Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Pudenciana Wilfred Kikwembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kavuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia niweze kuchangia katika hotuba hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa napenda niwapongeze Mawaziri wote na viongozi wote wa Wizara chini ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo mmekuwa mkifanya kazi kwa bidii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja katika Sheria ambayo inaongelea mazao ya misitu ambayo ni Sheria ambayo inasema kwamba ni The Forest Act Cap 323 ni Sheria ya TFS agency ambayo schedule yake namba 8 na 14 zilizofanywa marekebisho kwa mwaka 2017.

Mheshimia Naibu Spika, naomba niende moja kwa moja kwenye fees na loyalty for forest product and services. Nimesimama hapa kutokana na malalamiko ya wananchi ambao Sheria hii imekuwa kwao ni kandamizi, imekuwa kwao ikiwaonea na kama ilikuwa ikifanya kazi kipindi kile kwa sasa hivi nafikiri haiko sawa sawa. Kwa hiyo ni vyema sasa niiombe Wizara waweze kuileta hii Sheria tuweze kuifanyia marekebisho iende na wakati kutokana na kwamba Mheshimiwa Rais amekwishatamka tozo zozote na fees zozote tunazoona kwamba zinawakandamiza wananchi tuzirekebishe ili tuweze kuendelea kupata mapato kwa urahisi na kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ninaongea nini shatter ya milango kwa one piece shatter ya mlango, kutoka Mpanda Mjini kwenda Jimboni kwangu Kavuu halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine wanatozwa per piece one shatter shilingi 50,500. Fremu moja ya mlango ama dirisha moja kutoka Mpanda Mjini kwenda Jimboni kwangu Kavuu shilingi 51,800, wakati shatter ya mlango pale Mpanda ataitengeneza kwa shilingi 22,000, mnamtoza 50,000 bado hajasafirisha kwenye gari kutoka Mpanda kwenda wapi kwenda Kavuu. Hii maana yake nini, maana yake mnawaambia wananchi wangu wa Kavuu hawapaswi kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye kima cha kati, kwa maana kwamba lengo tunataka kujenga uchumi wa kima cha kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lazima sasa hizi fees tuziangalie, lakini utakuta kuna kitanda shilingi 20,000, uyoga shilingi 200, sasa yaani unashindwa kuelewa, kiti ama stuli shilingi 17,250, dawati la shule mzazi ametengeneza dawati anapeleka kule Kavuu shilingi 17,250 kutoka halmashauri kwenda halmashauri yaani inamaana hizi ni fees ndani ya Mkoa mmoja. Kitu ambacho nafikiri ilikuwa imewekwa kwa ajili ya ku-discourage labda wale wafanyabiashara wakubwa wanaosafirisha mininga labda kutoka Inyonga kule kupeleka Mkoa mwingine na kwamba Mkoa mwingine unazilipia hizo fees.

Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana mfano mkeka ama kikapu unaambiwa ulipe shilingi 1,700, vitu vidogo vidogo vinavyotokana na mbao nikimaanisha labda mwiko, kijiko kwamba shilingi 1,700. Sasa nashindwa kuelewa, kama tunaona hizi zimekuwa ni kero naomba tuziondoshe kama Rais anavyoelekeza ili wananchi waweze kulipa vizuri na tuweze kuongeza mapato kwa wingi kwa sababu haiwezekani ndani ya Mkoa uka-charge hivi vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mila na desturi, binti anapoolewa anapewa kitanda, anapewa sofa, atapewa godoro hivyo vitu vyote lazima alipie sasa inakuwa kwa kweli haileti maana kabisa hata kidogo. Ukizingatia kwangu ni halmashauri mpya sitarajii na wala hatutarajii kuwe mafundi wengi wa kusema kwamba kule watajitosheleza wasiweze kusafisha, kwanza Mininga sasa hivi hakuna ndiyo tunaanza kusubiria ianze kuota upya kwahiyo naomba sana muangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nikumbushie tena kuhusu suala langu katika Kata ya Mwamapuli, Kata Luchima, Kata ya Majimoto Kijiji cha Luchima; pale tuliwaomba na TANAPA wamekwishaanza kutengeneza kisima kile. Naomba kisima kile kimaliziwe ili tuondoe mgogoro kati ya wananchi wanaotumia maji katika ule mto unaopakana na mbuga. Wananchi wamekuwa wakipigwa sana na Askari wa TANAPA na nimekwishaongea na wamekwishaanza kwanini hawamalizii kile kisima ili tuondoe migogoro inayotokea kati ya Wannachi pamoja na hao watu wa TANAPA.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niulize na naomba tena niongelee suala lingine; Askari wa TANAPA kati ya mwaka juzi na mwaka jana katika Kata ya Kibaoni walimgonga Mama mmoja pale na kwa bahati nzuri nafikiri nilikuwepo Jimboni yule Mama alifariki pale pale. Sasa naomba nielewe ni fidia ili mtampa yule Baba, huyo ni Mzee pale anaitwa Mzee Lusambo mke wake ndiye aliyegongwa na gari na wale TANAPA hawakusimama walipitiliza walichofanya ni kusaidia tu maziko. Kwa hiyo, nilikuwa naomba ni namna gani huyu Mzee Lusambo sasa kupitia kifo cha mke wake mtampa fidia ili naye aweze kuona kwamba angalau Serikali imeweza kumjali kwa sababu wanapita kwa speed kali kiasi kwamba inabidi muwe waangalifu na kuangalia namna ambavyo mtavuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nirejee katika kisima change cha Luchima, naomba kikamilike na ikiwezekana kikamilike mapema iwezekanavyo, Mheshimiwa Naibu Waziri uliniambia kwamba umekwishaongea na watu wa TANAPA na najua wako hapa, Mkurugenzi Kijazi yuko hapa, naomba sasa umuelekeze kile kisima kiishe haraka iwezekanavyo kabla ya Septemba kiwe kimekwisha na Wananchi waanze kutumia maji yale kuepuka vurugu ambazo wanazipata kutokana na Askari wa TANAPA.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sina mengi zaidi ya kuiomba Serikali ilete hiyo Sheria ili tuweze kuifanyia marekebisho Wananchi waweze kunufaika na mazao na vitu vyao wanavyosafirisha. Meza imekwishatumika una sababu gani ya kum-charge mtu wakati ana hama kutoka halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine? Na siyo kitu kipya na wala hakijazidi hata tani moja kwanini um- charge? Kwa hiyo, hizo ndiyo kero ambazo naziwakilisha kutoka kwa Wananchi wangu wa Jimbo la Kavuu ambao wamekuwa wakilalamika kila siku namna wanavyo hapa kutoka Mpanda Mjini kwenda Kavuu kwa ajili ya kufanya shughuli zao za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipatia nafasi hii, naunga mkono hoja, naomba Serikali mzingatie haya yote niliyokwisha waeleza, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)