Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naungana na walionitangulia kuwapongeza sana Wenyeviti hawa wawili; Mheshimiwa Serukamba pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya UKIMWI. Nimefurahi sana kwa taarifa zao nzuri sana, ushauri wao na maoni yao kuhusu maeneo ambayo wanayasimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze upande wa elimu. Kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Prof. Ndalichako, Waziri wa Elimu kwa kuja Sumve kwenye mahafali. Ujio wake Mheshimiwa Prof. Ndalichako umemuibua kijana mmoja wa kutoka shule zetu za Serikali anayeitwa Mayeka Ndaki aliyepata Division 1.7 shule za Serikali. Ujuo wake Mheshimiwa Waziri kwa kweli tunaufurahia sana; na wameniomba nimletee shukrani hizo ili akipata nafasi siyo vibaya, basi akapita tena kwa sababu aliwatia moyo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Prof. Ndalichako kwa Wilaya yetu ya Kwimba kutupatia Chuo cha VETA. Chuo hicho sasa tayari kimeshaanza kujengwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maana yake siyo Kwimba tu peke yake, ni zaidi ya vyuo karibu 50 vinajengwa nchi nzima kupitia bajeti iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa huu utaratibu mzuri wa Elimu Bila Malipo kuanzia Chekechea mpaka Kidato cha Nne. Naleta ombi kama Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati itampendeza; kama tumeweza kulipia Chekechea mpaka Kidato cha Nne, wanapofaulu hawa vijana kwenda Kidato cha Tano na Sita, mfuko unaweza ukawa mdogo lakini siku zijazo tunaweza tukawafikiria hawa vijana. Maana yake nao ni Watanzania. Kidato cha Tano na cha Sita, ikiwezekana nao waingie kwenye utaratibu huu wa Elimu Bila Malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nakuomba sana, ili tupate wanasayansi wengi na wazuri, tunazo maabara zetu huko kwenye maeneo yetu, tumeanzisha kwa nia nzuri tu. Namshauri Mheshimiwa Mwenyekiti na Waziri wa Elimu, tuone namna nzuri zaidi ya kukamilisha haya maboma ya maabara na kupeleka wataalam pia kwa maana ya Walimu wa Masomo ya Sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tunatengeneza maabara nzuri, tunapeleka na vifaa labda, lakini Walimu wa Masomo ya Sayansi hawapo, inakuwa ni kazi bure. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu nzuri sana hii ya Maendeleo ya Jamii, angalau alione hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, nafikiri Mheshimiwa Waziri Jafo hayupo, lakini Serikali ipo; Mkoa wa Mwanza wakati wanafanya ukarabati katika ukamilishwaji wa maboma, Wilaya ya Kwimba peke yake ndiyo iliyosahaulika. Sijui ni kwa sababu gani? Hii kila siku nimekuwa nikiisema. Ni Wilaya peke yake iliyosahaulika, wilaya nyingine zote zilipewa fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha hayo maboma. Sisi tukaja baadaye tukaomba tupatiwe fedha za maboma 21, lakini mpaka leo, hazijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nije Wizara ya Afya. Nawapongeza wananchi wa Wilaya ya Kwimba na Mkoa wa Mwanza na Watanzania wote kwa ujumla. Wananchi wamejitolea kujenga Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya, cha ajabu ni kwamba hospitali zile ukienda baada ya kufunguliwa utakuta kuna mganga mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tukiziimarisha hizi hospitali zetu kwa maana ya Zahanati, zikaimarika vizuri kukawa na wataalam wa kutosha, tukaviimarisha Vituo vya Afya vikawa na wataalam wa kutosha, madawa, X-Ray, Ultrasound na kadhalika, hutapata wagonjwa wa kwenda kwenye Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa, vinginevyo labda mgonjwa awe amezidiwa sana. Tukiwa na Zahanati na Vituo vya Afya vyenye vyombo vya kutibia na waganga wa kutosha, nina uhakika itasaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwa haina maana, zile nguvu za wananchi tunazipoteza bure. Tumejenga Zahanati, Vituo vya Afya kwa gharama kubwa, ambavyo kwa sasa inakaribia shilingi milioni 900, lakini ukienda unakuta wataalam hawapo. Inakuwa tu kama jitu liko pale, white elephant liko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bado wanaweza kutumia utaratibu mzuri ambao naupendekeza kwa upande wa elimu na kwa upande wa afya. Kama hatuna wataalam wa masomo ya sayansi, hatuna waganga wa kutosha, hivi wale wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu katika vyuo vyetu upande wa elimu na afya, wakati tunasubiri ajira, ili kupunguza hii gap iliyopo ya upungufu wa wafanyakazi, ni jambo ambalo linawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wale mlioshiriki kwenye Mkutano wa SADC pale Dar es Salaam, Rais wa Afrika Kusini alikuja na familia yake inaitwa YES (Youth Employment Service). Unawachukua hawa vijana waliomaliza vyuo wanakwenda kupata uzoefu kwenye maeneo hao. Wakati huo huo watakuwa wanafundisha au wanatoa huduma kuliko kuwaacha tu, wanapata uzoefu. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Waziri wa Afya, hebu tuangalie na hilo nalo mkiona linafaa basi tuweze kufanya hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nitakuwa simtendei haki Rais wangu kama sitampongeza kwa kazi nzuri sana za kizalendo anazozifanya nchi hii. Nawaomba sana Watanzania wenzangu wote, hata upande wa kule kwa rafiki yangu Mheshimiwa Mbowe, Rais anafanya kazi nzuri sana, nzuri mno na kila mtu anaona. Cha kufanya ni sisi Watanzania tuungane tumwombee ili aendelee na kasi ya kutuletelea maendeleo Watanzania wote. Haya mengine yatafuata baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme, Mheshimiwa Mbatia alisema maneno mazuri sana jana, nikawa nafikiria, Mwalimu Nyerere alikaribishwa pale New York na Mama Mongella, akamkuta Mganda mmoja, huyo Mganda akamwuliza Mwalimu, Mwalimu siku hizi kwenu sisikii neno ukabila, Mwalimu akamwambia, mama ilikuwa zamani, siyo leo; saa hizi wanasema!

Mheshimiwa Naibu Spika, nami namwambia Mheshimiwa Mbatia, ule utaratibu wa 1995 tulipoingia Bungeni na ustahimilivu wa namna ile na kuitetea Serikali ilikuwa wakati huo baba, siyo leo. Sasa Wabunge wote humu, hasa upande ule kule kuna mhemko! Uchaguzi kesho kutwa, wanafikiria, hivi viti kweli nitavirudia tena mwakani! Hiki ni kionjo tu, itakapofika kwenye Bunge la Bajeti ni mshike mshike! Kwa hiyo, tuvumiliane tu ndugu zangu. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)