Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pasipo kifani kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umewakilishwa na Waziri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa mama Kilango Malecela leo alikuwa anachangia nikamwomba aniazime dakika zake tano na akakubali. Sasa kama wewe itakupendeza basi niunganishe dakika tano za Mheshimiwa mama Malecela na za kwangu nipate dakika kumi ili niweze kutoa nilichonacho. Nimezungumza naye akasema anachangia na akaniruhusu lakini nikasema nikipata ruhusa yako na hekima yako itapendeza sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima, hiyo hairusiwi, Wabunge huwa hawapeani muda lakini muda wako sasa unazidi kwenda kwa hayo maombi ambayo yamechukua muda kidogo, tafadhali anza kuchangia. (Makofi/Kicheko)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno machache sana kwa sababu ya muda wangu, kuna hoja zinazungumzwa hapa kuonyesha kana kwamba awamu ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haijafanya jambo lolote. Mtu yeyote ambaye haoni kwamba miaka mitano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haijafanya chochote basi anaweza kuwa na ugonjwa hatari sana ambao hauwezi kutibika hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua fika kwamba kuanzia mwaka 1976 mpaka 1981, Tanzania ilikuwa na ndege almost 11 na mpaka tunafika kwenye ubinafsishaji tulikuwa na ndege 9 na mpaka Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anaingia madarakani tukawa hatuna ndege. Hata hivyo, tangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameingia madarakani tuna ndege zinaelekea 12 sasa. Asiyeona hayo ana ugonjwa special unahitaji daktari special. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unakumbuka vizuri Shirika la TANESCO, kabla ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajaingia madarakani lilikuwa linaendeshwa kwa kupewa ruzuku shilingi bilioni 438 kila mwaka, lakini tangu 2015 Shirika la TANESCO linajiendesha kwa fedha yake lenyewe na linafanya vizuri sana. Asiyeona ana ugonjwa maalum unahitaji daktari maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, mwaka 2015 Tanzania yote ilikuwa na vijiji 2,018 vilivyokuwa na umeme lakini leo ndani ya miaka mitano vijiji 10,263 vina umeme katika nchi ya Tanzania. Kwa taarifa ya asiyeona ni kwamba vimebaki vijiji 2,005 tu Tanzania yote iwe na umeme. Pamoja na mambo mengine yote lakini mwenye macho ni muhimu aone kitu gani kimefanyika na wapi tunaelekea kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanasema msiongelee sana Stigler’s Gorge ni ileile, sikiliza nikwambie tangu Tanzania ianze ina megawatt za umeme 1,602, hii ni tangu Mwalimu Nyerere, Mheshimiwa Mwinyi, Mheshimiwa Mkapa na Mheshimiwa JK Kikwete, utaachaje kuongelea Stigler’s Gorge ambao ni mradi mmoja wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambao umetupa megawatt 2,115. Lazima akili iwe likizo au ina matatizo maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hebu tuseme ukweli, mimi nimekuwa Japan, wao wana treni inakwenda kwa speed 250 na wana nyingine ambayo watazindua mwaka ujao inayotembea chini ya ardhi inayokwenda kilomita 500 kwa saa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania kwa Afrika Mashariki tumekuwa nchi ya kwanza kutekeleza mradi wa treni yenye uwezo wa kwenda kilomita 160 kwa saa. Utasemaje Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajafanya vitu vyake? Unahitaji dawa maalum na daktari maalum kusema hivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haitoshi, hebu tuangalie ukweli, wakati Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli anaingia madarakani tunaambiwa tembo wa Tanzania walikuwa wamebaki 15,000, leo kwa taarifa ya Wizara ya Maliasili tuna tembo 60,000. Kwa utawala wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli mpaka tembo wanaanza kuzaana bila utaratibu. Huwezi kusema Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hajafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano afya, nagusia kila mahali kwa sababu muda wangu haunitoshi, tangu Uhuru tumekuwa na Hospitali za Wilaya 77 lakini miaka mitano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli tumejenga Hospitali zingine za Wilaya 102. Utabezaje hizo juhudi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haraka haraka tulikuwa na Hospitali za Rufaa za Mikoa 18 tu tangu Uhuru ndani ya miaka tano zimejengwa mpya 10. Asiyeona ana ugonjwa unaitwa Schizophrenia.