Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mtu wa kwanza kabisa kuchangia Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha Februari, 2019 mpaka Januari, 2020.

Mheshimiwa Spika, acha nijikite kwenye Wizara zote tatu kwenye mambo muhimu ambayo nilifikiri kwamba yanahitaji kusukumwa ili kuleta ufanisi katika Wizara hizo. Naomba nianze na Wizara ya Mambo ya Ndani na nianze na kipengele kile cha Sekta ya Ulinzi Binafsi.

Mheshimiwa Spika, Makampuni ya Ulinzi Binafsi yalianza hapa nchini mwaka 1980 yakiwa na makampuni mawili tu; Ultimate Security na Group Four. Makampuni hayo yamezidi, leo hii yako 2,000 na zaidi, yakiajiri askari walinzi wanaozidi 200,000, karibu 250,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sekta hii ilianza miaka 40 iliyopita na haina sheria yoyote, haina miongozo yoyote, haina kanuni yoyote, wala ilipoanzishwa haikuwa hata na GN. Kwa hiyo, ilianzishwa tu na matakwa ya aliyekuwa IGP Philemon Mgaya kutokana na ombwe la kuhitaji ulinzi baada ya Serikali kubadilisha Sera ya Mali kutoka mali za Serikali na kuwa mali za watu binafsi zilizokuwa zimetaifishwa wakati ule na mashirika mapya yaliyoanzishwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa muda wa miaka yote hii makampuni haya yaliyoanzishwa kwa kanuni kwamba walioanzisha walikuwa ni Askari wastaafu wakiwa na miaka 60 na leo kama bado wapo wana miaka 100; kwa hiyo, makampuni haya yameendeshwa kwa kurithiana.

Mheshimiwa Spika, waliorithi makampuni haya huenda hawana hata ujuzi kabisa wa Sekta ya Ulinzi Binafsi, kwa hiyo, wanakamata silaha, wana bunduki, na kadhalika, lakini vibali vilivyokuwa vinatoka havikuwa na kanuni yoyote ya kusema kampuni, mwenye kampuni, mradi yeye alikuwa Askari. Bahati mbaya walipofariki, wamerithi watoto, wamerithi wake zao na ndugu wengine ambao hawana taaluma ya ulinzi. Kwa hiyo, uko umuhimu sasa wa kuanzisha au Bunge lako litunge sheria ya sekta ya ulinzi binafsi.

Mheshimiwa Spika, nilifanya juhudi kubwa ya kuleta Sheria ya sekta ya Ulinzi Binafsi hapa Bungeni; nikaleta Ofisini kwako na baadaye Serikali wakaichukua wakasema wangeileta hapa Bungeni kwa sababu ni muhimu sana na imetokea hivi karibuni mali nyingi za binafsi na miradi inahitaji ulinzi na makampuni yamejiimarisha kuleta wataalam wengine kutoka nje wenye uwezo mkubwa, makomandoo, wengine wakiwa ni Askari wenye rank za juu.

Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri makampuni yameanzishwa na wataalam waliokuwepo wakati ule, ma-IGP wote waliostaafu wameanzisha makampuni ya ulinzi, viongozi wengi wa majeshi wameanzisha kampuni za ulinzi, lakini hakuna sheria ya kuya-control makampuni haya jinsi ya kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nashauri na Kamati ilishauri kwamba sasa umefika wakati Serikali ilete sheria ile ambayo inaishikilia mpaka sasa. Kwa hiyo, nategemea Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa ajaribu kutueleza sheria hii muhimu ya Sekta ya Ulinzi Binafsi inakuja lini Bungeni ili tuweze kuipitisha na baadaye itumike kwa ajili ya kuyaongoza makampuni? Hatuwezi kuyafukuza makampuni ya ulinzi, hatuwezi kuifunga Sekta ya Ulinzi Binafsi, ila tunaweza kui- control kwa kutumia sheria.

Mheshimiwa Spika, liko suala la NIDA. Katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Taasisi ya NIDA imepewa jukumu la kugawa vitambulisho katika nchi yetu kwa wananchi wote nchini, lakini nasikitika sana NIDA imekuwa tatizo kubwa sana ambalo ni kichomi ambacho kimeshindwa kutatulika. Serikali imesaidia sana kuwapa fedha, lakini hatuelewi!

