Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami niungane na Wabunge wenzangu kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Spika, nimeusoma Mpango huu vizuri sana lakini kuna mahali ambapo sipaoni pametiliwa umuhimu napo ni sehemu ya afya. Suala hili la afya kwa sasa sisi Majimboni ndiyo suala ambalo ni gumu sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mwalimu Nyerere mpaka mwaka 1985 ilikuwa inatoa matibabu bure kwa raia wote wa Tanzania. Wakati huo tunafahamu vizuri labda tu kwa vijana, Serikali ilikuwa imefilisika baada ya vita vya Uganda lakini Serikali ilikuwa inatoa matibabu bure. Leo nikiangalia kwenye Mpango hakuna mahala ambapo panaelezea namna gani wananchi wetu wapatapa matibabu. Mheshimiwa Sunga ameeleza vizuri watu wetu kweli ni maskini na bei za matibabu na dawa mwananchi wa kawaida wa Tanzania hawezi. Namuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha afikirie kama anaweza kuongeza bei kidogo au shilingi 30/40 kwenye mafuta ili wananchi wetu tuwapatie matibabu bure. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nalisema hili kwa sababu leo tunakusanya shilingi trilioni 2 na waliotuchangia hizi shilingi trilioni 2 ndiyo hawa, ni sahihi kweli mwananchi akienda hospitali akiwa hana pesa hakuna kitu chochote anaweza kufanya matokeo yake anaenda kukabiliana na kifo. Ni sahihi sisi Wabunge wote tunatoka Majimbo ambayo yana matatizo makubwa sana, hakuna Mbunge ambaye ametumwa nyama au sukari na wapiga kura wake labda Mheshimiwa Gwajima Mchungaji Kawe kwa kuwa Jimbo lake ni zuri kidogo lakini sisi kwenye Majimbo yetu hali ya umaskini wa wananchi wetu ni mbaya. Kwa kuwa wananchi hawa hawana tatizo la nyama wala sukari, wanaipita nyama hapo wanaenda kununua mchicha bila hata malalamishi tatizo lao ni dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri ugonjwa ni kitu ambacho mtu hawezi akajisingizia. Sidhani kama hofu ya Serikali ya kutoa matibabu kuwa bure kama ina sababu ya msingi. Kwa sababu sidhani kuna nchi duniani ambayo iliwahi kutibu watu wake bure ikafilisika sidhani, haiwezi kufilisika. Duniani nchi zinafilisika kwa vitu viwili; ni vita na ujenzi, hakuna kitu kingine. Kwa mapato tuliyonayo, tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha afikirie ili tukawatendee haki wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hili tatizo la bima Mheshimiwa Waziri wa Afya yuko hapa, bima ni sawasawa na kamari. Tunaona Polisi kwa wachezesha kamari endapo mchezesha kamari ameliwa, akiwa hana pesa polisi wanakuja, vipi mtu aliye na bima anapokwenda hospitali anapoambiwa dawa hakuna kwa nini Mheshimiwa Simbachawene asipunguze traffic barabarani atuhamishie baadhi ya polisi hospitalini ili mgonjwa anapoambiwa na bima hakuna dawa aende akaripoti polisi. Kwa sababu traffic anahangaika na mtu ambaye hakufunga mkanda ana Landcruiser ambaye akimuona traffic anafunga akitoka anafungua lakini huyo ndiyo anakimbizana naye. Mheshimiwa Simbachawene tuhamishie baadhi ya traffic wawe hospitalini ili mtu akikosa dawa aende pale polisi ili anusuru uhai wake. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hapo ndipo panapohitaji usalama kabisa huku kwingine kote tunasumbuka. Usalama unahitajika pale mtu anapokuwa anaumwa, aende mtu polisi kawaida kama wanavyotetewa wacheza kamari itatusaidia. Sasa hivi simu zote tunazopokea Wabunge nusu ni kwa ajili ya dawa na matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwaombe pia wenzetu wa Wizara ya Afya, kwa nini hakuna regulatory kwenye hizi dawa na matibabu. Tuna EWURA kwenye maeneo ya mafuta, tuna TFDA na TBS, kwa nini kwenye dawa pana kigugumizi na wakati dawa ndiyo kitu cha muhimu na cha mwisho kabisa kwenye maisha ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, leo tumeshuhudia watu wana- charge dawa mpaka shilingi milioni 5, unaposema milioni 5 kwa mtu wa kawaida anazipata wapi pesa hizo. Vilevile tunaona sasa hivi ukiwa na bima ghafla wanakwambia tumeondoa hiki, wao ndiyo walipokea