Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Kwanza naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili naomba nimshukuru sana Mungu, kwa kunijaalia kufikia nafasi hii, na kwa kweli kwa kupata nafasi ya kushiriki katika Wizara hii, Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini kipekee kupata nafasi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika juhudi zake za kuwakomboa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniamini na kunipa nafasi, na kufanya kazi hii, naamini sifa ya ziada kuliko watu wengine lakini ilimpendeza niweze kumtumikia katika nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ili kuyaweka vizuri maneno yangu, naomba wale ambao huwa wanasoma biblia watasoma katika zaburi ya 116 mstari wa 12 na inasema nimtumikie nini Bwana katika mambo yote aliyonijalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana viongozi wote, Makamu wa Rais, na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote ambao nimekuwa nikipata ushirikiano mkubwa. Kipekee naomba nitumie nafasi hii, kumshukuru sana Waziri wangu wa Maliasili na Utalii kwa namna ambavyo ananipa ushirikiano na kwa kweli kwa namna ambavyo ananipa miongozo mingi katika kufanikisha kazi yake. Ninaishukuru sana ofisi yako na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla, nimepata ushirikiano mkubwa sana kwenye Kamati na naishukuru sana Kamati kwa namna ambavyo imekuwa ikitusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niwashukuru pia wapiga kura wangu. Tulizoea siku zote baada ya Bunge nilikuwepo muda wote jimboni lakini sasa hawanioni lakini wameendelea kuwa na imani na mimi. Ninaishukuru pia familia yangu, kwa uvumilivu wote ambao wameupata hasa katika muda huu ambapo muda mwingi sipati muda wa kufanya kazi na familia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani zote hizo, naomba sasa nitumie nafasi hii kujibu maeneo machache ambayo naweza kupata nafasi kwa dakika hizi kumi na tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, nianze labda na tatizo la udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu. Serikali imechukua hatua nyingi za kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo, mamba na viboko. Kimsingi pamoja na hatua zote ambazo tulikuwa tunachukua, tulikuwa na tatizo kubwa la kanuni; kwa hiyo tumeanza kuandaa kanuni za shoroba na maeneo ya mtawanyiko ya wanyamapori kwa lengo la kuhifadhi na kupunguza migongano baina ya wananchi na wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeendelea kuendesha doria za kawaida za pamoja ili kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, kuelimisha wananchi kuhusu matumizi ya mbinu tofauti kama vile kuweka mizinga ya nyuki, kulima pilipili kwenye mipaka ya mashamba, kuweka oil chafu kwenye maeneo ya mashamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kushirikiana na halmashauri kuunda na kuwezesha vikundi vya kijamii vinavyodhibiti wanyama waharibifu, kufatilia mienendo ya wanyamapori hususan tembo; na hivi karibuni tulimshuhudia Mheshimiwa Waziri akiwavalisha mikanda ya kielektoniki
yaani (callars) kwa lengo la kubaini mienendo yao. Pia kuendelea na mipango mikakati ya kitaifa ya namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakiri kwamba hivi karibu kumekuwepo sana na tatizo kubwa sana wanyamapori kuzagaa katika maeneo mengi, na hii inatokana kwa kweli na sasa wanyama wamekuwa huru. Mwanzo walikuwa wanawindwa hovyo na kwa sababu hiyo ulikuwa unaweza kufikiri kwamba sasa wanyama wamekwisha Tanzania, lakini baada ya udhibiti mkali, sasa wanyama imekuwa kila unapoamka asubuhi unasikia wanyama wako kila eneo wamezagaa. Kwa hiyo tumeendelea kuweka Mipango Mikakati ya kukabiliana na changamoto hiyo ambayo tunaamini kwamba baada ya mikakati hiyo Wizara yetu itafanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika kukabiliana na changamoto ya watu ya kuuwawa na Mamba. Wizara imefanya sensa nchi nzima ambapo mwezi Oktoba mwaka jana mpaka Novemba taarifa ya sensa imeonesha kwamba, mamba wameongezeka katika maeneo yaliyohifadhiwa na mamba wamepungua katika maeneo ambayo hayakuhifadhiwa. Wizara itafanya utaratibu wa kuwavuna hawa mamba na utaratibu huu tayari tunauandaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imefanya sensa ya Viboko katika maeneo ya Mafia na maeneo mengine. Takwimu zinaonesha kwamba katika Kisiwa cha Mafia viboko wako sasa kumi na sita na kuna mabwawa matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Changamoto ya wanyama hawa katika kisiwa hiki inaonekana kwamba inapanuka kwa sababu wanashambulia watu na kuvamia mashamba. Wizara itafanya juhudi za kutoa elimu kwa wananchi lakini pia tutawavuna viboko wakorofi ambao wamekuwa wakishambulia watu na mashamba ili kuwapunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yetu inafahamu kwamba ziko changamoto za