Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MOHAMED H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza ndugu yangu, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, Waziri wa Maliasili pamoja na mdogo wangu Mheshimiwa Kanyasu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara yao, waendelee kuchapa kazi, sisi tuko nyuma yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajielekeza kwenye ushauri zaidi. TANAPA - Hifadhi ya Taifa tulikuwa tuna hifadhi 16 na katika hifadhi 16 hifadhi tano tu ndizo zilizokuwa zimeweza ku-break even point; Hifadhi ya Arusha National Park, Kilimanjaro National Park, Serengeti, Manyara na Tarangire, lakini hifadhi nyingine 11 zilizokuwa hapo awali zilikuwa hazijaweza ku-break even point na sasa hivi tumeiongezea TANAPA hifadhi nyingine tano kwa hiyo, wana hifadhi 11, kwa hiyo, mzigo uliokuwa unaendeshwa katika hifadhi hizi nyingine 11 umeongezewa nyingine tano zimekuwa 16, kwa hiyo, kwenye eneo hili tuna hifadhi 16 ambazo hazi--break even point, kwa hiyo, TANAPA tumewaongezea mzigo mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tunatakiwa tuliangalie kwa makini. Lengo letu ni kuhakikisha hizi hifadhi zinatuletea mapato ya kutosha, lakini kama hatutakuwa tuna mkakati mzuri wa kuhakikisha tunazisaidia hizi hifadhi zikapata mapato ya kutosha hilo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hifadhi kama Saadani. Saadani ina utalii wa aina yake, hapa tunaweza tukapata hadi maeneo ya fukwe. Sasa naiomba sana Wizara ije na mikakati mizuri ambayo itatusaidia kwenye hifadhi hizi 16 ambazo tumeziorodhesha sasa ziweze ku--break even point, otherwise tutakuwa hatuna sababu ya kuongeza kwa sababu kwenye taarifa yake ambayo Waziri ameizungumza amesema bado kuna hifadhi mbili kwa maana ya Moyowosi na Rubando Rumanyika, wanataka kuziingiza kwenye Hifadhi za Taifa kwa hiyo, tutakuwa tunazidi kuwaongezea hawa wenzetu wa Nationa Park mzigo mzito. Tunajua Dkt. Kijazi anafanya kazi nzuri, lakini watakuwa wanambebesha mzigo ambao atakuwa anashindwa kuufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwenye eneo hili, gawio ambalo linapelekwa kwenye Serikali Kuu hawa wenzetu wangeli-retain kusudi waweze kuzihudumia hizo hifadhi zilizobaki kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie hili. Tunataka hizi hifadhi ziendelee kutupatia pesa, kwa hiyo, hilo gawio tuli-retain kwenye hizi hifadhi kusudi hawa wenzetu wa National Park waweze kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima wenzetu watuambie wana mikakati gani ambayo wameitengeneza kwa ajili ya kuhakikisha wanaboresha utalii hapa nchini? Sisi kama Watanzania tumekuwa mara nyingi tunategemea utalii wa nje; je, tuna mikakati gani ya kuhakikisha tunakuza utalii wa ndani?

Mheshimiwa Naibu Spika, utalii wa ndani unaweza kuboreshwa tu kama tutatengeneza infrastructures za uhakika ambazo zitawasaidia watu wa kawaida waende kutalii ndani. Gharama za utalii zikiwa ziko rahisi zaidi Watanzania wengi watapata nafasi ya kwenda kupumzika. Kwa mfano Saadani, Mbuga ya Saadani iko karibu na mikoa mashuhuri kama Mkoa wa Dar-es-Salaam, Morogoro na kadhalika, kama tutaitengezea utaratibu wa infrastructure kwa maana ya maboma mle ndani yakawa bei rahisi, itakuwa rahisi kwa watu siku za weekend, Jumamosi na Jumapili kwenda pale Saadani na kupumzika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka kuchangia ni suala la Ruaha National Park. Ruaha National Park ni mbuga ya pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika baada ya Mbuga ya Kruger ile ya South Africa, lakini pamoja na ukubwa uliokuwepo hii mbuga inaonekana iko idle na hakuna mkakati wowote ambao unaonesha unataka kuikuza hii Mbuga ya Ruaha National Park. Kwa Sababu tuna interest ya kuhakikisha utalii ulioko pale katikati ya Tanzania uwe unalingana na ule wa Kusini mwa Tanzania, kwa hiyo, tutengeneze mkakati tuhakikishe na mbuga kama ya Ruaha Nationa Park inapewa kipaumbele na inaboreshwa kusudi iwe miongoni mwa mbuga muhimu katika nchi yetu. Ruaha