Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza, nimsaidie kaka yangu Marwa Ryoba, kaka yangu wa zamani kwamba ukitembea na Ilani ya Uchaguzi ya CHADEMA ujitahidi upate na vitabu vingine vitatu vitakusaidia sana. Najua una kazi kubwa sana uko ulipo, tafuta Sera ya CHADEMA ambatanisha na Mpango wa Utekelezaji wa Bajeti na bajeti kivuli ya CHADEMA. Hapo utakuwa umefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania ….

TAARIFA

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome, kuna taarifa, Mheshimiwa Ryoba.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa, kwa wale tuliogombea kupitia CHADEMA…

MBUNGE FULANI: Yeye hajagombea.

MHE. MARWA R. CHACHA: Document tuliyopewa ni Ilani, CHADEMA haikuwa na Sera, juzi tu ndiyo wametengeneza Sera, hawajawahi kuwa na Sera, wana hii Ilani.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MBUNGE FULANI: Yeye hajagombea.

MHE. MARWA R. CHACHA: Huyo ni Viti Maalum hajawahi kugombea Ubunge.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome Wycliffe Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 8(b) inasema: “Serikali ili kuhakikisha kwamba inatekeleza majukumu yake ni lazima ihakikishe inaweka ustawi wa watu”. Nasema hivi, Mbunge yeyote aliyemo humu ndani ambaye ataunga mkono bajeti hii ya Mheshimiwa Dkt. Mpango halafu akajiita mzalendo nitamshangaa. Nasema hivyo kwa sababu zifuatazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii ya Mheshimiwa Dkt. Mpango imekwenda kupeleka asilimia 39% ya bajeti yote kujenga Stigler’s na SGR, maendeleo ya vitu. Bajeti hii inakwenda kinyume na dunia inayokwenda, dunia kwenye Sustainable Development Goals Stigler’s kwa maana ya miundombinu na nishati ni kipaumbele Na.7 na Na.9. Kipaumbele Na.1 ni kufuta umasikini; Na.2 ni kuhakikisha hakuna njaa kwenye nchi; Na.3 ni afya; Na.4 ni elimu bora; Na.5 ni usawa wa kijinsia; Na.6 ni maji safi na salama, sasa ndiyo unakuja Na.7 nishati nafuu kwa maana ya Stigler’s Gorge then unakuja Na.8 kazi yenye staha na Na.9 ni miundombinu ambayo ndiyo SGR. (Makofi)

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba, kuna taarifa, Mheshimiwa Kuchauka.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumpa taarifa mzungumzaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati jana nachangia nilisema kwamba asilimia 65% ya watu wetu wanategemea sana kilimo na nikaainisha moja ya matatizo ya kilimo ni miundombinu ambayo ingewezesha wakulima wetu kufikisha mazao yao kwenye masoko. Nikazungumzia suala la reli na barabara. Sasa anaposema kwamba Serikali hii inaingiza fedha nyingi kwenye miundombinu inaacha maendeleo ya watu hapo namshangaa. Maendeleo ya watu yanakuja baada ya kuimarisha miundombinu ili wakulima waweze kutoa mazao yao mashambani na kuyafikisha kwenye masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa hiyo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, unilindie muda wangu, tafadhali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lugha nyingine msemaji aliyetoka kunipa taarifa anamaanisha kwamba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ya wanyonge imepeleka ile shilingi trilioni 33.1 ambayo leo tunatamba ndiyo bajeti ya Serikali, hayo anayoyasema yeye ni shilingi trilioni nane tu, pesa nyingine yote wamekwenda kuboresha miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba kununua dawa tunapambana kwenye trilioni nane, Wabunge 395 tuliopo humu ndani dawa ni trilioni nane hiyo tunagombania, kupunguza udumavu wa wananchi trilioni nane, kwenda kumtua mama ndoo kichwani kelele zote trilioni 8 na kuinua kilimo trilioni nane; kwa mwaka huu wote wa fedha na mambo mengine yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pesa nyingine yote ambayo iliyopo inakwenda kulipa deni la Taifa trilioni tisa, kwenye mishahara trilioni saba trilioni tatu matumizi mengineyo na kwenye pesa ya maendeleo hiyo trilioni nane usisahau ndiyo tunapoenda kutoa hela ya Stiegler’s na SGR yaani reli ya kati na huo mtambo wa kufua umeme wa Mto Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Serikali inaturudisha nyuma ambako hatukuwahi kufikiria. Hivi jiulize swali, mwaka jana wamesema projection zao ilikuwa ni kukusanya trilioni 1.4, wakakusanya trilioni 1.2. Na hiyo pesa wameikusanya alisema hapa Mheshimiwa Lwakatare, walitumia mizinga ya aina zote; matrafiki wakapanda juu ya mti, DPP akapeleka kesi, huku wajasiliamali vitambulisho 20,000, kila aina ya mbinu wakaishia 1.2 trilioni. Sasa angalia sasa hivi wana- projection ya kukusanya 1.6 trilioni, tutapona kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vipaumbele vyao sasa vya kufikisha 1.6, wanaenda kuweka kodi kwenye peremende, wanahangaika na mawigi, wanakwenda chocolate waweke kodi, leo wametoa VAT kwenye taulo za kike. Hiyo ndiyo aina ya wataalam tulionao kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, atakayeunga mkono bajeti hii nitamshangaa. Kwanza imewekeza kwenye vitu lakini pili pesa yote ya kuendesha miradi inatokana na wananchi wenyewe…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: wanasema asilimia 15 ya bajeti watatoa kutoka kwenye…

