Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipatia hii nafasi ili nami niweze kuchangia katika mjadala huu unaondelea. Kwanza nianze kwa kukipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa uliopatikana katika uchaguzi mkuu, lakini pia naomba nimpongeze sana Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana katika awamu hii ukilinganisha na mahali tulikotoka, lakini pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Vwawa kwa kunichagua na kunifanya kwamba niwe Mbunge kwa awamu ya pili, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachangia hotuba ya Rais na ninaona hapa kuna hotuba ziko mbili, ya mwaka 2015 na ya mwaka 2020. Na mimi naamini lengo la hotuba zote mbili ni kutupa mwelekeo kwamba tulikotoka tumetoka wapi, tumefika wapi, tunataka twende wapi.

Mheshimiwa Spika, Baba wa Taifa aliwahi kutuambia kwamba ili nchi yoyote iweze kuendelea inahitaji vitu vine, tunahitaji ardhi, watu, siasa safi na tunahitaji uongozi bora katika hivi vitu vyote tumepata mafanikio makubwa. Cha kwanza ardhi tunayo ya kutosha, watu tunao, lakini siasa safi tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao uongozi tumekuwa na tatizo dogo kwenye uongozi na tunaona kabisa nchi yoyote inayotaka kuendelea duniani uongozi imara ni msingi mkubwa sana katika kulifanya Taifa lolote lifikie malengo yake. Na kwa hatua hiyo, ukichukua hotuba ya Rais yam waka 2015 aliyoitoa mambo aliyoyafanya na tukiona matokeo yake sasahivi, labda kwa sababu ya muda nitasema tu machache.

Mheshimiwa Spika, la kwanza kwa kuonesha umahiri wa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, la kwanza jambo lililoshindikana kwa miaka yote ya Serikali zote zilizotangulia pamoja na kwamba, kila Serikali ilifanya mambo makubwa, lakini jambo lililoshindikana la kuhamishia Serikali Dodoma limewezekana. Hiyo inapima ubora wa kiongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili alilolifanya Rais Magufuli ni kuikokota nchi kutoka kwenye nchi maskini na kuifikisha kuwa nchi ya kipato cha kati. Hili sio jambo la kubeza, ni jambo kubwa ambalo limefanyika, ni jambo kubwa ambalo viongozi wote wanastahili kupongezwa likiwemo Bunge la Kumi na Moja kwa kazi kubwa ya kuisaidia nchi kutoka tulikotoka mpaka tumeiingiza kuwa nchi ya kipato cha kati. Sasa tumekuwa ni nchi ya kipato cha kati kwenye ile lower boundary. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukiisoma ile hotuba ina mambo mengi, kwa sababu ya muda siwezi kusema, lakini jambo la tatu ni miradi mikubwa aliyoweza kuitekeleza ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza ambayo imebaki kama alama. Ukichukua mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ambao unaendelea sasa hivi, mkoloni alijenga reli ya kati, tulipopata uhuru tumejenga reli ya TAZARA, sasa tunajenga SGR kwa hela yetu. Hili ni jambo la kujipongeza na ni maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi wa kujenga bwawa la umeme, tunajenga kwa fedha zetu. Tumenunua ndege, tunajenga viwanda, barabara, kila aiina ya mafanikio. Haya yote ndio yanapima utekelezaji wa hotuba aliyoitoa Rais mwaka 2015. Mwaka 2020 Rais anatuambia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda ni quote ukurasa ule wa 26. Anasema, “mbali na hatua hizo kwa lengo la kukuza uchumi, kupambana na umaskini na pia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira tunakusudia kwenye miaka mitano ijayo kuweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta kuu za uchumi na uzalishaji, hususan, kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini, biashara na utalii.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake nini? Hotuba ya Rais aliyoitoa ya awamu ya pili inatupa muelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kipindi cha pili. Na hii kama kweli tukiweka nguvu tukawekeza kwenye sekta za uzalishaji za kukuza uchumi ni wazi kabisa miaka mitano itakapokwisha tutakuwa tumefikia sasa kwenda kuwa nchi ya kipato cha kati cha uwanda wa juu. Na hili linawezekana kama Bunge litaweka targets na malengo thabiti ya kuisimamia Serikali na kuishauri Serikali. Na ninaamini haya yanawezekana kwa uongozi wako na kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mungu awabariki. Ahsanteni, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)