Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri na lenye kuleta matumaini.

Mheshimiwa Spika, suala la bandari ya uvuvi limekuwa linasuasua kwa muda mrefu sana. Mwaka wa fedha 2013/ 2014 zilitengwa fedha kwa ajili ya pre-feasibility study na kiasi cha shilingi milioni 500 na mshauri elekezi alilipwa na kazi ilifanyika na mpaka sasa hatujui matokeo ya kazi ile. Baadaye fedha zimekuwa zikitengwa kila mwaka kwa kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, hata bajeti hii tunayoitekeleza 2018/2019 zimetengwa fedha kwa ajili ya bandari hiyo ya uvuvi lakini hatuoni matokeo yeyote; na mpaka sasa hata eneo la kujenga bandari hiyo bado halijapatikana. Kwenye bajeti ijayo kupitia kitabu chake Mheshimiwa Waziri anaomba aidhinishiwe shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kazi ileile ya ushauri elekezi.

Mheshimiwa Spika, faida za bandari ya uvuvi ni nyingi ikiwemo utoaji wa ajira kwa vijana wetu nimuombe Mheshimiwa Waziri kuwa sasa fedha hizi bilioni 1.4 ziende na kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, uvuvi katika bahari ni fursa ambayo nchi inatakiwa iitumie vema. Kwa sasa uvuvi katika Bahari Kuu umedumaa na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Deep Sea Fishing Authority (DSFA) kwa sasa ipo katika hali mbaya sana. Mamlaka hii haipati bajeti yeyote kutoka Serikalini na inaendeshwa kwa mapato ya meli za uvuvi za kimataifa zinapokata leseni ya kuja kuvua katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilianzisha tozo ya dola 0.4 kwa kilo ya samaki itakayovuliwa. Baada ya kuanzishwa kwa tozo hii nchini wamegoma kuleta meli zao katika eneo letu hili la EEZ (Exclusive Economic Zone). Ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri na Serikali Kuu kwa ujumla waifute tozo hii ili kuokoa mamlaka yetu hii.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikifuta tozo hiyo Serikali ianze kujipanga kwa kununua meli zake zenyewe za uvuvi wa Bahari Kuu sambamba na ujenzi wa bandari ya uvuvi kama nilivyoandika hapo awali. Nimeona kwenye hotuba kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufufua Shirika la Uvuvi (TAFICO) pamoja na mipango ya kununua meli mbili za uvuvi; hili ni jambo jema. Niiombe Serikali sasa iongeze kasi ya kutekeleza malengo haya.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni Kuhusu Hifadhi ya Bahari Mafia (MPRU) Taasisi hii imepewa Mamlaka ya kuwekeza katika visiwa vidogo vya uvuvi. Mwekezaji huyu amekumbwa na changamoto za kutoshirikisha Mamlaka za Halmashauri ya Wilaya kwenye kutoa vibali stahiki kama vibali vya ujenzi. Nikuombe Mheshimiwa Waziri Mamlaka hii ya MPRU ampe maagizo ya kufuata sheria za nchi.

Mheshimiwa Spika, lingine ni hili linalohusu vifaa vinavyotumia FAD’S (Fishing Aggregating Devices); tunaomba viletwe Mafia kwani kwa sasa wavuvi wanatumia njia za kutosa magari mabovu baharini na kuchafua mazingira.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono.