Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru wewe mwenye binafsi kwa kutupa nafasi. Pia nashukuru Kamati ya Kilimo Maji na Mifugo kwa michango mizuri ambayo wametoa kwa namna ambavyo wameishauri Serikali na sisi tunasema kwamba ushauri wao wote tumeupokea, tutaufanyia kazi ili tuweze kutekeleza vizuri itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC. Kwa kweli tunampongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuridhia itifaki hii ya maendeleo za nchi za Kusini mwa Afrika, inatupa heshima kubwa kwamba Mwenyekiti wetu sasa atakuwa na nafasi nzuri ya kuweza kutekeleza majukumu yale yote ambapo amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Nchi za SADC. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge tuunge mkono itifaki hii kwa sababu ina manufaa makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetoa maoni mengi kuhusu uwekezaji kwenye utafiti na wengi wameshauri kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuwekeza asilimia moja kwenye mapato ghafi ya Taifa. Ni kweli wazo ni zuri na wengi wameshauri hivyo, tunapokea, lakini nataka niseme tu kwamba uwekezaji kwenye utafiti tunaouzungumzia ni utafiti kwa ujumla, siyo kwenye kilimo peke yake. One percent kutoka kwenye GDP ni kwenye utafiti wote katika Wizara nzima, iwe kwenye elimu iwe kwenye kilimo na maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, maana yake ukichukuwa kwa mfano sasa hivi pato la Taifa ambalo ni takribani zaidi ya Dola za Marekani bilioni 54, maana yake tunahitaji karibu almost trilioni moja kwa ajili ya uwekezaji. Ni wazo zuri, nasi Serikali tunalipokea, lakini wakati wa kupanga vipaumbele, tunaangalia kwa sababu ya mapato kidogo yanayokuwepo, vipaumbele ni nini? Tuwekeze kiasi gani? Kwa hiyo, hili tunalichukuwa, tunaendelea kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya utafiti, inatoka kwenye vyazo vya ndani, inaweza ikatoka kwa Washirika wa Maendeleo, inaweza ikatoka kwa watu binafsi. Sisi kama Serikali kwa mfano upande wa kilimo, mwaka huu tumetenga zaidi ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya utafiti wa mbegu; na hizi hela tutahakikisha kwa kweli TARI wanafanya vizuri katika kufanikisha utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi Wagunduzi wetu wa mbegu wamefanya vizuri sana. Kwa mfano, katika Afrika sina uhakika kama kuna taasisi kama TARI kule Naliendele, kazi ambayo wameifanya na ugunduzi ambao wameufanya na mbegu ambazo zimegundulika, sina uhakika kwenye zao la korosho kama kuna taasisi hapa Afrika ambayo imefanya kama vile; na mbegu zetu sasa hivi zinatumika katika nchi nyingi hapa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuridhia itifaki hii, maana yake manufaa ya mbegu zetu ambazo zinatumika sasa hivi Zambia na nchi nyingine, tutakuwa na uwezo sasa wa kupata angalau mrahaba unaotokana na ugunduzi huu. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba mambo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo kazi ya kufanya mapitio. Sasa hivi tunapitia Sera yetu ya Kilimo ya Mwaka 2013, pia tutakuja na sheria mpya ambayo itakuwa ni jumuifu, ambayo itarekebisha vikwazo vyote ambavyo vitafanya itifaki hii ishindwe kutekelezeka. Kwa hiyo, tutarekebisha kama tulivyoshauriwa na Waheshimiwa Wabunge na Kamati, haya yote tutayazingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge, pamoja na Mheshimiwa Haonga wamechangia sana namna ya kuboresha mbegu, nami nakubaliana na suala la kubadilishwa mbegu za asili. Mbegu za asili ndiyo zimetufikisha hapa, nasi tutakuja sasa hivi na sheria nyingine kwa ajili ya kulinda hizi mbege za asili. Kwa sababu ili uje na mbegu nyingine za kisasa, ni lazima hata mbegu ya asili uitambue; na utakapokuwa una-cross, unaunganisha, basi zote hizi tunataka tuwatambue na tuhakikishe tunalinda kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Nina uhakika kama haya tutayatekeleza, mambo yatakwenda vizuri sana. Kwa hiyo, nilihakikishie Bunge hili kwamba itifaki hii itakuwa na manufaa makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ni nyingi tumeshazisema, kwa sababu ya muda hatutaweza kusema mengi, lakini nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwa pamoja, turidhie Itifaki hii ya Ugunduzi wa Mbegu Mpya za Mimea ili ziwe na manufaa na wagunduzi wetu wapate kuwa na motisha ya kuendelea na ugunduzi na kufanya utafiti wa kila namna; nami nina uhakika mkisharidhia, wagunduzi wengi au watafiti wengi wataenda kuwekeza kule kwa sababu wana uhakika sasa wakiwekeza watapata faida na watapata mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.