Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha lakini kabla sijaenda huko nipende kusema kwamba sisi kama wapinzani mnavyotuita, sisi kazi yetu ni kueleza yale maeneo ambayo hayajakaa sawasawa lakini yale yaliyokaa sawasawa sisi hatuna haja ya kumpaka mafuta Mheshimiwa Waziri au Rais, tunaangalia yale mabovu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mpokee maoni ya Kambi ya Upinzani kwa sababu tunaeleza hayo. Sasa Mheshimiwa Dkt. Mpango wewe unapakwa lubricant halafu then wanaweza kukuangalia saa nyingine mambo yakaharibika. Kwa hiyo, yale mabaya tunapokueleza usikatae naomba uyapokee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine pia vijana wameeleza leo mambo mazuri sana, nimefurahi sana au nimefurahishwa sana na Mheshimiwa Mlinga alipokuwa anasema kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa anatumia Ilani ya CHADEMA, natoa pongezi nyingi sana kwa sababu ile ilani iliandikwa vizuri sana na ilifanyiwa kazi na watalaam vizuri sana, haikuwa hovyohovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la picha ambazo anazisema mwenzangu Mheshimiwa Marwa Ryoba, picha zipo hata mahali popote hata kwenye vitabu vyetu hivi vya Mheshimiwa Dkt. Mpango vina picha, picha siyo tatizo la mtu. Yule hakwenda kuandika Ilani bali Lowassa alihamia CHADEMA kama yeye alivyohamia CCM. Kwa hiyo, siyo suala la kwamba alienda kufanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwaeleze kwamba hakuna kitu kibaya kama kujifunua uwezo wako wa kutumia akili. Kwa hiyo, hawa vijana wasipende kujifunuafunua, huyu anayekuja huku anakwenda kule muogopeni sana mtu wa namna hiyo, lakini kubwa zaidi, hata usemi wa Mheshimiwa Rais siku moja aliwakaribisha akasema ng’ombe aliyekatwa mkia hata kwenye zizi ng’ombe wenzake wanamuona. Kwa hiyo, kwa kuwa wamekatwa mikia, mnawaona kwa hiyo, muendelee kuwatumia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge naona mnapiga makofi, wakati huohuo mlipozungumwa nyie kuhusu mkia mlitaka kunyanyuka hapa. Mheshimiwa Rose Kamili hayo maneno nadhani ulikuwa umekaa hapo wakati nikiyatolea maelezo. Kwa hiyo, hakuna mtu anatakiwa kuzungumzwa kana kwamba yeye ana mkia au yeye ni mkia. Kama nilivyokataa kuhusu ninyi, hivyohivyo na ninyi huku nawakataza kuita wenzenu wamekatwa mikia au wamekatwa chochote ama wao ni mikia.

Kwa hiyo, na ninyi ndio mnapenda sana kutumia neno linaitwa double standard. Kwa hiyo, ndiyo muelewe maana ya double standard ndiyo hii. Namna ambavyo yeye nimemkataza na nyie msitumie, nashangaa wanaoshangilia wakati wao walitaka kunyanyuka wakati Mheshimiwa Ryoba Chacha alikuwa anachangia.

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimenukuu usemi wa Mheshimiwa Rais Magufuli… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Rose Kamili yeye hakunukuu kitabu, si alinukuu Biblia ama hukumsikia? Alinukuu kitabu cha Biblia na nimemkatalia, wewe unasema umenukuu maneno ya Mheshimiwa Rais, aah! Si sawasaw na ndiyo maana nimesema nawashangaa wa upande wako wanaokupigia makofi kwa sababu wao walitaka kuonesha kujisikia vibaya wakati Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha akichangia, kwa hivyo nashangaa sana. Tafadhali, hayo maneno yasitumike kama ambavyo nimeyakataa upande wa Chama cha Mapinduzi, na ninyi msiyatumie CHADEMA ama chama chochote humu ndani.

