Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwa maana ya mwaka 2021/2022 – 2025/2026.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri mapema kwamba mimi ni mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa hiyo, nimechangia mara nyingi katika maeneo mengi. Kwa sasa nitumie nafasi hii kuchangia eneo moja tu ambalo pia nilitumia nafasi kama hii kuchangia Mpango kwa mara kwanza mwezi Februari katika eneo la ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kutuwasilishia Mpango mzuri. Pia, nimpongeze Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti kwa jinsi ambavyo waliweza kutuongoza na kufikia mapendekezo hayo ambayo Waheshimiwa Wajumbe wameyaona. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huu una maeneo matano ya vipaumbele, lakini binafsi nitajielekeza katika eneo moja la kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Hapa yako mambo mengi ya elimu, afya na kadhalika lakini mimi nimebeba hili la ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasema sana juu ya eneo la ardhi na hasa upimaji, Mpango wetu ulieleza wazi nia yake ya kupima ardhi nchi nzima. Nia hii wala si mpya sana kwenye Mpango wa Tatu, ilikuwepo pia kwenye Mpango wa Pili. Nikikumbuka sana katika Mpango wa Pili tumeendelea sana kupima ardhi na hapa niipongeze sana Wizara ya kisekta kwa kufanya kazi nzuri sana kitakwimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tufahamu vizuri maana halisi ya kupima ardhi ni lazima tujue faida zake. Nitataja chache sana kwa sababu ya muda, tukipima ardhi maana yake tutatambua kisheria umiliki halali wa kipande kilichopimwa, kuongeza thamani ya ardhi, kuongeza usalama wa ardhi, kutumika kama dhamana na zaidi kuondoa migogoro kwa majirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, hizo zikiwa ni sifa chache sana lakini malengo ya upimaji katika kipindi kilichopita cha Mpango wa Pili tumepima vizuri sana. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 – 2019/2020 tumetoka katika upimaji wa karibu viwanja 74,000 mpaka kufikia viwanja 150,000 ni ongezeko zaidi ya nusu yaani mara mbili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mpango mzuri ambao upo sana ndiyo maana nina wasifia sana, katika kipindi hiki cha Mpango wa Tatu naona sasa wanaelekea kwenye kupima ardhi katika kiwango cha 300,000 mpaka 500,000 kwa mwaka, hili ni jambo kubwa sana. Zaidi nijielekeze na nilisema Februari nchi hii ni kubwa, ina eneo la ardhi kubwa sana lakini toka Uhuru tumeshapima asilimia 25 tu na najua malengo kwa miaka mitano ijayo itakuwa labda kwa ziada ya asilimia 100 maana yake ni mara mbili kufikia asilimia 45. Ni ukweli tukijielekeza sana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam ambao una watu zaidi ya milioni sita katika makadirio kati ya milioni 61 kwa nchi nzima, unaweza ukaona tuna idadi kubwa na tukiwekeza pale tunaweza tukapata tija sana ya kuinua watu wetu kiuchumi. Tukiinua watu hawa kiuchumi maana yake itaenda sambamba kwa maana ya multiplier effect katika maeneo mengine ambayo yatatusaidia sana kujiinua kiuchumi lakini vilevile kuongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima tuseme ukweli, nimepongeza kwa kiasi lakini ipo kazi bado haijafanyika na mimi muda mwingi naipima kazi ya sekta hii katika Mkoa wa Dar es Salaam vis a vis mikoa mingine na nipongeze sana. Trend ya mwaka 2015/2016 – 2019/2020 na hasa miaka miwili ya mwisho utaona Mkoa wa Dodoma vis a vis Mkoa wa Dar es Salaam, nilijaribu kupitapita kitakwimu nikakutana na kitabu kimoja cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri cha mwisho kwa sekta hii 2021, karibu kama ukurasa 170 unaweza ukaona viwanja vilivyopimwa 2018/2019 Dar es Salaam ni 25,490 lakini mwaka huo huo Dodoma imepima 