Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa neema ya kuondoka CHADEMA kuja CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua nilikuwa kule ng’ambo kumbe nilikuwa sijui tulichokuwa tunakifanya kule, tulikuwa tunasema uwongo kwa kile tusichokiamini. Nimekuwa nikisawakiliza Wabunge wa CHADEMA na wa kule ng’ambo kwa ujumla wanasema Serikali ya CCM inafanya maendeleo ya vitu na siyo maendeleo ya watu, nawasikiliza nasema hawa vipi hawa au wamerogwa?(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Ayoub 13:4 inasema “lakini ninyi hubuni maneno ya uwongo, ninyi nyote ni matabibu wasiofaa”. Isaya 9:15 inasema “Mzee mwenye kuheshimiwa ndiye kichwa na Nabii afundishae uongo ndiye mkia”, Manabii wafundishao uongo ndiyo mikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina Ilani ya CHADEMA hapa. Nilikuwa Mbunge wa CHADEMA, niliinadi hii wakati nikiwa mgombea ninaijua na wanaijua. Leo nataka nipite humu tuangalie maendeleo ya vitu kwamba kweli Serikali ya CCM inafanya maendeleo ya vitu na siyo maendeleo ya watu, nitaangalia baadhi ya maeneo, naomba nianze na Bandari. Wao wanapinga ujenzi wa bandari na wanasema ukiangalia kwenye ukurasa wa 40 wa Ilani yao watafanya nini:

Kwanza ni kujenga reli mpya na kukarabati zilizopo kwa viwango vya kisasa kwa kuzingatia maslahi ya nchi. wanaopinga reli ya kisasa ya standard gauge ni akina nani?

WABUNGE FULANI: Wao.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni kuboresha zilizopo na kujenga mpya kama vitega uchumi vya Taifa. Tatu, ni kujenga Shirika la Ndege la Taifa linalojiendesha kwa misingi ya faida. Ndege zimenunuliwa wa kwanza kupinga ndege ni watu gani?

WABUNGE FULANI: Hao hao.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia ukurasa wa 41 unasema Shirika la Ndege la Taifa Air Tanzania…..

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Kuhusu utaratibu

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha subiri kidogo. Mheshimiwa Selasini naomba ukae kidogo. Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha pamoja na kwamba umenukuu kitabu cha dini kwamba kinawaita pengine watu wa aina fulani kwamba wao ni mikia na kitu kama hicho, lakini kwa kuwa sehemu hii Waheshimiwa Wabunge siyo kwamba vinakatazwa vitabu vya dini kunukuu, lakini pale ambapo ile lugha iliyotumika kwa sababu hatuna uwezo wa kuanza kutoa mahubiri na kutoa maana halisi ya hayo maneno humu ndani, yale maneno yako uliyoyachukua mwanzo, uliyoyanukuu kwenye kitabu cha dini Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha matumizi yake kwenye kusema nani ni mkia na nani siyo mkia hayataweza kutumika humu ndani kwa sababu siyo lugha ya Kibunge.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nimekuelewa lakini maana yangu ni kwamba, Ilani ya CHADEMA iliongelea ndege lakini wakija humu ndani wanakataa kwa nini? Ni watu wa namna gani hawa, tuwaite jina gani? Mimi acha niende. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 41 wa Ilani yao inasema: “mizigo yote mizito kusafirishwa kwa njia ya reli na meli” leo wanageuka hapa, tuwaite jina gani? hawa watu wa ajabu sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 45 wa Ilani yao wanasema kupiga marufuku uuzaji wa korosho ambazo hazijabanguliwa na kuhakikisha kwamba asilimia 100 ya korosho zote tunazozalisha zaidi ya tani 200,000 zinabanguliwa hapa Tanzania. Rais Magufuli amesema hakuna kuuza nje Korosho nini? ambazo hazijabanguliwa na akasema Wanajeshi, bangua hata kwa midomo yenu kabangue tuuze korosho zilizokuwa processed wanakataa. Wewe ngoja nipite kwenye Ilani tulia kwani mnaisomaga basi ninyi! Hawa wanaambiwaga fanya hivi wanafanya hata bila kufikiria.(Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 53 unasema: “vipaumbele havijawekwa kwenye uendelezaji wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme wa bei nafuu vilivyopo nchini, mfano Stigler’s kwenye Bonde la Mto Rufiji”. Wanasimama hapa wanapinga mradi wa umeme wa Stigler’s hawa tuwaite vipi, kwenye Ilani yao ipo hapa? (Makofi)

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. MARWA R. CHACHA: Tulia.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka nataka kuamini umezingatia matakwa ya Kanuni ya 68(8).