Mheshimiwa Spika, NIDA au Kitambulisho cha Taifa vijijini, nafikiri mpaka tutazeeka, tutaondoka wananchi wa Tanzania nzima hawatapata vitambulisho kwa sababu, hakuna msimamo au mkakati maalum wa kwenda vijijini kama ambavyo daftari la kupiga kura limeenda. Wananchi wote wanaotaka kupiga kura wamepata kadi za kupigia kura.

Mheshimiwa Spika, ulikuwa ni mpango mzuri wa NEC uliofanyika kufika vijijini. NIDA kijijini kwangu katika Jimbo langu sijawaona, hawajaenda, lakini wameenda sehemu ndogo tu, yaani sehemu za miji, basi. Hili limekuwa tatizo kubwa, limejitokeza hata wakati wa kusajili simu kwa vidole ambapo ilikuwa ni lazima NIDA uwenayo, imeonesha ni kiasi gani tatizo ni kubwa. Tusingejua kama tatizo ni kubwa kama kusingekuwa na kusajili line za simu. Kwa hiyo, nashauri na Kamati yetu imeshauri kwamba NIDA waje na mkakati mpya wa kufikia sehemu zote za vijiji.

Mheshimiwa Spika, liko suala lingine la wakimbizi. Wakimbizi kwa uungwana wetu Serikali iliwapa uraia, lakini bahati mbaya sana ikawaacha kwenye makambi yale yale waliyopatia uraia na wameanza kujiunda na kuunda na kuelewana wenyewe kwa wenyewe na wana mpango hata wa kuwa na Serikali yao ndani ya eneo lile walilomo; na kumekuwa na utata mkubwa sana, wakimbizi hawa sasa wanaishi kama raia wa Tanzania wa kawaida na wanasoma sana, wanajiingiza kwenye sehemu nyingine za kazi, sehemu za majeshi na sehemu za elimu ya juu.

Mheshimiwa Spika, tatizo linaonekana kwamba kwa vile wanakaa pamoja pale pale, mkakati wa kuwasambaza wakimbizi hawa ni suala la muhimu sasa ili wasije wakakaa na kuunda mkakati ambao utakuja kuleta hasara kwenye Serikali yetu na wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwenye shughuli za kazi za Wizara ya Mambo ya Nje tuliongelea mambo ya mipaka yetu na tuligusa mpaka wa Uganda ambako kumekuwa na utata wa nyuzi ngapi mpaka wa Tanzania unapita, lakini pia suala la mpaka wa Malawi, iko haja sasa Wizara ya Mambo ya Nje ione umuhimu wa kuweka mipaka katika maeneo ambayo tunafikiri kwamba yana utata katika Ziwa Nyasa na kule Uganda.

Mheshimiwa Spika, mwishoni nitoe shukrani kubwa, sikupata nafasi ya kuongea wakati wa sekta hizi nyingine. Nitoe shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Joseph John Pombe Magufuli pamoja na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ambayo imeleta maendeleo makubwa katika Jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu tumepata Kituo cha Afya kimoja kwa gharama ya shilingi milioni 850; pia, tumepata Hospitali ya Wilaya kwa shilingi bilioni mbili. Vile vile tumepata mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria ambao utakuwa kwenye vijiji 40, kwenye 500 vijiji 80. Pia mradi wa REA una vijiji 18 katika vijiji vile 82. Tunaomba basi tuongezewe idadi ya vijiji ambavyo vitapata umeme wa REA.

Mheshimiwa Spika, pia tumepata mradi wa Kituo cha VETA kwa shilingi bilioni tano na sasa hivi kuna mpango wa kujenga Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi ambayo itagharimu mabilioni mengi. Yote haya kwa kweli yamekuwa njozi tulikuwa tunaota, lakini kwa kipindi cha miaka minne Mheshimiwa Rais ametuletea mambo haya yote. Wananchi wangu wanafurahi sana, wanamshukuru sana na wanamwombea maisha marefu Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)