Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Humphrey Herson Polepole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mimi naomba kuungana na Wabunge wenzangu kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa mwaka 2021/2022 na 2025/2026 na nitapenda kujikita katika maeneo manne kwa ufupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ni ukweli usiopingika ya kwamba ulimwenguni biashara ndogo ndogo, biashara ndogo na biashara za kati ndizo zinachukua asilimia kubwa ya uchumi ulimwenguni. Kwa lugha ya Kiingereza Micro small and medium enterprises ndizo ambazo zina-constitute most of the economies Ulimwenguni, na neno biashara, ukisema enterprises kama ni biashara, lakini nikisema enterprises inaweza kuwa kampuni ndogo enterprises inaweza kuwa mradi fulani wa uzalishaji enterprises inaweza kuwa shughuli ambayo mtu anaifanya kujiletea kipato. Nitatumia neno enterprises nikimaanisha kwa maana ya tafsiri hiyo pana.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wote waliofanikiwa ulimwenguni ma-bilionea ma-trilionea kwa mtindo huo wote walianza kama micro entrepreneurs ama unasema small entrepreneurs. Mimi ushauri wangu kwenye mpango, tujikite sana kwenye kuwezesha micro-small and medium enterprises kwasababu hawa ndio injini ya uchumi wowote na ikiwepo hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu za tangu mwaka 2010 micro small medium enterprises zilikuwa kama 2,700,000, kwa maana ya wale ambao wamezianzisha; lakini kwa sera yetu hapa Tanzania ukitazama tafsiri wanasema micro enterprises ni zile ambazo zinawamiliki chini ya watano halafu wale wanaokuwa small wanakuwa watano mpaka hapo mbele kumi, halafu wale wakubwa wanaanzia kumi na kuendelea mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa Tanzania watu wengi wanaosimama katikati ya ama mazao ya shambani na bidhaa inayokwenda kutumika nje ni hawa watu wa Micro small and Medium Enterprises. Iwapo tukiwawezesha vya kutosha hili ni eneo lingine kubwa sana la kikodi ambalo linaweza kuchangia vikubwa sana katika Pato letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotakiwa kufanyika, kwanza, ni kuwatambua watu hawa. Watu wengi katika eneo hili bado siyo rasmi wanasema ni informal sector lakini kimsingi ajira karibia zote, kwa takwimu za mwaka 2010 Micro, Small and Medium Enterprises peke yao walikuwa wana-constitute kwa zaidi ya 31% ya ajira zote hapa Tanzania na hawa ni watu milioni 2,700,000 peke yake. Kama tungekuwa tumewafanya wawe mara mbili maana yake wakawa kama milioni 6 hivi wale waanzishaji wa biashara, nazungumzia biashara hizi zote kwa maana kuanzia Micro, Small and Medium ni wale wenye kipato kisichozidi bilioni 1 basi tungeweza kuona ajira zaidi ya 70% zinatoka katika eneo hili la biashara hizi ndogo ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali tuwapatie uwezeshaji bila mizengwe, milolongo mirefu na bureaucracy. Utaratibu ambao tayari Serikali imeanza kuufanyia kazi ni mzuri sana na umekuwa na matunda ni kuwatambua Watanzania. Sasa hivi asilimia kubwa ya Watanzania wana vitambulisho vya NIDA. Kitambulisho cha NIDA unaweza ukamfahamu mtu jina lake ukiacha taarifa zile za msingi lakini unaweza kufahamu anatoka wapi, ana shughuli gani na tukiendelea kuboresha tunaweza hata kupata taarifa za kifedha na za kibenki za kila Mtanzania; benki yake ni wapi, anashughulika na jambo gani. Kwa hiyo, tutakuwa tumewaondoa watu hawa wengi kwenye Micro, Small and Medium Enterprises kwenye kigingi kikubwa cha kupata uwezeshaji wa kifedha kwa msingi wa collateral ama wanasema dhamana.

