Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi. Naomba nianze kwa kutoa masikitiko yangu kwa Waheshimiwa Wabunge vijana ambao wako kwenye Bunge hili ambao kimsingi zaidi ya asilimia 60 ni vijana. Natoa masikitiko yangu kwa sababu kama vijana, tunao wajibu kama ambavyo kila kizazi kina wajibu wake, kama vijana tunao wajibu wa kulisaidia Taifa hili kwa sababu tuna Tanzania moja tu, sasa haiwezekani vijana tuko zaidi ya asilimia 60 kwenye Bunge hili lakini tunashindwa kutoa msaada kwa ajili ya kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe wito kwa vijana ambao wengine wameshachangia, lakini najua wanaweza kuchangia tena kwa maandishi wakashauri yaliyo bora na mema kwa ajili ya Taifa hili. Ambao bado, nawashauri, hatuna Tanzania nyingine, tuna Tanzania hii moja, tutoe michango yenye tija kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Mpango wa Mwaka Mmoja…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat, nasikia kuna taarifa mahali. Hebu ngoja tuelewane kidogo. Subiri kwanza Mheshimiwa Saashisha.

Mheshimiwa Nusrat, takwimu za kuwatuhumu vijana wote humu ndani, unamaanisha hakuna kijana aliyesimama akatoa mchango! Yaani wataanzia kutoa mchango baada ya wewe kutoa mchango? Maana umeisema kwa namna kana kwamba vijana wote waliochangia, hakuna wazo walilotoa kabisa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Afute kauli.

MWENYEKITI: Hiyo haikai sawasawa. Nanyi mnakumbuka takwimu alizozitoa Mheshimiwa Spika humu ndani. Mimi nilisikiliza michango yote, nami huhudhuria Bunge kila siku, Wabunge vijana wanafanya kazi nzuri.

MBUNGE FULANI: Alikuwa gerezani, arudishwe ndani.

MWENYEKITI: Wanaishauri Serikali, wametoa mawazo ya kuboresha maisha ya vijana. Wameeleza kuhusu mikopo, kuwekeza kwenye mitandao, kilimo na kuhusu Benki ya Vijana. Tunataka nini jamani? Mheshimiwa Nusrat, ongezea pale ambapo wenzako wamechangia. Lile ambalo wenzako hawajaliona, changia wewe, lakini usioneshe kana kwamba hakuna kijana anayetoa mchango humu ndani isipokuwa wewe. Hapana, hiyo haikai sawasawa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Anawaza kufukuzwa kwenye chama.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat endelea. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Labda ningefika mpaka mwisho ndiyo mngejua namaanisha nini.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-recognize kwa waliyozungumza, kwa sababu kimsingi hakuna tupu iliyo tupu kabisa. Kwa hiyo, kuna waliyoyazungumza.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hanje, ngoja kwanza. Hebu tutulie kidogo.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, nimesimama.

MBUNGE FULANI: Kutachafuka humu ndani! Vijana tumeongea, tumefanya kazi kubwa! Kutachafuka humu!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, nimesimama, kwa hiyo, mkae. (Kicheko)

Waheshimiwa Wabunge, tuelewane jambo moja. Nimeeleza hapa kwa kirefu nikiwa nimekaa. Nimelazimika kusimama kwa sababu Bunge hili watu wanaotakiwa kusimamia utaratibu ni wale wanaosimamia vikao. Na mimi nimeeleza vizuri; michango ya vijana waliopita, wa vyama vyote ambao wameshachangia, wamefanya kazi nzuri. (Makofi/Kicheko)

Hiyo michango waliyoitoa ni ya muhimu yote. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sana!

MWENYEKITI: Hakuna kijana aliyesimama hapa ambaye hajatoa mchango wa muhimu kwenye mapendekezo haya ya Mpango. Kwa muktadha huo, ndiyo maana nimemwambia Mheshimiwa Nusrat, naye ni kijana, aanzie pale ambapo wenzake wameishia, achangie mchango wake. Yale ambayo wanaona…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mtulie kidogo, mkitajwa majina, mnakuwa wa kwanza. Mtulie msikilize. Nikiwa nimesimama hakuna mtu anaruhusiwa kuzungumza. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kweli! (Makofi)

MWENYEKITI: Tuelewane vizuri; na tuheshimiane. Nikiwa nimesimama, Bunge linatakiwa kutulia.

