Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. David Mwakiposa Kihenzile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. DAVID M. KIHENZILE: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kushukuru kwa Mpango huu ambao umeandikwa vizuri sana. Nitajikita kwenye sekta moja tu ambapo nizungumzia mahusiano kati ya Mpango hu una Sekta ya Ujenzi. Kabla sijafika huko, labda nimnukuu mmoja wa waasisi wa Marekani aliyekuwa anaitwa Benjamin Franklin ambaye aliwahi kutuambia kwamba failing to plan is planning to fail, unapokosea kupanga, basi unapanga kushindwa.

Mheshimiwa Spika, niungane kwanza na mtangulizi mmoja aliyezungumza pale juu kwamba tuweke mfumo mzuri wa kufuatilia, je, tunayokubaliana hapa yanatekelezwa? Mambo ya kimkakati na yenye tija sana yanapewa uzito sawa na Wabunge tunavyopendekeza? Hilo nataka iwe kama angalizo.

Mheshimiwa Spika, ukisoma Mpango katika maeneo ya kipaumbele, eneo namba mbili linazungumza linasema; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji wa huduma. Pia ukienda kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wetu, kwenye malengo mahsusi, namba tatu anasema:

“Kujenga uchumi wa viwanda kama msingi unaoongoza mauzo ya nje ili kuimarisha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, SADC na Central.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Spika, tumekubali, tumeamua kujenga nchi ya viwanda. Lazima pia tunapotamka hilo tukubaliane, tunatamka viwanda kama theories au tunatamka viwanda kiutendaji. Nitajikita kwenye maeneo machache kama nilivyosema na pengine labda ningeshauri na Wabunge wakasome tafiti ya mtu mmoja anaitwa Peter Samuel Abdi ambaye anasema anahusianisha infrastructure na Industrialization, jinsi vitu hivi vinavyokwenda pamoja. Naomba nijikite kwenye ukanda wa viwanda. Kama tunataka nchi yetu twende kwenye viwanda na mwaka 2015 hapa wakati Hayati anahutubia alisema angependa kuona mwaka 2020, Sekta ya Viwanda itoe asilimia 30 ya ajira. Tulipofanya tathmini mwaka jana tukabaini asilimia nane inatokana na ajira kwenye viwanda. Hakuna anayejiuliza, hii asilimia 22 tumekwama wapi? Naomba niende kwenye kesi ya upande kwa mfano wa viwanda pale Mufindi.

Mheshimiwa Spika, pale Mufindi ikiwa inawakilisha sehemu zingine za nchi hii, maeneo ambayo yamejitenga yenyewe kuwa ya viwanda pale kuna viwanda karibu 10 na viwanda hivi viko kuanzia miaka ya 1961 vilianza. Vinalipa kodi zaidi ya bilioni 40 takriban, naweza kukutajia kwa uchache. Kuna Kiwanda cha Karatasi, hiki kinatengeneza karatasi hapa nchini kwetu na kupeleka nje. Kuna Viwanda vya Nguzo, kuna Viwanda vya Chai vimekusanyana pale. Sasa niwaombe wenzetu wa Sekta ya Ujenzi Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi yuko pale, Mheshimiwa Waziri wa Fedha yuko pale; maeneo kama haya ambayo wakiyakusanya yanaweza kuingizia Taifa bilioni 40, lakini tunayasoma kwenye takwimu pia kwamba katika miaka hii, kati ya viwanda 23 vya mbao peke yake, viwanda karibu 23 kati ya 27 vilikufa, hakuna anayejiuliza sababu ya kufa ni nini? Ningemwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake walifanyie tathmini jambo hili.

Mheshimiwa Spika, pia tunaposema tuimarishe Sekta ya Viwanda kama msingi wa kuongoza nchi yetu, tunamaanisha magari yanayopangana barabarani zaidi ya 200 kila siku kipindi cha mvua, yatapita kiurahisi, utasafirisha bidhaa zako kutoka kiwandani mpaka nje. Kumbuka viwanda hivi vinapeleka bidhaa ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu. Unahangaika kuanzisha viwanda vingine wakati vile vilivyopo mahitaji yake 50 ikiwemo barabara hujajenga, are we serious? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu, kwa kuwa agenda ya viwanda iliasiisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa kuwa, iliendelezwa na watangulizi wake mpaka Mheshimiwa Mama Samia sasa, Rais wetu wa Awamu ya Sita. Na kwa kuwa maeneo kama yale yametajwa kwenye Ilani ya CCM ninaomba tuyape kipaumbele ikiwezekana tuimarishe miundombinu yake, tujenge barabara, tupeleke umeme, tupeleke maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifanya siku moja ziara pale, unamkuta mwenye kiwanda anasema bwana mimi hapa kodi inayolipa ni dola milioni mbili karibu nukta mbili, lakini shida yangu kubwa tazama huko nje hali ilivyo mbaya, sina barabara, anakwambia lakini umeme hapa ndani hautoshelezi.

Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, kwa kumalizia. Kwa kuwa, maeneo kama haya yametajwa kwenye Ilani ya CCM kuanzia 2005 mpaka sasa. Kwa kuwa, Mwalimu Nyerere aliahidi. Kwa kuwa, Rais Kikwete alirudia, kwa kuwa, baba yetu hayati Dkt. Magufuli ameyazungumza tena mwaka jana. Namna nzuri ya kuwaenzi viongozi hawa ni kuanza kutenda kusema inatosha. Tutakuwa na mipango hapa, tunakaa hapa ndani tunazungumza utekelezaji hauonekani wa baadhi ya maeneo. Kimshingi maeneo ambayo sisi huku nje tunakuwa hatuelewi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inawezekana labda kuna maelezo mazuri kama kwa kutumia msemo wako. Kunaweza kuwa na maelezo mazuri sana ya kwamba, barabara hizi hatuwezi kuzijenga kwasababu hizi na hizi na hizi, lakini sisi hatuelewi. Eneo hili limeajiri watu karibu elfu kumi, eneo hili linalipa kodi zaidi ya bilioni 40, eneo hili magari yanayopita na ajira pengine, n.k. shida ni nini?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuhitimisha ninaunga mkono hoja, lakini naombeni maeneo ya kimkakati tuyatazame kwa njia ya kipekee. Ahsante sana. (Makofi)