71,571. Kwa mwaka uliofuatia 2019/2020 mpaka Aprili, Dar es Salaam tumepima viwanja 11,125, Dodoma 76,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ndipo ninaposhangaa. Ninashangaa kwa kuona kwamba bado hatujaamua kupima ardhi, tungeamua kupima ardhi hii haiwezekani eneo lenye watu milioni sita tunapima ardhi viwanja 14,000. Watu wenye watu takriban milioni mbili wanapima viwanja 70,000 mpaka 75,000. Hii imekuwa ni changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni ukweli pia katika mwaka 2017/2018, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aliwahi kutoa kauli moja nzuri sana juu ya kurasimisha ardhi nchi nzima. Jambo hili lilikuwa ni zuri sana kwa maana katika malengo yale niliyoyasema kama faida ya kupima ardhi utaona huko kuinua wananchi kiuchumi. Alitamani kuona maeneo ambayo yameendelezwa kiholela sasa basi watu waweze kupimiwa bila kubomolewa na baadaye hati zile ziwasaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mfano wa kawaida sana, Mkoa wa Dar es Salaam kwenye lile jambo la urasimishaji ambayo nikinukuu kauli ya Mheshimiwa Waziri aliyoitoa tarehe 23 Oktoba, 2017 alisema: “Hatutobomoa nyumba ya mtu bali tutaendelea na urasimishaji wa makazi kwa maeneo yaliyojengwa holela ili yawe makazi rasmi na wananchi wapelekewe huduma muhimu kama vile barabara, umeme na maji. Muhimu wapewe hati miliki ili ziwasaidie kiuchumi na waweze kulipa kodi ya ardhi, lakini nitazuia ujenzi mpya holela katika miji yetu kwa mujibu wa sheria. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi, tarehe 23 Oktoba, 2017”.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo hapa kwa kumalizia dakika zilizobakia. Kitakwimu, urasimishaji huu umekuwa donda kubwa Dar es Salaam kama sample ya nchi nzima. Dar es Salaam katika Wilaya ya Ubungo nikienda Jimbo la Kibamba kwenye Kata sita nabeba kata mbili tu, maana huko kwingine ni nyingi sana, katika kata mbili tu katika nia njema ya kupima ardhi hii ili itusaidie sana kwenda kwenye Mpango wa Tatu, katika makampuni yaliyosajiliwa, kwenye usajili, uthamini, wana mambo kama matatu hivi lakini viwanja vilivyotambuliwa na kupimwa kati ya viwanja 10,000 ndani ya kata moja ya Kibamba ni viwanja 3,000 tu ndiyo vimewekewa mawe, hati ni 20 katika kipindi cha miaka miwili na zaidi. Kata ya Mbezi, katika viwanja vilivyopimwa 33,000 hakuna hati hata moja katika kipindi cha miaka miwili na nusu Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, fedha ni zipi zimechangwa? Kwenye ile Kata ya Kibamba peke yake shilingi milioni 890 wakati Kata ya Mbezi ni shilingi bilioni 2.57, ukizijumlisha ni zaidi ya shilingi bilioni 3 zimechangwa na Watanzania maskini lakini mpaka sana hawajawahi kuona hati ndani ya kipindi cha miaka miwili, haya ni magumu hata kuyatamka. Leo tunasimama tunazungumzia Mpango uje utusaidie kwenda mbele katika kipindi cha miaka mitato 2021-2026. Kwa kweli lazima tuoneshe tuna nia njema kusema haya tunayoyasema ili tuyatende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili halijawahi kwenda sawa, tunatambua wakati tunapeleka urasimishaji upande mmoja watu wanaambiwa wachange fedha zao ili twende sawa wapate hati, kuna upande mwingine zaidi ya halmashauri 27 zimepewa zaidi ya shilingi bilioni 6 hadi 10. Tumeona Kamati ilikuwa Iringa juzi tu na ikakuta zaidi ya shilingi milioni 400 waliyopewa ile halmashauri wameshindwa hata kurejesha, ni revolving lakini wameshindwa kurudisha lakini hawa waliotoa hela zao zinaenda kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana jukumu la Wizara kwenye hili ni kutoa hati siyo makampuni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nitarudi kuongelea sekta hii vizuri sana. Nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)