Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia kwenye hii hoja yetu ya Kilimo. Kwanza kabisa niunge hoja mkono kwa asilimia mia moja na nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sana katika taarifa au hoja aliyoisoma Mheshimiwa Waziri amekiri kabisa kwamba, kuna matatizo ya climate change kwenye maeneo mbalimbali ya Tanzania ambayo yanaweza yakasababisha upungufu wa mazao au chakula hasa katika Mkoa wetu wa Shinyanga. Mimi naongelea Mkoa wetu wa Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilinganisha mikoa ambayo hali ya hewa ikibadilika kidogo tu mambo yanakuwa tofauti kabisa na watu walivyotarajia katika suala zima la kilimo. Ukilinganisha Mikoa ya Shinyanga na mikoa ya Kusini, mikoa ya Kusini ukiongelea masuala mazima ya umwagiliaji wanakushangaa. Mikoa ile imeneemeka na mvua ni nyingi na watu wanalima vizuri sana, lakini Mkoa kama wa Shinyanga hivi ninavyozungumza hali ya mazao katika Jimbo la Solwa per se, Jimbo la Solwa sasahivi mazao mengi yamekauka. Ukienda Bariadi, ukienda Mkoa wa Simiyu, ukienda kote mambo ni hivyohivyo yanakauka halafu baadaye kidogo tena mvua inanyesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili nataka tu nimshauri Mheshimiwa Waziri kwenye maeneo ambayo ni muhimu sana ya kimkakati katika kuyaokoa, sisi katika Mkoa wa Shinyanga tunalima vizuri sana na hatupendi kuomba chakula, kinachohitajika pale ni kutengenezewa miundombinu itakayokwenda kuondoa tatizo hili la tatizo la njaa. Sasa eneo pekee, nimweleze Mheshimiwa Waziri, angechukua Mkoa wa Shinyanga na mikoa mingine ambayo anaiona yeye inafaa kwa kuanzia hizi fedha kwa ajili ya umwagiliaji skimu za umwagiliaji ziende maeneo hayo kwa sababu, hakuna eneo linaweza likatusaidia au kuwasaidia wakulima wa Jimbo la Solwa kama skimu ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Solwa tuna skimu sita, lakini skimu ambazo ziko vizuri ni skimu tatu ambazo hata hivyo upembuzi yakinifu ulishafanyika na tumeshaomba fedha kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa kwenye maeneo hayo. Hizo skimu zipo kweli, tunashukuru sana kwanza Serikali ka kufanya kazi kubwa ya kutuletea skimu hizo, lakini skimu ni mifereji ina maana kwamba, mvua ikikauka na yenyewe haina kazi kwa hiyo, ili mifereji ifanye kazi vizuri lazima ujenge bwawa, lile bwawa ndio linanywesha, ndio linamwaga pale kwenye skimu ya umwagiliaji kwenye mifereji, wakulima wanalima hata kama mvua haipo. Hivi ninavyoongea sasa hivi kuna tatizo kubwa sana la njaa, yaani njaa ipo, baada ya miezi miwili mitatu itakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina skimu ya umwagiliaji ya Nyida ambayo kwenye taarifa hapa kampuni au Shirika la Maendeleo la JICA ndio sasahivi linafanya kazi pale katika kutengeneza ile mifereji. Tunawashukuru sana na tunashukuru sana Serikali kwa kuliona hilo. Gharama inayotumika pale ni milioni 466, urefu wa mita 1,325 itakuwa ni skimu ya umwagiliaji nzuri sana. Kinachotakiwa pale ni kujenga bwawa tu, upembuzi wa bwawa na usanifu ulishamalizika na tulishaomba maombi maalum kabisa ya 2.5 billion ili sasa skimu ile iweze kukamilika, Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida katika Jimbo la Solwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Umwagiliaji katika Kata ya Masengwa, Skimu ya Umwagiliaji katika Bwawa la Ishololo, wote huu ni umwagiliaji ambao sasa hivi nataka Serikali kwa jicho la huruma sana, kama ni fedha kwa ajili ya kuwasaidia wakulima, kama ni fedha kwa ajili ya kuondokana na matatizo haya ya njaa katika Mkoa wa Shinyanga, eneo muhimu sana, mimi binafsi namshauri sana Mheshimiwa Waziri tujikite sana kwenye skimu ya umwagiliaji. Kwa hiyo, naomba sana na tayari tulishaomba fedha hizo na tayari iko Wizarani kwako, sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kujibu hoja zetu Mheshimiwa ni matarajio yangu ataniambia kwamba, fedha zote