Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Dr. Dorothy Onesphoro Gwajima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kutoa mchango wangu wa dakika hizi chache kuhusu wasilisho hili wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ijayo.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa shukurani zangu za pekee kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini niendelee kuhudumu kwenye Sekta hii ya Afya.

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Afya ni sekta ya huduma za jamii na mpango huu hauwezi ukatekelezeka kwa ufanisi mkubwa kama Taifa hili litakuwa na afya isiyo njema. Kwa hiyo, Sekta ya Afya tunatambua kwamba lazima tujikite kwenye masuala mazima ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukizwa na pale inapotokea watu wameumwa, waweze kutibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mjadala huu kwenye Bunge hili ukiangalia umepambwa na imani kubwa kabisa inayotutaka Sekta ya Afya tusimamie Bima ya Afya kwa wote. Natambua kazi kubwa iliyofanywa ya mchakato huu wa kuelekea kwenye Bima ya Afya kwa wote, nami nimeipokea, tuko kwenye hatua za mwisho kabisa za kuleta Muswada wa Sheria. Awali tulidhani ni Septemba, lakini tumeona hapana, hapa tulipo tumeongeza kasi mpaka salamu mle imebadilika. Tukiingia, “Bima ya Afya kwa Wote! Kazi iendelee!” Ndiyo badala ya habari ya asubuhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo ni kwamba, tupate ridhaa ya vyombo vyote vya Serikali kwenye hatua hii iliyofikia ya kuandaa rasimu wa Muswada wa Sheria ili Juni kwenye Bunge lako Tukufu tuje na huo Muswada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepata michango mingine mbalimbali, huu specifically ulikuwa umechangiwa na Mheshimiwa Josephat Kandege, Mbunge. Kwa hiyo, hili ndilo wasilisho letu kwenye hoja hiyo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, yeye alichangia kusema kwamba katika maendeleo haya, hawa wa Biomedical Engineers wanajifunza kwa vitendo ile internship yao kwa kulipa pesa, hatuwezi kuharakisha maendeleo ya matengenezo ya vitaa tiba vya kisasa tunavyovipata. Akaomba kwamba tuwapunguzie malipo. Nasi sekta yetu imefuta hayo malipo waliyokuwa wanalipa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia niongelee suala lingine lililochangiwa na Mheshimiwa Kandege kuhusu hatima ya maendeleo ya upatikanaji wa vifaa tiba nchini. Nitambue kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, kwamba mwaka 2018 mpaka 2020, shilingi bilioni 64 zimenunua vifaa tiba mbalimbali katika hospitali za kipigwa na katika Hospitali za Afya ya Msingi na bado zoezi hili linaendelea. Katika ngazi ya hospitali za kipingwa, tumeweza kutumia vifaa hivi vya kisasa kabisa kama LINAC na CT Simulators na vifaa vingine vingi, hadi tukapunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kutoka 164 kwa mwaka 2015/ 2016 mpaka wawili mwaka 1920/2020. Kwa hiyo, mwaka huu sasa tutawasilisha bajeti ya shilingi bilioni 229 ili kuendeleza kupata vifaa tiba hivi kuanzia ngazi zote za kibingwa mpaka huko chini. Tunaomba Bunge lako Tukufu lipitishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la watumishi. Watumishi bado ni changamoto na hapa tutawasilisha bajeti ya shilingi bilioni 144.9 tukiomba Bunge lako lipitishe ili tuweze kusogeza upatikanaji wa watumishi kwenye vituo mbalimbali vikiwepo hivi 487 vilivyojengwa kwenye ngazi ya Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja iliyochangiwa na Mheshimiwa Fatma Toufiq ya kuhusu namna gani tutaweza kuwafuatilia akina mama wajawazito waweze kujulikana wanapopata huduma ya Afya ya uzazi kuanzia kipindi cha mimba, wakati wa kujifungua na baada.

Mheshimiwa Spika, kwanza tumejenga hivi vituo kama nilivyovitaja hapo ambapo huduma zimesongezwa karibu yao na hospitali 102 za Halmashauri zimejengwa. Hapa tumemsikia Waziri, pacha wangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu Waziri wa nchi, TAMISEMI akisema kwamba amepewa maelekezo na Mheshimiwa Rais kuendelea kujenga hizo hospitali katika Halmashauri zilizobaki ambazo hazikujengewa. Yote hii ni mikakati ya kusogeza huduma za mama mjamzito ili aweze kuwa na ujauzito salama hadi kujifungua.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo tumebuni kitu kingine ambacho ni kanzidata, kwamba anaporipoti tu kliniki, ule wakati aliporipoti anaingizwa kwenye database, anafuatiliwa ili hata kama akipotea, tujue amepotelea wapi? Utekelezaji huu umeshaanza kutekelezwa Arusha, ambapo huko ndiko ameteuliwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Sichwale na tunaupeleka nchi nzima. Kwa hiyo, itakuwa ikishaingizwa pale, akipotea tu, mpaka VEO atuambie alipopotelea huyu mama, yuko wapi?

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa michango yote. Naunga mkono hoja, naomba kuwasilisha.