MBUNGE FULANI: Sawa.

MWENYEKITI: It is only me who should be speaking because I have the right to speak. (Makofi/Kicheko)

Kwa hiyo, nikiwa nazungumza, kila mtu anapaswa kunyamaza. Ndiyo kanuni zetu zinavyosema. Tusome Kanuni, tuzielewe ili humu ndani tuheshimiane kama tunavyoitana Waheshimiwa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, hoja ya kwamba hakuna tupu, tupu kabisa, hakuna Mbunge yeyote aliyemtupu humu ndani. Kila Mbunge analo jambo ambalo wale waliomtuma wanaamini atalifanya humu ndani. Ndiyo maana kanuni zinamlinda kila Mbunge anapopata fursa ya kuchangia. Nami ni kazi yangu kumlinda kila Mbunge kwa mujibu wa kanuni zetu. (Makofi)

Bunge letu hili, alishasema Mheshimiwa Spika wakati linaanza, tukiamua kuliletea dharau, tunajidharau wenyewe. Tukiamua kuliheshimu, tunalitafutia heshima sisi wenyewe. Kwa hiyo, humu ndani tuheshimiane kama ambavyo sisi tumeamua kuheshimiana na wale waliotutuma wanatuita Waheshimiwa. Kila Mbunge anao mchango wake, hakuna Mbunge aliye tupu humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nizungumze, kwa sababu mipango ilikuwa imepangwa kwa miaka 15 kwa miaka mitano mitano, for the last ten years, ripoti za CAG zinaonyesha kuna failure kubwa sana katika utekelezaji wa mipango. Bajeti zinapangwa, mambo hayaendi kwa sababu…

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, haijawahi kutokea Mbunge akaweka mapendekezo au akazungumza…

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat kuna taarifa. Mheshimiwa Jaqueline Msongozi.

MHE. JAQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nataka tu nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza, kwanza afute kauli yake aliyoongea kwanza, halafu ndiyo aendelee na mchango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Kicheko/Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walzungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, nimeshatoa maelezo ya namna ya kwenda kuanzia hapa tulipo. Mheshimiwa Nusrat.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nilikuwa nazungumza kwamba, tunafeli kwa sababu hatuna sheria. Ibara ya 63(3)(c) inaruhusu Bunge kutunga sheria ya kusimamia mipango kwa ajili ya kusaidia uwajibikaji na kusaidia mipango kufanya kazi. Mpaka sasa for the last ten years hatujawahi kuletewa Muswada. By then mimi nimekuja lakini hakuna Muswada uliowahi kuletwa hapa Bungeni (If I am not right, kuna wakongwe watasema) kwa ajili ya kusaidia ufanikishaji na usimamiaji wa mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kila siku tunapanga, tunarudi hapa kwenye kilimo. Tunaona kabisa tumetoka hatua moja, tumeenda hatua mbili mbele, tumerudi nane nyuma. Tunarudi tunasema tunapanga tena. Bajeti haiendi mathalan…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: … bajeti ya maendeleo imetekelezwa kwa asilimia 17.55.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat kuna taarifa. Mheshimiwa Ndaisaba.

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kumpatia taarifa Mheshimiwa Nusrat. Katika maelezo yake amesema kwamba tunafeli kwa sababu hatuna sheria ya kusimamia mipango. Naomba nimfahamishe kwamba kila jambo linalotungwa; bajeti ya Serikali, lina sheria mama na lina-fall kwenye specific category ambayo ina sheria zake. Ukienda kwenye kilimo kuna sheria, kwenye maji kuna sheria, kwenye barabara kuna sheria. Sheria zile ndizo zinazoratibu utekelezaji wa mipango ya Serikali