National Park ni mbuga ambayo ina tembo wakubwa ambao huwezi kuwalinganisha na tembo wanaopatikana katika maeneo mengine yoyote hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilipenda kuchangia ni eneo la msitu na eneo hili nataka tena kutoa ushauri. Mheshimiwa Waziri naomba atusaidie sana tuangalie bei na tozo mbalimbali kwenye eneo hili la mazao ya misitu. Biashara ya msitu katika Mikoa ya Njombe na Iringa ni moja ya biashara nzuri sana katika mkoa wetu, lakini cha kusikitisha kwa sababu ya tozo hizi zilizopo biashara hii imeshakuwa ngumu. Uchumi wa Mufindi ulikuwa unategemea sana biashara ya msitu, lakini kwa sasa hivi kutokana na tozo zilizopo nyingi kwenye hili eneo imekuwa ngumu hizi biashara kufanyika kwa hiyo, watu wameshaanza kuhama. Mbao zimekuwa bei ghali kwa hiyo, kumetokea mbadala, watu badala ya kuezeka kwa kutumia mbao, sasa hivi wanaezeka kwa kutumia vyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aliangalie hili jambo. Tumewekeza hela nyingi kwenye eneo la msitu, lakini tukiendelea kuliacha hili zao likaendelea kukaa kwa utaratibu huu litapotea kabisa na msitu utakuwa hauna thamani tena. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri zile tozo zilizopo kwenye eneo hili ziangaliwe upya na thamani na gharama za kuuza mbao kwenye eneo hili tuziangalie upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri ni mahusiano, Mheshimiwa Waziri angetusikiliza ingekuwa bora zaidi kuliko anachokifanya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahusiano yaliyopo kati ya maliasili pamoja na maeneo yetu katika Majimbo ya Mufindi Kaskazini; katika Jimbo la Mufindi Kaskazini ni eneo ambalo tumewekeza sana katika Mradi wa Sao Hill kwa maana tumepanda miti mingi, lakini infrastructure nyingi zinaharibiwa sana wakati wa uvunaji wa misitu, lakini maliasili hawachangii chochote katika utengenezaji wa ile miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri jambo hili aliangalie kwa kina. Sisi watu wa Mufindi Kaskazini hili jambo linatusikitisha sana. Tukiwaomba hata siku nyingine wenzetu watupe makatapila na mimi kama Mbunge wao nitoe hela kidogo katika Mfuko wa Jimbo nichangie, hawako tayari kwenye jambo hili. Kwa hiyo, itafika kipindi sisi watu wa Jimbo la Mufindi Kaskazini tutakataa wenzetu wasiende tena kwenye msitu, watumie barabara za kwao, wasitumie barabara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha atwambie tunajengaje mahusiano ya kuhakikisha wenzetu walioko kule Sao Hill wanatusaidia katika kutengeneza infrastructure za barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho ambalo nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, kule katika Jimbo la Mufindi Kaskazini kuna maeneo mawili ambayo ni mazuri sana kwa ajili ya utalii. La kwanza lipo Mpangatazara. Kule Mpangatazara kuna kisiwa ambacho kinahama, asubuhi utakuta kisiwa kiko kushoto baadae utakuta kiko Kaskazini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri namwomba sana Waziri awatume wataalam wake waje kwenye maeneo yale na waangalie, pale pana utalii mkubwa kwenye hilo eneo la Mpangatazara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine katika eneo hilo kuna waterfalls za Mpangatazara ambazo huwezi kuzipata sehemu yoyote hapa nchini. Kwa hiyo, utalii uko kwenye maeneo mengi, lakini kitu kingine, tulikuwa tuna vyura va Kihansi ambao walivuma sana miaka ya nyuma, lakini leo hatusikii chochote kuhusu vyura wa Kihansi, vyura hawa wanazaa, hakuna vyura wowote hapa duniani ambao wanazaa. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, wenzetu wazungu walikuja wakawachukua wale vyura wakawapeleka Ulaya, lakini sisi Watanzania tumenyamaza kimya hatutaki kuendelea kuukuza utalii katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atwambie sisi kama Watanzania tuna mkakati gani kuhakikisha tunaendelea kuenzi eneo hili la utalii wa vyura ambao wanazaa ambao huwezi kuwapata sehemu yoyote hapa duniani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Nawataka vijana waendelee kuchapa kazi. (Makofi)