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba unilindie muda wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye hotuba aliyotupatia Mheshimiwa Dkt. Mpango, nataka kunukuu maneno ya Mheshimiwa Dkt. Mpango ya ukurasa wa 95 aliyesema kwamba anawasihi wananchi wachague wenye sifa mpaka tisa. Sasa nachukua kimoja tu kile cha kwamba awe mwepesi kuona, kusikiliza na kuguswa na shida za wananchi wake tena awe jasiri kupigania haki za wanyonge na awe na uwezo wa ubunifu katika kutatua kero za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa usemi wake huu mzuri Mheshimiwa Dkt. Mpango, nakwenda moja kwa moja kwenye Wizara ya Kilimo na Mifugo. Wizara ya Mifugo kwa kweli imenisikitisha sana, kama kweli usemi wake wa kiongozi awe hivyo, imekuwaje Wizara hii ya Mifugo ipewe fedha za maendeleo sifuri wakati Bunge hili liliidhinisha bilioni nne, tena hela ndogo sana, bilioni nne, lakini hawakupata hata senti tano. Kwa hiyo masikitiko yangu ni kwamba, sasa kauli yake ambayo amesema kiongozi anatakiwa awe anasikiliza wanyonge na kutatua kero imekuwaje hata ile bajeti isitekelezwe. Pia hiyo bajeti hata sasa hivi inaonekana kwamba ni ndogo sana kwa kupelekwa Wizara hiyo ya Mifugo. Naomba hebu aiangalie sana; hii Wizara inadhalilika au haifai au ni kitu gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha anapeleka mshahara tu lakini mambo ya maendeleo hayajulikani na hii Wizara ndiyo anayoitegemea kwenye viwanda ambapo anasema ndiyo kipaumbele chake sasa hivi kwenye kitabu chake, kwenye ukurasa wa 31, kwamba watahakikisha viwanda vinaendelezwa na kilimo ambapo kilimo hicho kuna kilimo, mifugo na uvuvi. Sasa ataendelezaje kama hapeleki hata shilingi moja, kwa kweli hilo waliangalie sana, wametudhalilisha. Ndiyo maana nasema kumpaka mafuta siyo sahihi kwa sababu kuna jambo ambalo ni kubwa sana linatakiwa lifanyiwe kazi. Hii Wizara itaendeshwaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwangalie Mheshimiwa Mpina, amechoka. Anakimbiakimbia na visu na rula na nini, ni taabu kwa sababu hakuna hela za miradi. Amuonee huruma, tunaomba hii Wizara aiangalie kwa jicho la huruma, kwa kweli hii ni hali mbaya sana. Sisi kama Upinzani tunaona kwa kweli hajafanya fair na hawa ndio watu wengi walioko huko ambao anawategemea wapige kura, atawapataje na kura ataipataje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni Wizara ya Kilimo; Wizara hii 2018 tuliidhinisha bilioni 150.2, lakini hadi Machi imetolewa bilioni 16.5; hivi kweli ndiyo anasema atafungua viwanda, vya nini, viko wapi? Atamhamasisha nani wakati Waziri hakupeleka fedha inavyotakiwa? Wakati anapeleka fedha nyingine nyingi Wizara ya Mambo ya Ndani, zote mpaka sijui asilimia mia moja na kitu, lakini Wizara ambayo ina watu wengi haipelekewi kitu chochote. Nadhani hapo tufikirie sana kitu cha kufanya ili usemi wake aliousema kiongozi anayechaguliwa ni wa namna gani, basi aliangalie hilo. Nadhani kiongozi bora anafaa achaguliwe kutoka CHADEMA kwa sababu ndio wanaomuuliza maswali na hawampaki mafuta, nafiki hiyo ilani nyingine tuiache sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la wazee; habari ya wazee haionekani kabisa kuzungumzwa. Ni kweli analeta habari ya kufuta tozo ya pedi lakini habari ya wazee kama akina Rose Kamili hajaiona, hebu aliangalie hilo, tunafanyaje kuhusu wazee? Mheshimiwa mama Jenista alikuwa Mwenyekiti wetu wa Kamati, tulikuwa tumelilia sana wazee waweze kulipwa 20,000 kwa mwezi ili waweze kukimu maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wanahangaika wanaombaomba, wanapita barabarani wanawaona. Sasa je, tunawasaidiaje? Nyumba za wazee ziko ngapi, kila mkoa una nyumba ya wazee, hakuna; anafanyaje kuhusu wazee? Naomba sana hata Wabunge hilo walione, hata wao watazeeka hakuna ambaye atabaki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)