Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Prof. Adolf Faustine Mkenda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rombo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nitangulie kusema kwamba naunga mkono hoja na kwa vile ni mara yangu ya kwanza kabisa kuzungumza kwenye Bunge lako Tukufu, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Chama Cha Mapinduzi na wapiga kura wa Jimbo la Rombo wa kuniwezesha kuwa Mbunge kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameniamini kwa kunifanya kuwa Waziri wa Kilimo. Shukrani pekee ninazoweza kumpelekea ni kwamba, nitafanya kazi wa bidii, maarifa na juhudi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imepitia kwenye simanzi kubwa sana kwa kuondokewa na Mheshimiwa aliyekuwa Rais wetu, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, lakini tunamshukuru Mungu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametusimamia vizuri, tumeendelea na msiba vizuri ametufariji na kuleta matumaini makubwa sana kwenye nchi yetu. Tunamshukuru sana, tuendelee kumuunga mkono.

Mheshimiwa Spika, kilimo kimezungumzwa sana katika mjadala wa Waheshimiwa Wabunge na masuala yaliyozungumzwa ambayo sitaweza kuyazungumzia yote, mengi tutayaona kwenye majibu ya bajeti yetu, ni umwagiliaji, zaidi ya Waheshimwa Wabunge 10; suala la mafuta ya kula, zaidi ya Waheshimiwa Wabunge saba; pembejeo za kilimo, Waheshimiwa Wabunge 12; huduma za ugani, Waheshimiwa Wabunge watano; utafiti, Waheshimiwa Wabunge wanne; masoko, Waheshimiwa Wabunge watano; sera kwa ujumla, Waheshimiwa Wabunge tisa, mazao na ushirika Waheshimiwa Wabunge 10.

Mheshimiwa Spika, ukijaribu kuangalia, sehemu kubwa wa yale yaliyozungumzwa ukiyatafrisiri yanazungumza kwenye umuhimu wa kuongeza tija kwenye kilimo. Yaani kuongeza kiasi cha mazao ambacho tunaweza kukipata kwa heka moja au kile ambacho tunaweza kukipata kwa juhudi ambazo tunazitoa. Kwa kweli hiyo inaendana sana na maudhui ya Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao moja ya term, flagship statement yake ni kujenga uchumi shindani. Hatuwezi kushindana kwenye mazao endapo gharama ya uzalishaji itakuwa kubwa sana, lakini kwa heka moja tunazalisha kidogo

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye mafuta ya kula kwa mfano changamoto yake, ni kwamba sisi gharama ya kuzalisha mazao yanayoweza kutuletea mafuta ni kubwa sana. Mchikichi kwa mfano, kwenye hekta moja sisi tunaweza tukapata mafuta tani 1.6, lakini wenzetu tunakochukua mafuta sasa hivi hayo Mawese Malaysia, Indonesia na kadhalika, wanapata tani 10 kwa hekta na hili ni suala la tija.

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla wake ukiangalia kwa sababu siwezi kuingia kwa detail sana, ukiangalia pato la Taifa letu lote, utaona kwamba kilimo kinachangia takribani theluthi moja tu ya pato la Taifa, lakini nguvu kazi inayoenda kwenye kilimo ni zaidi ya theluthi mbili ya nguvu kazi yote hapa nchini. Maana yake ni kwamba, juhudi zinazozafanywa na mkulima, zinaleta kipato kidogo sana katika nchi yetu tija ipo chini sana na hatuwezi kuingia kwenye ushindani bila kutatua tatizo hili. Kwa hiyo, changamoto kubwa kabisa ya kilimo ni kuhakikisha kwamba gharama ya uzalishaji zinashuka, maana yake ni kwamba na bei ya mazao ishuke, lakini kipato cha mkulima kiongezeke. Hiyo inawezekana tu endapo tunaweza kuzalisha zaidi kwa hekta moja na gharama zikishuka zitatusaidia kujenga viwanda na kuleta ushindani kwenye uzalishaji wa mafuta ya kula na kwenye kuuza kwa nchi za jirani ambazo tunashughulika nazo.

Mheshimiwa Spika, sisi tunachukua maoni yote ya Waheshimiwa Wabunge ambayo wameyatoa hapa ambayo ni mengi sana na tumeya-summarize. Mengine mazuri sana, tutayafanyia kazi, lakini niwape matumaini Waheshimiwa Wabunge baadhi ya vitu ambavyo tayari viko kwenye mchakato na tunaomba tutakapokuja hapa na hotuba ya bajeti na maombi ya fedha mtupitishie kwanza.