tulizoomba ameshatupa, ili twende sasa tukawaambie wananchi waende wachimbe mabwawa na Mungu atambariki sana na tunaunga hoja mkono vizuri na Serikali ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Masengo ni skimu ya muda mrefu sana. Kuna wakati tuliwahi kupata fedha milioni 900, lakini kutokana na committment nyingi za Serikali fedha hizi hatukuletewa, tukasema haina shida, lakini sasa hivi tunaomba. Bahati nzuri sana usanifu, narudia tena, usanifu ulishafanyika kwa skimu zote tatu hizi, kwa hiyo, suala hapa ni kutafuta fedha tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye Bwawa la Ishololo ambalo nalo ni muhimu sana kwenye Kata ya Usule, bwawa hili lilianza mradi mwaka 2013. Mkandarasi aliyepewa bwawa hili alifikia asilimia 30 na muda wake wa mkataba ukawa umekwisha kwa hiyo, fedha tulizopewa na Bank of Africa wakasitisha wakaondoka. Kwa hiyo, mradi umefika asilimia 30 na umesimama mpaka hivi ninaongea leo. Tumerudia tena usanifu, tumeomba fedha kwa mara ya pili ni 1.2 billion.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninayoongea haya ni miradi ambayo inafanyika, iko njiani tunakwenda kukamilisha, siongelei miradi mipya. Katika hoja yake Mheshimiwa Waziri amesema atajikita zaidi kwenye miradi ambayo haikukamilika, iko kati ya asilimia 30, 50 mpaka mwisho, kwa hiyo, miradi hii ninayomweleza ya Skimu ya Umwagiliaji ya Nyida, skimu ya Umwagiliaji ya Masengwa, Bwawa la Ishololo ni miradi ambayo ipo katika asilimia 30 au 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea hii Wizara ya Kilimo ina Waziri ambaye namwaminia sana. Mheshimiwa Waziri namwamini sana, najua kabisa atayachukua haya, atakwenda kuyafanyia kazi. Sisi Waheshimiwa Wabunge katika Mkoa wa Shinyanga hakuna kitu kinatusumbua sisi kama mabadiliko ya hali ya hewa. Yaani hali ya hewa ikikataa mvua kidogo tu mazao yanakauka na mambo yote yanakuwa yameharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu wa Maafisa Ugani 56. Maafisa Ugani ni watu muhimu sana, bila kuwa na Maafisa Ugani kwenda kuwaeleza wakulima, wakulima bado wanalima kilimo kilekile cha zamani, kilimo kisichokuwa na tija, kilimo ambacho kwa kweli, wanatumia nguvu kubwa, lakini mafanikio yao yanakuwa ni madogo. Kwa hiyo, pamoja na kuwa tuna upungufu wa Maafisa 56 ni kweli inawezekana kabisa akatuletea 10, 20, ninachoomba atuongezee pale ambapo anaona inampendeza, ili sasa Jimbo la Solwa tuweze kuongeza Maafisa Ugani wazuri waweze kutoa elimu vizuri, hii ni pamoja na usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani wanapata shida sana kwenda kwa wakulima. Mheshimiwa Waziri atuletee mwongozo tu kwamba, katika bajeti ya mwaka huu tunahitaji, Halmashauri ninyi katika mwongozo wa kilimo kwamba, mpange pikipiki kwa ajili ya Maafisa Ugani hata kwa ngazi ya kata. Tunaweza tukaanzia kwa ngazi ya kata peke yake. Mimi nina kata 26 nikipata pikipiki 26 maana yake tayari tumeshajenga network ya Maafisa Ugani na wakulima, tutakuwa tayari tumewajengea uwezo mzuri mno wakulima kulima kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri sana katika Jimbo la Solwa tuna zao moja la dengu ambalo linatumika kama zao la biashara, lakini zao la dengu wanalima kata kama nne au tano tu. Ukichukua Kata ya Salawe, Kata ya Bhukande, Kata ya Mwakitolyo na Kata ya Solwa ndio wanaolima dengu na hiyo dengu kwa mfano hivi sasa hivi kama kuna matatizo ya mazao, kutokuwepo na mazao hawavuni vizuri wanategemea mazao hayo ya dengu, lakini kata zilizobaki zote wanategemea zaidi mahindi pamoja na mpunga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina mengi zaidi ya hapa. Nilikuwa nataka tu kujikita zaidi kwenye masuala mazima ya umwagiliaji na hili suala la umwagiliaji hatuna namna yoyote kabisa katika kuokoa wakulima wa Jimbo la Solwa au Mkoa wa Shinyanga...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja mkono. Nakushukuru sana. (Makofi)