pesa, halafu wao tena katikati ndiyo walioamua kwamba ugonjwa huu tumeshauondoa na wewe umeugua na hauna kitu chochote, nafikiri hapo Mpango uangalie vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili la matibabu nafikiri hata mimi mwenyewe ningekuwa na maisha ya chini kule kijijini kwa hali iliyoko leo ni kitu kinahuzunisha sanasana. Tuwaombe Wizara ya Afya na yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri wa Fedha basi aruhusu hata bili za maji au bili za umeme ziwe dhamana ili mimi kama naumwa niende na bili yangu ya maji au umeme baada ya kupata ile hesabu ya hospitali wanigawanyie mle kidogo kidogo niwe nalipa pamoja na bili ya maji au umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naliongea suala hili kwa mapana kwa sababu hili suala linatusumbua sana. Unakuta mtu amepata matatizo unaambiwa kwamba huyu hana bondi ya pesa, hatuwezi kumtibu mpaka upate 300,000 za kuweka dhamana, je, huyo mtu anayesababisha kifo hiki kwa ajili ya pesa yeye siyo mhalifu kama wahalifu wengine? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna ubaya gani Serikali ikaweka utaratibu wa kukopesha wagonjwa kama inaona vigumu? Makampuni ya simu leo yanakopesha bila hata kumuona mtu mpaka shilingi laki tatu, Serikali yetu inaona ubaya gani kumkopesha mgonjwa matibabu? Atalipa tu maana tuna vitambulisho watu wote wanajulikana akopeshwe na baada ya mwaka kama itaona madeni yamekuwa hivi Serikali inaweza ikawafutia watu wake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hawa ndiyo wapiga kura wetu, haya mambo yote tunaongea kiingereza sijui nini, mimi naona shida kubwa. Kwa kuwa suala la elimu limeanza kujadiliwa, suala ambalo limebaki na mgogoro ni suala la afya. Tunaomba sana kwenye Mpango huu Mheshimiwa Waziri alifikirie sana. Tumeweka shilingi 50 kwa ajili ya maji tumeweka Sh.50 kwa ajili ya REA, afikirie kama anaweza kuweka hata Sh.30 kwa ajili ya afya. Wataalamu wa uchumi wanasema vitu au maisha yatapanda ni uongo. Bei ya nauli ya daladala leo ina miaka mitano haijawahi kupanda pamoja na bei ya mafuta kupanda, hata nauli za mabasi hazijawahi kupata, hata mafuta yakishuka hatuoni impact yoyote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba wenzetu wataalamu wa uchumi wasije wakalivuruga wakasema sijui maisha yatapanda, maisha yapi, maisha ya Tanzania …

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mnaona Maseneta wanavyo argue point, amekuja na issue yake leo ya afya na bima ya afya, dakika zake zote anazitumbukiza pale. Endelea Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli wataalamu wetu wa uchumi wasije wakaleta yale matarakimu yao ya kusema ooh maisha yatapanda, uchumi wa Amerika ukiongeza bei ya mafuta ndiyo unapanda uchumi wa Tanzania hauna hata mahusiano. Leo vijijini hata mafuta ya taa hakuna kuna solar kila kona, kwa hiyo, mtu asilete tena maneno ya uongo, hakuna. Hata kama mafuta ya taa yakipanda kule kijijini kibaba huwa hakibadiliki huwa kina bei ileile tu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha alifikirie kwani tutakuwa tumewatendea haki sana wananchi. Kweli tumejenga zahanati kila mahala lakini wananchi wanahitaji zahanati bila dawa? Maana kama mwananchi haponi, haoni thamani hata ya ile zahanati.

Mheshimiwa Spika, ni hofu bure tu, leo tunakopesha wanafunzi zaidi ya shilingi bilioni 600, kweli tunakataa kumkopesha mtu uhai? Ni suala ambalo Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatakiwa alifikirie kwa mapana kwenye Mpango wake. Hii itatusaidia sana na tutakwenda kule vijijini tukiwa kweli tuko huru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Majimbo yetu yale ya vijijini hawana shida ya nyama wala sukari. Sisi kwetu kijijini ukinywa chai wanakuuliza leo unakunywa chai unaumwa? Hawana tatizo, ni haya ya mjini ndiyo yenye matatizo lakini sisi hatuna tatizo la sukari hata wanashangaa tunapolalamikia sukari. Kwa hiyo, tunaomba Waziri wa Fedha atufikirie sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)