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa ya mwisho hiyo kwa Mheshimiwa Salome Makamba

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nataka nimueleweshe ndugu yangu Mheshimiwa Salome Makamba kwa sababu yeye ni mwanasheria, mimi ni administrator by professional. Unapotaka kujua pesa kiasi gani imepelekwa kwenye Sekta ya Elimu usiangalie Wizara ya Elimu pekee, nenda kaangalie TAMISEMI, Utumishi na Elimu yenyewe. Na hata Wizara ya Afya ukitaka ujue pesa kiasi gani imepelekwa kwenye Sekta ya Afya nenda kaangalie TAMISEMI ndiyo utakuta ujenzi wa miundombinu, vituo vya afya na Hospitali za Wilaya na Wizara ya Afya yenyewe pamoja na Utumishi mishahara ya madaktari. Kwa hiyo, usiangalie Wizara ya Afya, nenda kaangalie na Wizara nyingine. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome Makamba unaipokea taarifa hiyo?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, hapana, naomba niendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasema kwamba asilimia 85 ya makusanyo ya Serikali wanakusanya mapato kutoka kwa wananchi mapato ya kikodi yaani hizo njia walizokuwa nazo na peremende na kila kitu wanatafuta asilimia 85 ambayo mwaka uliopita walifeli. Asilimia 15 wanategemea wafadhili na mikopo nafuu kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa angalia picha inavyokwenda, hawa wafadhili mwaka jana kwa mujibu wa Ripoti ya UNESCO walikata misaada Tanzania kwa zaidi ya asilimia 49. Na haya yote wameyasema kwa nini wamekata mikopo hiyo, wamekata mikopo na wamekata misaada. Hali ya demokrasia nchini siyo shwari, utawala bora hakuna, uhuru wa vyama vya siasa hakuna, hivi hao watu mnaotegemea watawapa hiyo asilimia 15 itatoka wapi? Wanakwenda kuwakamua Watanzania kwa kiwango ambacho mzalendo yeyote aliyepo humu ndani hawezi kukubaliana na hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kukubali Mheshimiwa Dkt. Mpango ku-support bajeti yako mpaka utakaponieleza ni vyanzo vipi vya uhakika ulivyojiandaa navyo vya kupata pesa kwa ajili ya kuendesha bajeti yako. Mpaka utakaponieleza ni lini utaboresha private sector ambayo ndiyo engine ya uchumi wa nchi, utaiboresha lini ili uitoe Serikali kwenye matrilioni ya kununua ndege, kujenga SGR na kwenda kujenga sijui mradi wa Mto Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo yafanywe na private sector, ninyi mtekeleze Katiba ya nchi yetu kama livyoapa kuilinda kwa kwenda kufanya maendeleo ya watu badala ya kufanya maendeleo ya vitu. Sitopiga kura ya ndiyo kwenye bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2019/2020. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)