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimezingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nafurahi sana kuona mzungumzaji pale anakubali kwamba kweli CHADEMA tumeandaa Ilani sahihi kabisa kwa ajili ya kuendesha Taifa hili na Serikali ya CCM imeyachukua na sasa hivi inayatumia kuhakikisha kwamba inatekeleza majukumu yote ambayo tulikuwa tumeweka kwenye Ilani yetu. Tunashukuru sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakajoka, hapo sasa ni ufafanuzi wa jambo gani uliloeleza? Kila wakati nawakumbusha matumizi ya Kanuni.

Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, endelea na mchango wako.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru leo baada ya kusoma hili andiko wamekubali kwamba CCM inafanya kazi, ahsante sana. Leo ndiyo wamekubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia ukurasa wa 57 pia wameongelea, Serikali ya CHADEMA sio ya UKAWA, Serikali ya CHADEMA itaupa uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji kipaumbele namba moja, yaani nyie vigeugeu kweli kweli sijawahi kuona. Imeandikwa kwamba kipaumbele cha kwanza cha uzalishaji wa umeme, cha kwanza maji, wameandika kwenye Ilani. Leo akisimama pale anasoma huwa nakaa nawaangalia hivi hawa wako sawasawa hapa kweli? Serikali ya CHADEMA itaupa uzalishaji mkubwa wa umeme wa maji kipaumbele namba moja, umeme wa makaa ya mawe kipaumbele namba mbili, umeme wa gesi asilia kipaumbele namba tatu, muende mkasoma Ilani yenu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi namshukuru Mungu kwa kuniipa neema ya kutoka kule. Unajua wale watu ukisema moja ongeza moja ni mbili, CCM akisema moja ongeza moja ni mbili wao watasema ni saba.

TAARIFA

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Goodluck.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa anayeongea kuwa CHADEMA walikopa kwetu mgombea pamoja na Ilani. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hebu…

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee.

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa Ryoba.

Waheshimiwa Wabunge, Kanuni hizi zinatutaka tutumie wakati wetu vizuri. Kwa hiyo, zinavyosema taarifa unakuwa unatoa ufafanuzi kwenye jambo analochangia mtu mwingine, kwenye hoja yake. Mheshimiwa Ryoba Chacha.

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, unaona ukurasa huu kwenye hii Ilani, Mheshimiwa Mlinga alisema Lowassa ndiye aliyeandika Ilani wakakataa, ona kwenye huu ukurasa picha ya Lowassa hii hapa. Kwa hiyo, Lowassa alivyotoka CCM aliondoka na ile Ilani ya CCM aka- copy akapeleka kule.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MHE. MARWA R. CHACHA: Ndiyo, huo ndiyo ukweli.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MHE. MARWA R. CHACHA: Hii hapa, anayebisha asimame apinge, mimi ninayo hii hapa, hakuna wa kupinga wanajua ni ukweli. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya CHADEMA na UKAWA ilikuwa ni ufisadi, Mheshimiwa Magufuli ameshughulika na ufisadi. Unawasikia wanaongelea ufisadi sasa hivi, kimya, hola hamna kitu, yaani sasa hivi hawana hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine wanasema ukurasa wa 37, sekta ya bandari imegubikwa na rushwa pamoja na utendaji mbovu kiasi kwamba mrundikano wa mizigo umekuwa mkubwa sana bandari na kupelekea mapato yake kuwa madogo kulingana na fursa za usafirishaji. Mheshimiwa Magufuli alivyoingia tu madarakani ziara zake za kwanza zile alienda wapi?

WABUNGE FULANI: Bandarini.

MHE. MARWA R. CHACHA: Bandarini akaenda akafumua, kuna watu walijifanya Miungu, eeh Mheshimiwa Magufuli ni mwanaume, haki ya mama. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, nilikuwa nataka kuwakumbusha tu kwamba waiunge mkono Serikali ya CCM maana inafanya mambo mazuri kama mimi nilivyofanya ukienda Serengeti sasa hivi mambo safi kabisa. (Makofi)