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Gwajima, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namsubiri. (Kicheko)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda tu nimpe taarifa anayenisubiri, kwanza hapa tunachangia Mpango kushauri Serikali, tunavyosema Mpango haujatekelezeka hatumaanishi kwamba Mheshimiwa Dkt. Magufuli wa Awamu ya Tano hajafanya kitu. Mfano kwenye umeme alipotaja target tuliyojiwekea mpaka 2021 ilikuwa tufikie megawatt 4,915 lakini mpaka sasa hivi tuna megawatt 1,601 wakati mwaka 2014/2015 ilikuwa ni megawatt 1,501. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema kwamba wanaweka target na hazifikiwi siyo kwamba tunasema hakijafanyika kitu lakini wanavyoweka viashiria basi viweze kufikiwa angalua kwa asilimia 80. Asipambe bali ashauri ili Serikali ifanyie kazi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Esther Matiko. Mheshimiwa kabla sijakuuliza kama unapokea taarifa, nadhani tuwe tunaelewana vizuri, mtu anayegoma kutambua kilichofanyika na mtu anayetambua kilichofanyika lakini anatoa ushauri wa nini kifanyike zaidi kuna tofauti kati ya hayo mambo mawili. Mheshimiwa Gwajima unapokea taarifa hiyo? (Makofi)

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimwambie msomi yeyote kabla hajaenda mbele ana-refer kwanza kule alipotoka. Mimi nime- refer kwanza alipotoka Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Mpango uliowekwa na Waziri wa Magufuli Mheshimiwa Dkt. Mpango wa kule tunapoelekea. Kwa hiyo, taarifa yake haina maana yoyote kwangu, naomba niendele Mheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vituo vya afya tangu Uhuru tulikuwa na vituo vya afya 535 lakini ndani ya miaka mitano tumejenga vituo vya afya 487. Kama hiyo haitoshi tangu uhuru tulikuwa na zahanati 4,554 lakini ndani ya miaka mitano tumejenga zahanati mpya 1,998.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme jambo moja kwamba haya yote niliyoyasema hayamaanishi kwamba tusitekeleze Mpango mpya uliowekwa mbele yetu. Nataka kila mtu afahamu kuna ugonjwa wa COVID-19 ambao ni ugonjwa umetikisa dunia na nchi yetu imechukuwa msimamo tofauti na nchi nyingine zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge nataka kutumia nafasi hii kuwatia moyo; msiogope. Msiogope mnapoambiwa kwamba kuna phase ya pili ya COVID-19. Kilicho na nguvu nyuma ya COVID-19 ni woga uliotengenezwa juu ya COVID-19; the fear over COVID-19 is even more powerful than COVID-19 itself.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote na watu wote tushinde woga, tusiogope, tumeshinda, tusonge mbele. Msimamo wetu wa kutokuchanjwa na msimamo wetu wa kutokufanya social distancing ni msimamo sahihi na utatufikisha mahali sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha mwisho, watu wengi wanazungumza kusahau tulikotoka wakifikiri historia when you don’t remember where you are coming from, you are bound to make mistakes where you are going thinking you are doing development, but you may do the same because you don’t know where you are coming from.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu kule nyuma ilikuwa na miradi ya wachimba madini. Tulikuwa tunapewa royalties peke yake, nchi yetu ilikuwa inapata royalties peke yake ya makampuni ya madini. Sasa hivi Mheshimiwa Rais amesukuma tunapata almost asilimia 50 na Tanzania ni wamiliki wenza wa madini yanayochimbwa na kampuni za madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)