Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi ya kuchangia na mimi ningependa nijielekeze katika mambo mawili. Tunapozungumzia maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa tunahusisha ukuaji wa uchumi, na tunapohusisha ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa tunaongelea mambo ya msingi sita; yaani uendelevu, uzalishaji, uwekezaji, mashirikiano, usalama pamoja na usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa kwenye usawa ndipo ambapo ningependa nijielekeze kwasababu ni suala ambalo linahusisha haki na utu wa watu. Na tunapozungumzia maendeleo ya watu kwa kiasi kikubwa tunahusisha utu na haki za watu. Yaani lengo kuu la maendeleo ya watu ni uhuru na haki za watu; huwezi kutofautisha hayo masuala mawili.

Mheshimiwa Spika, nazungumza haya kwasababu uhuru na haki ya mtu unahusisha uhuru wa kipato. Tunapojadili mpango huu ni muhimu sana kuweza kuweka baadhi ya mambo sawa, ambayo yanashika uhuru wa kipato cha mtu; na uhuru wa kipato cha mtu mara nyingi unalindwa na Sheria na taratibu za nchi.

Mheshimiwa Spika, ningependa nijielekeze hapa kwasababu zipo Sheria ambazo zinakandamiza uhuru wa kipato cha mtu, inawezekana kukawa na changamoto, na hapa ningependa nijihusishe specifical katika Sheria ya Uhujumu Uchumi, nafahamu imeongelewa sana lakini ningependa niweke mkazo hapa. Kwa ambao hawafahamu Sheria hii ya Uhujumu Uchumi na Utakatishaji Fedha ilikuja baada ya tukio la Septemba 11; pale ndipo ambapo Sheria hii ilisisitizwe iweze kuletwa katika mataifa ya Afrika na dunia kwa ujumla, ndipo na hapo sisi tukapata sheria hii. Lakini tulipokosea nchi nyingi za Afrika pamoja na Tanzania tulipata mapokeo ya sheria hii bila ya kuangalia mazingira yetu ya ndani.

Mheshimiwa Spika, na vile vile tulipopata sheria hii hatari zaidi hatukuwa na uzoefu na kujadili ama kuendesha mashtaka haya, na hivyo tukajikuta tunapokonya haki za watu za dhamana, lakini vile vile tukapoka mali za watu kwa kudhania, kwamba sheria inaruhusu ilhali kimsingi ilikuwa labda ni tafsiri mbaya ya sheria ama sheria hazikukaa sawa ama matumizi mabaya tu ya nafasi pamoja na madaraka ya watu waliodhaminiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema haya kwa sababu makosa mengi katika sheria zetu za Tanzania yana dhamana; ukiangalia wizi, ukwepaji wa kodi ni makosa ambayo yana dhamana lakini ilivyokuja sheria hii dhamana ikanyimwa. Hata hivyo, watafsiri wetu wa sheria wametufelisha sehemu moja, makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha ni matokeo ya makosa ya msingi yaani leo hii umeiba ama unatuhumiwa kwa ukwepaji kodi, mpaka ukwepaji kodi uwe- establish ndipo pale utaweza kujua, je, ukwepaji kodi ulisababisha utakatishaji wa fedha? Ndipo hapo unamhukumu mtu kwa kosa la kuhujumu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu makosa haya ya utakatishaji wa fedha ni vigumu sana kuya-prove wenzetu wa DPP wakaamua warahisishe Maisha. Moja, kwa sababu ni ngumu sana ku-prove sasa wanaamua pale kwenye kosa lako la msingi ambalo lina dhamana akuwekee na money laundering ili likose dhamana. Pili, kwa sababu halina dhamana utawekwa rumande sasa pale ndiyo wanakuja na negotiations (pre-bargaining) anakwambaia sasa hapa kuna shitaka hili na kwa sababu mashtaka haya yana sifa ya kukukalisha rumande miaka na miaka, mtu uko frustrated unawaza biashara zako, unawaza familia yako, unamuwaza mke au mume wako utakosa ku-negotiate ili uweze kutoka? Uta-negotiate tu na hapo ndipo ambapo watu wanapokwa mali zao kwa taratibu ambazo siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema utaratibu huu ni unyang’anyi tu wa bila silaha, tunapokonya watu kwa taratibu ambazo zingeweza kutafsiriwa ili ziweze kurahisisha watu wetu walinde kipato chao na utu wao. Kwa hiyo, haya masuala ya hii sheria, naomba sana Serikali yangu sikivu iangalie upya na inawezekana sheria haina matatizo ila tafsiri ya sheria kwa watendaji wetu iangalie mazingira ambayo tutalinda utu na kipato cha watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo napenda nijielekeze nalo ni kuhusiana na masuala la mawasiliano na teknolojia. Inawezekana nikaonekana kama mlalamikaji lakini napenda nisisitize hapa. Kwanza napenda niishukuru Serikali yangu Sikivu, tulipozungumza masuala ya mabando ilisikia ikatoa maelekezo na tunashukuru sana. Hata hivyo, bado naomba Serikali iangalie masuala ya mabando ili wananchi waweze kujikwamua kiuchumi. Vijana wengi wanatumia huduma hizi, toka mwezi wa kwanza tunalalamika huu ni mwezi wa nne masuala haya hayajafanyiwa kazi, tunapewa tu matamko lakini vijana wengi zaidi ya milioni 23 wanatumia mitandao ya simu kwa ajili ya shughuli zao, tunaomba tuangaliwe. Unapewa MB 300 kwa Sh.2000 unafanya biashara, vijana huku ndipo tulipokimbilia kwa sababu mfumo wa elimu haujaweza kutusaidia. Sasa kwa mantiki kama hizi tunasaidiwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TCRA imetoa tamko kwamba ikifika Mei Moja vijana zaidi ya 90,000 wanaosajili line wawe wana vibanda, leseni na TIN namba. Anasajili line kwa Sh.1000 na anapata wateja kwa kusambaa huku mtaani leo hii unamwambia awe na kibanda wateja atapata wapi? Airtel inawalipa vijana hao zaidi ya shilingi milioni 700 ikilipa kima cha chini lakini inalipa mpaka shilingi bilioni 1 kwa vijana 30,000 lakini wanaenda kukosa kazi hawa. Naomba Serikali yangu iangalie mambo kama haya ili vijana wa Taifa hili wasiwe frustrated na mazingira ya kibiashara. Naomba Serikali yangu ituangalie sisi vijana ambao tunalipenda Taifa letu na tunafanya kazi kwa juhudi kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunivumilia na kunipa dakika za ziada. (Makofi)