Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi asubuhi ya leo, naomba nianze na pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu yao yote kwa kutuletea bajeti nzuri sana, sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais amethubutu, leo tunazungumzia Tanzania ya viwanda kwa vitendo na mimi ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, nasema sera inatekelezeka! Wanaosema sera haitekelezeki, waje kwenye kamati yangu. Twende Kibaha tukaangalie viwanda vipya vilivyojengwa, twende maeneo yote tukaangalie viwanda vilivyoshamili, njooni tuangalie wawekezaji wanavoingia Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sera ya viwanda inatekelezeka kwa vitendo na Mheshimiwa Rais tumemshauri kama Kamati, akae na wadau azungumze nao, amekuwa msikivu, amekaa na wafanyabiashara, amekaa na wadau na amewasikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, ni Rais wa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaozungumza maneno ya pembeni wameishiwa hoja, Mwenyekiti wa kamati ndiyo mimi. Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda ndiyo mimi, ukweli naujua mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amefanya mambo ambayo tumemshauri sisi, zile tozo zote zilikuwa ni kero, leo tozo 54 zimeondoka, siyo jambo dogo. Hilo ni jambo kubwa na la mfano na la kuigwa na la kupongezwa na ametekeleza Ilani ya chama chake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais katika hili tunakupongeza, tuko na wewe, kanyaga twende. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Bashungwa, nimpongeze Ndugu Mhede, karibuni katika mchakato huu tusaidiane tufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongee kidogo muda unakwenda, nizungumzie suala la TRA. TRA kuna utaratibu ambao unasababisha wafanyabiashara na Watanzania wapate shida. Shida namba moja ni zile fomu za TIN, fomu zile zinaandikwa kwa kiingereza, wale wafanyabaishara wanapata shida kuzijaza, fomu zile zina urasimu, matokeo yake kuna vishoka wamekaa nje kwenye Ofisi za TRA, wanachukua zile fomu wanawajazia watu na vishoka wale wanawa-charge Watanzania shilingi 10,000 hadi shilingi 20,000; TRA tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fomu zile zimepitwa na wakati, wakati fomu zile zinaandaliwa nchi ilikuwa haina Vitambulisho vya Taifa, sasa hivi tuna vitambulisho vya Taifa vina kila kitu ndani, anuani zote zimo ndani, kile kitambulisho kinatosha kabisa kutengeneza fomu ambayo ni very simple na fomu hizohizo zina matatizo upande wa BRELA, nawaomba TRA waliangalie hili, fomu zilizopo zinaleta urasimu na vishoka tunawapa muda wa kutafuta fedha nje ya utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumze kwa upande wa TRA ni suala la kodi. Tumepunguza hizi kodi nyingi sana, sasa tunaomba wakasimamie ukadiriaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo lipo kwenye assessment, pale kwenye assessment ndiyo kuna matatizo, DG mpya tuna matumaini na wewe, ulikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda nakufahamu uwezo wako. Nenda kaibadilishe TRA. TRA ikibadilika uchumi wa nchi utakua, TRA ikiwa rafiki wa wafanyabishara, tutasonga mbele kwa kasi kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee kidogo suala la fedha za kigeni, niongee na Gavana kama yupo. Hatua zinazochukuliwa na Serikali tunaziunga mkono, lakini naomba ifahamike, biashara za Dubai, China na nchi nyingine duniani, biashara kubwa hizi zimetawaliwa na suala la kulipa fedha taslimu. Unapokwenda Dubai kununua mzigo, ukinunua mzigo wa dola laki moja, wale wafanyabiashara wanataka cash dola laki moja. Sasa je, utaratibu wa kupeleka cash dola laki moja ukoje? BOT watusaidie namna bora ya kuhakikisha biashara zinarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kariakoo imepotea katika ramani ya biashara. Tulikuwa tuna Kariakoo ya Burundi, Rwanda, Malawi, Uganda na Congo, leo Kariakoo ile imepotea
