Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya mifugo pamoja na uvuvi. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu, kwa kazi nzuri wanayoifanya, pia na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, Mheshimiwa Mpina, Mheshimiwa Ulega, Naibu, Katibu Mkuu Prof. Elisante, pamoja na Katibu Mkuu wa Uvuvi, Tamatama.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema kuwa, Wizara ya Mifugo, pamoja na Uvuvi, inajitahidi ninapenda kuwapa pongezi kwa kazi nzuri sana wanayoifanya. Licha ya bajeti kupungua pungua au kufanya nini, lakini wanajitahidi sana kwa kazi nzuri wanayoendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwapongeza, naomba niongelee kwenye bajeti ya maendeleo, ni kweli, bajeti ya maendeleo imeshuka, imeshuka kwa asilimia 40. Kwa hiyo, nashauri kuwa, hiyo fedha ndogo mnayoipata na kuwa wasiwasi na hiyo miradi ya maendeleo itatekelezwaje kwa hiyo fedha kidogo bilioni tano, naomba sana, tena sana hiyo fedha itakayotolewa, iweze kutekelezwa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, operations za uvuvi, operations za uvuvi zimekuwa zikiendeshwa hapa nchini, Pwani, Kanda ya Ziwa, Tanga, pia hiyo ni Pwani pia. Lakini tunaweza kukutana na wavuvi, kwa kweli operation ni nzuri, naipenda, ni nzuri na Serikali inaipeda, kwa sababu inainua kipato, hao samaki wanaweza kuzalia kwa sababu operation hiyo inasaidia samaki waweze kutaga vizuri, kuliko waweze kuvuna samaki wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mpina nilikuwa nashauri elimu endelee; kabla ya kuchoma nyavu za hao wafugaji waweze kupata elimu ya kutosha ya ni saizi gani ya matundu inayotumika kwa samaki, dagaa, kwa samaki sangara, kwa samaki terapia? Ni aina gani na ni wapi wanapatikana? Swali linakuja, je, tukishazichoma hizo nyavu wale wanaoleta nyavu hapa nchini wanafanywaje? Nilikuwa naomba pia waweze kulifuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna migogoro ya ardhi na watumiaji ardhi. Hii migogoro ya ardhi inatokana na; kwa mfano kwa upande wa wafugaji na wakulima, nina mfano kidogo; juzi juzi pale Ulanga mifugo imeingia kwenye shamba la mpunga pale Nakafulu, wamekula mpunga wote wamemaliza. Kwa hiyo nilikuwa nashauri kuwa mikakati iwepo ya kuwaeleza kuwa wafugaji na wakulima waheshimiane ili migogoro iweze kupungua.

Mheshimiwa Spika kuna mikakati inayoendelea ambayo imepangwa na Serikali, naomba hiyo mikakati iweze kutimilika isiwe mikakati tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Malisho.Tatizo hili la migogoro linaletwa na malisho. Nikisema malisho ya mifugo naamanisha mikunde pamoja na nyasi. Mtoe elimu ya jinsi ya kustawisha hayo malisho (shamba darasa).

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri kuwa haya mashamba darasa yawe kwenye kila kata, hasa kwenye mikoa ile ambayo ni ya wafugaji, ili waweze kujua ni malisho gani na jinsi ya kustawisha hayo malisho.

Mheshimiwa Spika, vilevile tatizo lililopo ni mbegu; mbegu za malisho hazipatikani kwa urahisi. Kuna wakulima wafugaji ambao wanatafuta mbegu lakini hazipatikani madukani. Ningeliomba Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri hizi mbegu ziweze kupatika mashambani kusudi Maafisa Ugani waweze kufanya kazi yao ya kuwaelimisha hawa wafugaji jinsi ya kustawisha haya malisho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kuhusu Ufugaji wa Kisasa. Ni kweli mifugo iko mingi, iko hata hapa Dodoma, iko Manyara, iko Mwanza, na iko kila mahala. Hata hivyo ninaishauri Wizara kuwa ule mpango mkakati mliouweka naomba ufuatwe ili tuweze kufuga kwa kisasa na tuweze kupata mazao mema mazuri kutoka kwenye mifugo yetu. Mifugo tukiiendeleza vizuri tunaweza kupata kuinua kipato chetu pamoja na lishe kutokana na mifugo. Kwa hiyo nilikuwa nashauri jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, Vyakula vya Mifugo Hasa Kuku. Ni kweli kuwa tulitoa tozo na ada tulipunguza kwenye vyakula vya kuku hapa Bungeni. Hata hivyo, licha ya kupunguza hizo tozo na ada tatizo bado liko palepale kwenye vyakula vya kuku. Akina mama na vijana wangeweza kweli kufuga kuku, lakini wanapata tatizo kwa sababu vyakula vya kuku bado viko juu. Najua Mheshimiwa Waziri utaweza kuniambia kuwa watumie malighafi inayozalishwa hapa nchini. Ni kweli, nimefanya utafiti, viwanda hivi ni vya hapa nchini, vinazalisha chakula cha kuku na vinatumia malighafi inayozalishwa hapa nchini lakini bado chakula kiko juu. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba ulifanyie kazi kusudi wanawake, vijana, na wakulima wengine waweze kuendelea kwenye tasnia hii ya ufugaji wa kuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tozo kwenye Sekta hii ya Mifugo imekuwa kubwa na nyingi lakini nashukuru na naipongeza Serikali. Kwenye hotuba ya Waziri amesema…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Dkt. Ishengoma.

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kabla sijamaliza naunga mkono hoja, lakini uvuvi wa aquaculture, naomba utiliwe mkazo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.