malipo yanayotokana na shambulio la wanyama waharibifu. Ni kweli kwamba kifuta jasho kimekuwa ni kidogo lakini na kifuta machozi. Wizara inaendelea kufanya mapitio ya Kanuni za kifuta jasho na kifuta machozi na tayari wataalamu wa Wizara wameandaa andiko na mapendekezo hatua inayofuata ni kupeleka rasimu ya Kanuni ya hizo kwa wadau mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya kanuni hizo yanakwenda sambasamba na mabadiliko ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya Mwaka 2009. Wizara pia inaendelea kulipa malipo ya kifuta jasho cha machozi kadiri madai yanavyowasilishwa, na kwa mwaka 2018/2019 jumla ya shilingi bilioni moja, milioni mia nne na ishirini sita, laki sita na thelathini na sita na mia tano zimelipwa kwa wananchi 7,320, hawa ni kutoka katika Wilaya 57. Kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni arobaini na mbili zimelipwa kwa wananchi 148 kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa. Malipo hayo yamefanyika tarehe 12 Februari.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba madai yako mengi na yanashughulikiwa; na Mheshimiwa Catherine alitaka orodha ya watu waliolipwa Serengeti, namuomba Mheshimiwa Catherine kama hatajari baada ya kikao hiki, tunaweza tukawasiliana tukampatia hiyo orodha kwa sababu ni Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, malipo ya kifuta jasho au kifuta machozi yalikuwa yanachelewa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kuchelewa kwa kuwasilishwa kwa taarifa kutoka kwa waathirika kwa sababu zipo taratibu nyingi ambazo zinatakiwa kupitiwa kabla ya kufikia hatua ya kupata malipo. Wizara kwa kushirikiana na Giz, inaboresha mfumo wa kuwasilisha taarifa kwa kuanzisha kanda nne ambazo zitakuwa zinapokea na kufanya tathimini ya athari zinazotokana na shambulio hilo, ambazo tunazipokea Wizarani kwa njia ya elektoniki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na Taasisi zake inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu za kuwasilisha madai kwa mujibu wa sheria lakini pia ndani ya wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maeneo machache tu ya Waheshimiwa Wabunge ambayo walisema yalishatolewa maelekezo na Wizara yangu lakini hayajafanyika. Nikianza na Mheshimiwa Dkt. Kikwembe, amezungumza kuhusu suala la watu wetu wa TANAPA kugonga mtu na baadaye hawakusimama na haijulikani malipo hayo. Suala hili ni la kisheria linashughulikiwa kisheria na ninaamini pale ambapo mfumo wa kisheria utakapokamilika haki za aliyegongwa zitapatikana kulingana na kheria kwa sababu gari zile ziko insured

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili amezungumzia kuhusu kisima; TANAPA tayari wameshatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Kanda hiyo kukamilisha kisima hicho kama nilivyonitoa maelekezo wakati najibu swali. Kwa hiyo kisima hicho kitakamilika na wananchi watapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Malocha, alizungumzia usumbufu wanaoupata wananchi wa Ziwa Rukwa wanapokwenda kuvua, na akaeleza kwa masikitiko makubwa kwamba wananchi wamekuwa wakinyang’anywa mali zao na mitumbwi yao kubomolewa na afisa wetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara yangu ilishachukua hatua, Katibu Mkuu wa Wizara alituma ujumbe wa maafisa watatu kwenda kuchunguza malalamiko haya ya kinidhamu, ambayo Mheshimiwa Malocha aliyaleta ofisini, pamoja na Mbunge wa Viti maalum na tayari taratibu za kiofisi zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Malocha, baada ya tu ya Bunge hili nilikuwa nimekuahidi kwamba tutakwenda katika eneo hilo kufanya mkutano na wavuvi na kuwasikiliza, na pale ambapo hatua italazimika kuchukua pale pale tutachukua kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Getere, amekuwa akilalimikia kuhusu Kituo chake cha afya ambacho kimejengwa na taasisi yetu ya TANAPA, kimekamilika kwa miaka miwili iliyopita lakini hakifanyi kazi. Ni kwamba tayari uongozi wa TANAPA umeshamwelekeza Mkurugenzi wa Kanda hiyo ya Magharibi kukamilisha kituo hicho ili kiweze kufanya kazi haraka, na tayari pesa za Kituo hiki zimekwisha tengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwepo ahadi ya Mheshimiwa Waziri katika eneo la Kihibu, Waziri alifanya ziara na akaahidi milioni thelathini kwenye jimbo la Mheshimiwa Getere. Tayari aliwaelekeza TANAPA kuhakikisha kwamba pesa hizo zinatolewa na zinatolewa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, kwanza kwa pongezi zao ambazo wametupatia katika Wizara, lakini kwa ushirikiano mkubwa ambao wamekuwa wakitupa. Tuwahakikishie kwamba sisi ni watumishi wao; kwa hiyo pale ambapo wanadhani tunahitaji kutoa ushirikiano tuko tayari muda wote masaa yote kufanya kazi hiyo bila kubagua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Nakushukuru sana, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)