kwenye mtandao haipo na sababu ya kupotea ile Kariakoo zipo nyingi ikiwemo suala la namna ya kupeleka fedha za kigeni Dubai, China na nchi nyingine, lakini leo kwa ruhusa yako Kamati ya Bajeti tulikwenda Uganda na mimi nilikwenda. Unafika Uganda unawauliza wafanyabiashara wa Uganda mbona siku hizi hamji Dar es Salaam kuchukua mzigo wanakwambia sasa hivi wa Dar es Salaam wanakuja kwetu, wa Malawi wanakuja kwetu, wa Rwanda wanakuja kwetu. Hayo ndiyo majibu tuliyopewa Uganda na wale bahari hawana, Bandari hawana. BOT tujiulize kuna nini hapo, TRA tujiulize kuna nini. Kwa nini tumelipoteza soko ambalo lilikuwepo Dar es Salaam, soko la Kariakoo. Bidhaa zile zilikuwa zinapatikana pale zina grade zake. Ukinunua mzigo kule Dubai, China kuna light weight, kuna heavy weight sasa zile biashara zilizokuwa zinafanyika TRA wao hawajui light, hawajui heavy, hawajui nini, wao ni kodi, kodi, kodi matokeo yake tumeua mtandao wa biashara, tumewakatisha tamaa wafanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunatakiwa tufungue milango ya Kariakoo, leo tunatakiwa tujiulize tumekosea wapi, tumekwama wapi. Mheshimiwa Dkt. Mpango tukae tusaidiane tufanye mawazo ya pamoja, tuzungumze hili tuna ushahidi, tuna nia ya kusaidia eneo hili lirudi katika mtandao wa biashara katika nchi zote za maziwa ambayo yametuzunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie Mfuko wa Mazingira; Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kulikuwa na Mfuko wa Mazingira ulikuwa una kazi nzuri ya kufanyakazi ya mazingira kwenye Nchi yetu. Mfuko huu mwaka jana 2018/2019 ulitengewa bajeti ya shilingi milioni 500 fedha zile hazikutoka. Dkt. Mpango alivyokuja kwenye Kamati ya Uongozi na Bajeti akaahidi 2019/2020 zile milioni 500 zitawekwa. Nashangaa, naona zile milioni 500 hazipo na ule mfuko hauna hata senti moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni mwanamazingira, Mfuko wa Mazingira hauna senti hata moja maana yake una zero na mfuko haupo. Nimuombe Dkt.Mpango rudisha kauli yako, zile milioni 500 ni ndogo mno tuanze na hizo. Tukipata shilingi milioni 500 tunaanza hapo. Hilo ni la Mfuko wa Mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba niende Mvomero; Mvomero tuna barabara ya lami inayoanzia Magole-Turiani- Mziha-Handeni-Korogwe. Barabara ile iliwekwa na Serikali makusudi ni barabara mbadala kwa ajili ya barabara ya Chalinze-Segera. Kilometa 48 zimeshawekwa lami Turiani- Magole bado Turiani-Mziha-Handeni. Mwaka huu niipongeze Serikali wameweka bilioni moja katika barabara hiyo, naomba sasa barabara hiyo itangazwe, mradi ule uanze ili barabara ile ifunguke. Wenzetu wa Handeni-Korogwe waliashaweka lami kwenye barabara yao.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala la mazao ya biashara; kule kwangu wanalima miwa, Kagera kule wanalima kahawa, Mwanza wanalima pamba, eneo hili tuna shida. Eneo hili tuna shida, nimpongeze Waziri amezungumzia kahawa na wanasema katika hotuba yake kwamba watalinda kahawa lakini mimi napata shida kidogo; hotuba ya kiingereza ya Waziri inazungumzia roasted coffee. Wale watu wa Kagera wanataka instant coffee inayokuja kutoka nchi za nje ndiyo ushuru wake upandishwe kwa sababu viwanda vilivyopo Tanzania vya instant coffee ndiyo vinapata ushindani mkubwa. Sasa kwenye hotuba yake amezungumzia kahawa, hotuba ya kiswahili amezungumzia kahawa, lakini kwenye hotuba ya kiingereza amezungumia roasted coffee.

SPIKA: Ahsante Mwenyekiti.

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia, ahsante sana. (Makofi)