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo sheria nyingine anayotaka iibuke sheria juu ya sheria ni ya namna gani? Naomba apokee taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa kwa sababu nimezungumza kitu kingine na amezungumza kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wabunge sasa hicho nilichokizungumza kama vijana tungeweza kusimama pamoja tukashauri Serikali ilete Muswada kwa ajili ya kuhakikisha mipango tunayoipanga, itekelezwe ili tuepuke budget reallocation, tuepuke kutokupeleka bajeti kama zinavyopangwa kwenye Bunge la Bajeti, wanapanga bajeti hazipelekwi, Mpango wa Maendeleo…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: … bajeti ya maendeleo kwenye kilimo imepelekwa asilimia 17.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. NUSRAT S. HANJE: …asilimia 82 haijapelekwa…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, kwa Mheshimiwa Nusrat hii itakuwa taarifa ya mwisho. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Hussein Amar.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji anayeongea ni kana kwamba sisi wazee ama wenye umri mkubwa, hatustahiki kuchangia Mpango wa Maendeleo. Tumeletwa na wananchi na wametuamini pamoja na umri wetu kuja kuchangia maendeleo na kufikisha mipango yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa, vijana wanataka kuleta ubaguzi wakati tumeongoza kwenye kura kwa asilimia nyingi pamoja na umri wetu mkubwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tumsikilize. Mheshimiwa Nusrat, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mzee wangu shikamoo! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaheshimu wazee wote, lakini tunafahamu hata Wamasai wapo humu ndani, morani; huwezi kufananisha age. Yaani hiyo age conflict. Ila nawaheshimu sana wazee wangu. Mpo! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza kwamba bajeti ya maendeleo kwenye kilimo haijaenda kwa asilimia 82. Tuna shida ya mbegu kwenye Taifa, tuna tatizo la mbegu kwenye Taifa, lakini Serikali imetenga mashamba tisa ya kuzalisha mbegu. Ni shamba moja tu ambalo linazalisha mbegu, linafanya kazi mwaka mzima. Mashamba mengine yote nane yanategemea kilimo kwa kudra za Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwenye jambo moja. Mheshimiwa Spika juzi alivyokuwa kwenye kiti alitoa mfano akasema anatamani tupate kitu cha ziada kuwasaidia vijana wetu, anachukia kuwaona wako kwenye pool table. Naomba ku-declare interest, mimi ni Mwalimu. Kama nchi, tuna tatizo kwenye elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu, watoto wetu wanakosa vitu vitatu vya msingi na Waziri wa Elimu yupo asikilize. Elimu yetu haina career guidance, haina personal development. Leo tunazungumza soft skills, wasomi wengi wanaotoka vyuo vikuu, inawezekana nikiwemo mimi na wengi wetu humu na wengine wako nje, tunakosa vitu vya msingi. Tunafundishwa kwenye Civics Communication Skills, tunafundishwa self-esteem, self-confidence na nini, lakini tunashindwa ku-connect na maisha halisi. Ndiyo maana kuna motivation speakers. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu Mheshimiwa Eric Shigongo yule pale anaelewa, ndiyo maana leo kuna motivation speakers wengi kwa sababu tunashindwa, yaani hatuwezi ku-connect maisha ya shule na nini kipo mtaani, ndiyo maana watu hawawezi kujiongeza. Falsafa ya Kuanzia sokoni, watu walitakiwa wajifunze shule, siyo wanamaliza shule, ndiyo wanatoka wanakuja kuambiwa kwenye biashara tuanzie sokoni. No!

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna kitu kingine cha msingi tunakosa. Leo Waheshimiwa Wabunge wanakalishwa chini wanafundishwa investment, shule wanasoma pesa, lakini hawasomi financial management; elimu yetu inakosa financial management; tunasoma Book Keeping na Commerce (makabati), haina reality kwenye ukweli. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza nikatoa mchango wangu pia kwenye maandishi kuhusiana na elimu; nishauri kwa sababu kila mtu ana akili (everybody is genius), lakini if you judge a fish by its ability to climb a tree, anaishi maisha yake yote hajui kama yeye ana akili. Kwa hiyo, naweza nikashauri hiyo kwa sababu natamani kuona tunafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naishia hapo. (Makofi)