Mheshimiwa Spika, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia suala la utafiti. Tunaongeza fedha kwenye utafiti wa kilimo, kwa sababu bila utafiti hatuwezi kupata mbegu bora na hatuwezi kuwa na kilimo bora katika mazingira yetu. Kwa hilo moja tunaongeza na wataona na tunafanya hivyo kwa kuanzisha Mfuko wa Utafiti ambao tutaulezea hapa na vile ambavyo tutafanya.

Mheshimiwa Spika, katika utafiti tutalenga sana vitu viwili; kwanza mbegu, kupata mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya nchi yetu; na pili kilimo bora katika mazingira yetu. Katika suala la mbegu, tutajitahidi sasa kuzalisha mbegu nyingi kwa sababu kilio cha mbegu hata humu ndani ya Bunge lako Tukufu tumekisikia sana. Tunafanyaje? Mashamba yote ya ASA yaliyopo hapa tunayatengea fedha kwa ajili ya kufanya kilimo cha mbegu cha umwagiliaji ili tuhakikishe kwamba tutakuwa tunazalisha mbegu sio kwa kutegemea msimu wa kilimo, kwamba tunaendana na wakulima tunazalisha mbegu wakati tunazalisha chakula halafu zile mbegu tunasubiri mpaka mwaka ujao, lakini tuweze kuzalisha mbegu kwa mwaka mzima na kuzalisha mbegu za kutosha na hizo mbegu ziwe ni matokeo ya utafiti ambao utakuwa unafanywa na taasisi yetu ya utafiti kwa fedha ambazo tutaziongeza kama Waheshimiwa Wabunge watakavyosikia katika bajeti. Hilo tutalifanya pamoja na mambo mengine ya pembejeo.

Mheshimiwa Spika, suala lingine hata tukifanya utafiti, hasa upande wa agronomy, kilimo bora tunahitaji kufikisha matokeo ya utafiti kwa mkulima. Kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyozungumza ni muhimu sana kuimarisha shughuli za ugani hapa nchini, tuna kazi kubwa sana, kwa sababu namna fulani tumerudi nyuma katika eneo hilo. Maafisa Ugani wengi hawana usafiri, wanahitaji kutoa huduma kwa wakulima na namna ya kufuatilia utendaji wao haujawa mzuri sana, kwa hiyo tunafanya nini? Kwanza, tutanunua, tutakapoomba fedha hapa tunaomba mtukubalie, pikipiki 1500 kwa kuanzia, kwa ajili ya kuwagawia Maafisa Ugani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatenga mikoa mitatu ya kielelezo ya namna ya kufanya huduma za ugani kwa namna ambayo inaleta tija. Mikoa hiyo tunahitaja wakati tutakapo wasilisha hapo Bungeni. Tunaongeza juhudi za ufuatiliaji, kwa sasa hivi tuna kitu tayari kinachoitwa mobile kilimo. Kila Afisa Ugani ambaye tumemuunganisha naye anakuwa na simu anapomtembelea mkulima, anatoa taarifa na anatuwekea namba ya mkulima. Kwa hiyo tunaweza tukakaa ofisini hapa au kwenye halmashauri unampigia mkulima kumuuliza Afisa Ugani alivyokuja kulikuwa na shughuli gani na amekushauri nini.

Mheshimwa Spika, kwa hiyo tutalifuatilia hilo, tutaongeza sana hasa kwa hiyo mikoa mitatu ambayo tutaitaja siku hiyo kuhakikisha kwamba kweli tunafuatilia shughuli za ugani zinakwenda vizuri. Tutafufua na kuimarisha zile farmers’ fields schools, mashamba ya mfano, lakini kila Afisa Ugani hasa kwenye hii mikoa mitatu tutahakikisha na yeye ana shamba na tutamhudumia, tutamwezesha. Wakati tunamkagua utendaji wake tutaenda kuangalia na shamba lake likoje. Wakati kuna shamba la kielelezo katika eneo lake, tunataka kuhakikisha kwamba na yeye analima, anatuonesha anajua kitu ambacho anataka kwenda kuwashauri wakulima.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni pamoja na kuongeza huduma za kupima udongo kama zilivyosema hapa, kwa sababu matumizi ya pembejeo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, yapo mengi ya kusema, lakini kwa sababu ya muda, nashukuru sana na kama nilivyosema naunga mkono hoja. Tunaomba tukija kuomba fedha Bungeni zipitishwe. (Makofi)