Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na mimi nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyenijaalia uzima kufikia siku ya leo, lakini niwashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Nkasi Kaskazini kwa kuniamini na leo niko ndani ya Bunge kuwasilisha mawazo waliyonipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulingana na dakika tano nitazungumza kwa uchache sana. Siku alipokuja Mheshimiwa Rais ndani ya Bunge nilikuwepo hapa na leo tunazungumzia hotuba yake ambayo ni mwelekeo kwa Taifa letu. Ukitazama nchi yetu ya Tanzania kila kanda ina vitu ambavyo vipo vinaweza vikasaidia Taifa. Kanda yetu ya Nyanda za Juu Kusini na kwenye hotuba Mheshimiwa Rais amezungumzia zaidi kujikita kwenye kilimo. Nyanda za Juu Kusini tunajishughulisha na kilimo. Lakini pamoja na kilimo hicho ni namna gani kinanufaisha Taifa kwa ujumla. Ukizungumzia Nyanda za juu Kusini unazungumzia mikoa mitano ambayo inazalisha chakula na mazao ya biashara lakini sisi tumebahatika pia kupya bandari ya Kabwe, bandari ile ingetumika vizuri kulingana na mazao yanayozalishwa kwenye Nyanda za Juu Kusini sio tu kusaidia Nyanda za Juu Kusini, ingesaidia pia Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, kupitia bandari ile ambayo tayari Taifa limewekeza fedha nyingi tunategemea kupata matokeo ambayo yatakuwa ni matokeo chanya yatawasaidia wananchi wanaozunguka eneo lile la bandari lakini pia yatasaidia Taifa. Ili tuweze kusafirisha mazao ambayo tunaamini tunaweza tukapeleka nchi za jirani ambao wanaweza kutumia bandari yetu ya Kabwe ni lazima kiwe ni kilimo chenye tija. Wakati nazungumzia kilimo kwenye Nyanda za Juu Kusini tayari Serikali imeweka fedha nyingi kwenye miradi ya umwagiliaji, lakini ni miradi mingapi inafanya kazi mpaka leo? Unaitazama dhana ya Serikali kuwekeza fedha lakini namna gani tunakwenda kumalizia hizo fedha au viporo ambavyo tayari tumekwisha vianzisha?

Mheshimiwa Spika, wakati nazungumzia kilimo si kuwasaidia tu wakulima, lakini ukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Rais naye amekiri kwamba ajira zinazopatikana kwa mwaka haziendani na uhitimu wa wanafunzi kulingana na level mbalimbali. Tunaamini kilimo ndiyo ingekuwa muarobaini wa kuweza kumaliza jambo hilo. Kilimo tunachozungumzia hatuzungumzii kilimo cha mazoea. Kama tumeanzisha miradi ya umwagiliaji wanakwenda kuazalisha nini? Je, wanachozalisha watauza wapi? Mheshimiwa Rais baada ya kuzungumza ndani ya Bunge ni kazi ya Mawaziri sasa. Kwa mfano, natambua kwamba janga la Corona limepita dunia nzima hatufurahishwi nalo, lakini sisi tumebahatika wananchi wetu wameendelea kulima wamezalisha kwa wingi. Mpaka sasa tunatumiaje fursa hiyo kuweza kuwasaidia wananchi wetu ambao ni wakulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, wakati tunazungumza hapa pia tayari Serikali imewekeza fedha kwenye vyuo mbalimbali na hapa mimi nategemea TAMISEMI na Wizara ya Elimu hii asilimia nne ya kwenda kuwasaidia vijana hawa ambao wamemaliza level mbalimbali hawana ajira haisaidii sana, haileti yale matokeo ambayo tulikusudia. Leo hivi vyuo vya VETA wanakuwa wameshapata ujuzi. Kwa nini pale wanapokaribia kuhitimu wasipewe fedha kwa ajili ya mikopo na fedha hiyo ni rahisi kurudisha tofauti na sasa ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo wanamaliza wanakwenda kukaa tu mtaani. Kwa hiyo inakuwa haina utofauti na wale ambao wametoka shuleni hawajafundishwa namna ya kujiajiri. Lakini hawa tayari wameshapewa ni namna gani wanaweza kujiajiri. Kwa hiyo tunaweza tukatumia ile fedha badala ya kuwapa kiasi kidogo tukaangalia wahitimu ni kiasi gani watapewa fedha hizo waweze kusaidia na wale mataajiri watu wengine kupitia mafunzo ambayo wameyapata na itakuwa na maana Zaidi juu ya kwenda kuwa empower vijana pamoja na wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tukirudi kwenye kilimo hapo hapo hivi Vyuo vya Utafiti vikiwezeshwa kikamilifu watu watakuwa na uhakika wa kulimo wanachokilima. Watakuwa na uhakika wa mbegu zinazotoka kwa sababu tayari zimefanyiwa utafiti. Lakini leo hata ukiangalia maeneo ambayo watu wanalima, mtu anaamua kwamba yule alipata gunia 10 na mimi leo nitalima gunia 10. Hapana, tuambieni aina ya udongo huu mnaweza kulima zao fulani. Mkituambia pia tutajua soko la zao hilo liko wapi. Kwa hiyo, hata mtu anapoingia kwenye kilimo hawezi tena kufikiri ajira. Leo tutakwenda kuwafundisha vijana namna bora ni namna gani wanaweza kujiajiri. Ahsante. (Makofi)