Mheshimiwa Naibu Spika, si kila Mtanzania atakuwa na hati ya nyumba rasmi ya kwenda kupata mkopo lakini siku hizi kwenye masoko ya kileo ya mikopo tumeanza kuzungumza kuhusu mbadala wa collateral kwa maana ya dhamana ile ya kidesturi kama hati ya nyumba kwa kuanza kutoa ama mikopo midogo midogo ama kutumia utambulisho ambao hauna shaka. Sasa hivi ukitumia kile kitambulisho chako cha NIDA na tukiweka vizuri zaidi watu wetu wa TEHAMA Serikalini, inawezekana kujua mwenye kitambulisho hiki cha NIDA amekopa mkopo benki kwenye eneo fulani na hajalipa au mwenye kitambulisho hiki cha NIDA ana perform mkopo wake mahali fulani vizuri zaidi. Kwa hiyo, unapokwenda kwa mkopeshaji yeyote rasmi kwa maana ya Taasisi kwa kitambulisho tu kile kinaweza kukupatia uhalali wa wewe kupata mkopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia wanaoingia kwenye soko la ajira ni zaidi ya watu milioni 1 kila mwisho wa mwaka, hawa watu wanaoingia huku ni vijana na hawa vijana hawana hati za nyumba. Kama tukiweka utaratibu mzuri wa kuwatambua wakapata vitambulisho na tukapata wanasema guarantees kutoka kwa ndugu wa karibu na ndivyo ambavyo wenzetu wa Mashariki ya Mbali, Thailand wamefanikiwa kuwakopesha watu wengi sana na kufanikiwa ni kwa sababu ya kutumia utaratibu kama huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili litatoa ajira nyingi sana. Hawa ndiyo ambao baada ya kiwanda kutoa bidhaa wao ndiyo watachakata, watasambaza kidogo kidogo; hawa ndiyo ambao mgodi ukianza ndiyo watakaokwenda kuchukua madini yatakayotolewa na kuyauza kidogo kidogo. Ushahidi upo kwenye eneo la madini hizi bilioni nyingi zimetokea ni kwa sababu tumewarasimisha wachimba madini wadogo wadogo kwa kuwawekea masoko ya madini na tumeona pesa nyingi sana imepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ilikuwa ni kuhusu uchumi. Ni muhimu sana tukafahamu kwamba uchumi wetu umekuwa madhubuti kwa sababu tumewekeza katika ujenzi kama eneo moja kubwa na ni kigezo cha ukuaji wa kiuchumi. Ujenzi huu umesambaa nchi nzima; barabara, miundombinu ya reli, tumetengeneza meli maeneo mengi kabisa na sasa tuna Bwana la Mwalimu Nyerere na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia amesema lazima mambo haya yaendelee na Watanzania wanafahamu hivyo. Ujenzi mkubwa ni kigezo kikubwa sana cha ukuaji wa kiuchumi na uchumi ukikua ndiyo tutapata fedha, watu watapata ajira nyingi za muda mfupi na muda wa kati na hatimaye mwisho wa siku watu watapata kipato na wataweza kumudu maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali, ziko fikra kadhaa lakini napenda kusisitiza kwamba ni muhimu tukaendelea kusimamia nidhamu ya kusimamia uchumi wetu. Tumefanikiwa sana kuufanya mfumuko wa bei kwua single digit na kuna fikra nyingi kwenye eneo hili lakini fikra moja ni bayana ni kwamba mfumuko wa bei unapokuwa chini mnufaika ni mwananchi wa kawaida na hasa mnyonge. Ndiye ambaye mkate utaendelea kuwa bei ileile ndani ya muda mrefu, ataongeza kipato lakini bei ya mkate itabaki palepale. Pia wale wakubwa wakiuza mikate mingi kwa sababu wananchi wote wanaweza kununua na wao hatimaye wanaweza kutengeneza faida kwa maana hiyo. Kwa hiyo, kuendelea kuweka nidhamu ya usimamiaji wa uchumi na hasa kuhakikisha kwamba inflation haiongezeki katika kiwango ambacho tume-maintain ni muhimu sana kwa ukuaji wetu wa kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni masoko. Hapa Tanzania hatuna tatizo la uzalishaji, wakulima wanalima mazao kila mwaka. Kinachotakiwa sasa hivi ni kutumia mageuzi makubwa ya ki-TEHAMA kumuunganisha mkulima moja kwa moja na soko na kuondoa ukiritimba wa madalali. Wakulima wengi hawafahamiani na mnunuaji wa mwisho lakini kama hapa tungekuja na private sector wakatengeneza mifumo ya ki-TEHAMA ambayo inaweza kumwezesha mkulima akasema nina magunia 100 ya mahindi nika-post hapa kwenye application fulani halafu mtu fulani akasema nataka magunia 50 ya mahindi akaingia kwenye application hiyo wataonana kama ambavyo mifumo hii duniani ipo. Ali Baba alianza kidogo hivi mwaka 1999 yeye na mkewe na anakubaliana na hiki tunachokisema kwamba biashara ndogo sana na za kati wanaanza watu wachache. Hapa Tanzania kwa takwimu ni 2.9% tu ya biashara hizi zote za kati na hizi ndogo zaidi ndiyo zina watu zaidi ya watu watano mahali kwingine kote ni watu wachache sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu utawala bora na uwajibikaji. Mimi napenda kusema kwamba wakati wa msiba wa Hayati Magufuli wale watu walikuwa wanalia siyo kwa sababu Rais Magufuli ametangulia mbele ya haki, mimi nasema hapana. Wale watu walikuwa wanalia kwa sababu Rais Magufuli na Mama Samia walikuwa wana jambo lao na wananchi wale. Wale wananchi walikuwa wanalia wakionyesha concern yao kama yale ambayo Rais Magufuli na Mama Samia waliwaahidi hayo ndiyo yatakayoendelea hata wakati Magufuli hayupo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mama Samia ameeleza msimamo, amesema kazi iendelee. Rai yangu kwa Serikali, usimamizi mzuri wa rasilimali za Taifa letu unatokana na nidhamu nzuri ya viongozi wetu. Vita dhidi ya rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali za umma; mambo hayo hatutakiwi kurudi nyuma kamwe, asilani! Kinyume na hapo, Watanzania wale walilia watalia na baadhi yetu humu muda si mrefu kwa sababu watasema tumewageuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu tumsaidie Mheshimiwa mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ile ndoto ambayo walituletea yeye na Mzee Magufuli, tukawaamini na tukawapenda ikatimie chini ya uongozi wake katika kipindi hiki na kwa kadri ambavyo Mungu itampendeza na yeye mwenyewe kwa maana hiyo na Chama chetu cha Mapinduzi. Umuhimu sana kuliko yote, nimefurahia sana Mheshimiwa Rais amesema kukumbuka kuzingatia haki za watu wetu na hasa wanyonge. Ni muhimu sana viongozi wakaendelea kusimamia hilo wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)