Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ili nami niweze kuchangia mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu niseme kwamba tumepata somo zuri kutoka kwa Profesa, amezidi kutufundisha kwamba kuna maeneo ambayo sisi kama Taifa ni lazima tuongeze umakini na tuyafanyie kazi kwa uharaka ili tuweze kwenda kufanana na wenzetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nikianzia pale alipoishia alipokuwa anazungumzia uwezo wa NDC kuweza kuendesha mradi mkubwa kama ule ya kule Liganga na Mchuchuma. Ni kweli wasiwasi huo si yeye tu anao lakini naamini Wabunge wengi hasa wanaotoka maeneo hayo wanajiridhisha hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo mchango wangu ulikuwa ujikite sana kwenye suala zima la sera, Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kusema kwamba ili tuendelee tunahitaji mambo manne. Tunahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora. Hapa kwenye siasa safi ndipo ambapo tunapata zile sera (policy).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Taifa letu katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali iliyopita tumefanya mabadiliko mengi sana ya sheria mbalimbali, na nyingine pia kuziboresha kupitia Miscellaneous Amendments lakini hatukugusa kwenye sera; na ili tuwe na sheria tunaanza kwenye sera.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mawaziri wote hapa wa sekta hakuna hata mmoja ambaye sera yake ni ya wakati tuliokuwa nao, sera nyingi Serikalini zimepitwa na wakati sera nyingi zimekuwa kuukuu kiasi kwamba hata mipango mizuri tunayoipanga kwa sera zilizopo bado itakuwa ni vigumu kutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano tu kwenye eneo hilo la viwanda na biashara Sera ya Maendeleo Endelevu ya viwanda (Sustainable Industry Development Policy) 1996 hadi 2000. Leo tuko mwaka wa 2021, miaka 21 hakuna sera wala hakuna mabadiliko yoyote yanayofanyika huko, ama wamelikalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (Small and Medium Enterprises Development Policy 2003), hii Wizara imeikalia tangu 2011 wameanza mchakato mpaka tunavyozungumza mchakato bado unaendelea, kwa hiyo hilo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukienda kwenye Sera ya Taifa ya Biashara (National Trade Policy – NTP 2003) nayo ni hivyo hivyo, mchakato unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa bahati mbaya sana sheria iliyoanzisha viwanda ni ya mwaka 1967 tukiwa katika ujamaa mkongwe kabisa. Sasa hivi tupo katika angalau utandawazi hata sekta za viwanda inashikiliwa zaidi na sekta binafsi siyo viwanda vile ya umma ambapo wakati huo mashirika kama TIRDO kama SIDO na halikadhalika ndiyo yalikuwa yanaweza ku-back up. Kwa hiyo utaona kabisa kwamba ndiyo maana hata eneo la viwanda na biashara kipindi hiki hatufanyi vizuri, kwasababu sera bado imepitwa na wakati lakini sheria yenyewe iliyoanzisha, Sheria ya Viwanda pia imepitwa na wakati sana, ya 1967.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa sana na eneo hili nadhani ni Ofisi ya Waziri Mkuu ndio wanaosimamia sera, ebu tuwape hawa Mawaziri wa Kisekta muda kabisa wa kuhakikisha kwamba sera hizi zinaenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimefurahi sana, juzi Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alipotoa angalau muda wa miezi mitatu kwa Waziri wa Uwekezaji kwenda kutengeneza Wizara, hilo ni jambo zuri, kwamba ni lazima tuwape muda. Tusiishie tu kwamba Waziri amepewa nanii anaondoka bila kumpa muda kwamba tunataka kipindi fulani tuwe tumeona sera ambayo imekamilika ili mambo yetu yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Ajira ni ya mwaka 2008. Hivi tunavyozungumza tunataka ajira milioni nane, ziko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini Sera ni ya mwaka 2008 inawezekana kabisa kuna mpishano kubwa kati ya Sera na mipango yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni lazima tuone kwamba mipango tunayoiweka na sera tuliyokuwa nayo ni kwa kiasi gani vinashabihiana ili kuweza kuzalisha zile ajira 2008. Sera ya Vijana ni ya mwaka 1998 Sera ya Michezo ya mwaka 1995. Sanaa ya Michezo ambayo sasa hivi tunaona kwamba eneo hili linachangia pato, nadhani ni la pili baada ya utalii, lakini sera yake ni ya mwaka 1995 ndiyo maana tunaona hata wasanii au kwenye michezo wanajiendesha wenyewe wenyewe hakuna mpango ambao Taifa kama Taifa tunaweza tukaona kama katika eneo la Michezo tunakwenda kwa mwelekeo upi. Kwa hiyo ni lazima Mheshimiwa Bashungwa fanyia kazi eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana hata Club ya Simba inapata taabu katika kuingia kwenye uwekezaji kwasababu michezo bado inaonekana ipo katika ridhaa, ilhali sasa hivi michezo ni sehemu ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Mambo ya Nje, diplomasia ya uchumi haijaandikwa popote, tunazungumza tu. Tupo katika diplomasia ya uchumi, lakini hakuna mahali popote kwamba kuna sera inaelekeza hivi, tutakuwa na waambata wa kibiashara katika balozi zetu tutakuwa na hiki, hakuna! Tunaizungumza mdomoni lakini lakini kwenye Makabrasha hakuna (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hili nalo ni eneo muhimu sana, tulitazame, hasa katika eneo hili la Kilimo ambapo tunatamani kuona kwamba mazao ya wakulima wetu yanavuka mipaka na kwenda kushindana na maeneo mengine. Sasa ni lazima sera hizi zisimamiwe na tuwape muda tuhakikishe kwamba tunakuwa na sera madhubuti zinazoweza kusimamia mpango wetu wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye elimu huku nako kuna double standard. Kuna wakati Waziri anatumia sera ya mwaka 1995, kuna wakati anatumia 2004, inategemea tu umembana katika angle gani, kwa hiyo anatafuta upenyo kwa kupitia sera. Kwa hiyo ni lazima tuwe specific, kwamba kwa elimu yetu tunatumia sera ya mwaka gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ya 2004 ndiyo ilituelekeza kwamba elimu ya Msingi iishie darasa la Sita, lakini hata Mtaala wa elimu ukaelekeza hivyo ndiyo maana miaka miwilli mitatu huko nyuma hakukuwa na vitabu vya darasa la saba. Baada ya kuanza kuhoji hili jambo nadhani wamenyofoka katika maeneo fulani fulani wametengeneza Mtaala wa Darasa la Saba; lakini kimsingi ilikuwa kwamba elimu ya msingi iishie darasa la saba katika kuboresha suala zima la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana kwamba eneo hili Serikali tunaomba kwamba tuboreshe sera zetu katika sekta zote ili ziweze kuendana na mipango hii mizuri ambayo tunaiweka ili ziweze kusaidia Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)