo umeme utakaobaki mahitaji yetu, mwakani tutahitaji umeme takribani megawatts 2,001. Kwa hiyo umeme utakaobaki takribani 2,102 tutaweza kuwauzia majirani zetu pia na kuingiza fedha nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nitoe taarifa, kwa sababu mradi huu na naomba nisali mbele yako, mradi huu ukamilike na nina uhakika utakamilika. Tarehe 15 Novemba, 2021, kabla ya saa kumi na mbili jioni tunaanza kujaza maji kwenye bwawa letu ili tuanze kupata umeme wa kutosha. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nimeona nilieleze vile jambo hili.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nishati, Spika hajakusikia bado umesemaje?

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Tarehe 15 Novemba, 2021, kabla ya saa kumi na mbili jioni tunaanza kujaza maji kwenye bwawa letu, kuelekea kwenye kupata umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwenye suala hilo. Naomba niishukuru sana Serikali, hadi sasa katika mradi huo tumeshalipa trilioni 2.04, ambayo ni sawa na asilimia mia moja ya mahitaji ya malipo yanayotakiwa kulipwa kwa Mkandarasi. Naipongeza Serikali kwa sababu hatujachelewa kulipa na tunayo matumaini tutaendelea kumlipa fedha ipo na mradi utakamilika kwa wakati. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye suala la matumizi ya gesi Mtwara, jambo ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwa kweli napenda kwa hekima ya pekee niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara na Lindi kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rasilimali ya gesi tuliyonayo kwa sasa tunazaidi ya trilioni 57.54 na maeneo makubwa sana tunayotumia ni kwenye kuzalisha umeme lakini tumeanza kutumia pia kwa matumizi ya nyumbani. Kwa Mtwara peke yake, kama nilivyowapongeza Waheshimiwa Wabunge, Mtwara tuna mitambo 13 ya kuzalisha umeme wa gesi. Na umeme wa gesi kwa Mtwara ambao ni megawati 30.45 wakati mahitaji yao ni megawati 15, tunayo ziada ya umeme kwa Mtwara na Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara na Lindi kwasababu wametuhamasisha sana kwamba umeme wa gesi unatumika. Lakini gesi hiihii inatumika kwa sababu suala la msingi ni hii gesi inatumikaje kwa Mtwara. Tumeanza kutumia gesi, na mpaka sasa tumetumia trilioni 0.053 kwa ajili ya kuwasambazia gesi nyumbani wnanachi wa Mtwara na maeneo ya Lindi.

SPIKA: Ahsante sana.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwamba tutaendelea kutenga gesi kwa ajili ya kutumia nyumbani.

Mheshimiwa Spika, kwasababu ya muda, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)