Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda. Nafikiri tatizo tulilonalo katika nchi yetu ni viongozi wetu wengi na Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi muda mrefu kuishi kwa kaulimbiu bila kuwa na utekelezaji. Kwa sababu tangu awamu zilizopita zote kuacha Awamu hii ya Tano, ukiangalia mtazamo wa viongozi wakuu ilikuwa ni Tanzania ya viwanda, wala wazo hili halijaanza sasa kwa Awamu ya Tano, lakini suala ni kwamba je, katika muda wote huo ni kwa kiwango gani tumefikia kwenye malengo ambayo tumekuwa tukiyazungumza; ni utayari gani uliopo juu ya viongozi wetu wanaopewa hizo dhamana za kutekeleza hayo? Ndilo swali ambalo tunatakiwa wote tujiulize.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana wakati mwingine viongozi wetu wakuu wana mawazo mazuri sana ya kutupeleka mahali, lakini inawezekana wasaidizi wao ama hawako tayari au hawana uelewa juu ya dhamira za viongozi wakuu wanazokuwa nazo juu ya safari tunayotakiwa twende. Kwa hiyo kuna haja ya kubadilisha sana mawazo na mitazamo yetu ili tufikie hapa tunapotarajia kupafikia. Vinginevyo dhana hii ya Tanzania ya viwanda itakuwa inakuwa ni wimbo tu kama ambavyo zimekuwa ni nyimbo tangu baada ya Serikali ya Awamu ya Kwanza katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani lilikuwa jambo jema tu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu imeamua kufikia malengo ya kuwa na Tanzania ya viwanda, kufikia uchumi wa kati, basi ingerudi pale ambapo mwaka 1985 Mwalimu Nyerere aliachia wakati anaacha nchi hii. Kwa sababu miaka hiyo tayari mwelekeo wa namna gani tunatakiwa tujenge Taifa la viwanda ulishaonekana katika nchi hii. Bahati mbaya Serikali hii hii ya Chama cha Mapinduzi, viongozi waliofuata baada ya Mwalimu wakaamua kuondoa yale matumaini yote ambayo yalikuwa yamewekwa kwa Watanzania juu ya kujenga Tanzania ya viwanda. Tumerudisha wazo hilo sasa kwa Awamu hii ya Tano, je, sisi wasaidizi wa Rais tuko tayari katika kufikia malengo hayo ama tunajaribu kumwonesha Rais kwamba tuna dhamira wakati hatuna dhamira hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri unajaribu kutafakari, je, kweli tuna hiyo dhamira; tumedhamiria kufika Tanzania ya viwanda? Kwa hiyo haya ni maswali ambayo sote tunatakiwa tujiulize kwa pamoja na nafikiri kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi wanatakiwa wajiangalie sana, tusipende kuishi kwa kauli mbiu ambazo tunazi-take by event, kwa matukio na hatuzifanyii kazi. Tusifanye suala la viwanda kama suala la zimamoto, tudhamirie kweli kwamba tunajenga Tanzania ya viwanda kwa sababu ni ukweli kwamba ndiyo kichocheo cha maendeleo ya Taifa hili kwa sasa na kwa siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu hiki cha bajeti, ukiangalia trend ya bajeti ya Wizara ya Viwanda mwaka 2017/2018, 2018/2019 na hata 2019/2020, unaona kabisa kwamba bajeti iliyotengwa inaonesha kwamba Serikali ina dhamira ya ku-facilitate ukuaji wa viwanda katika nchi hii na ukuaji wa biashara katika nchi hii. Hata hivyo, tofauti yake ni kwamba ukiangalia maneno ya viongozi wa Serikali, maneno hata ya kiongozi wetu mkuu, inaonekana kama vile Serikali imeamua sasa kufanya biashara yenyewe, imeamua kuendesha viwanda yenyewe, imeamua ku- centralize hivi vitu badala ya mfumo ambao tulishazoea kwamba tunategemea kuimarisha Private Sector.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa matokeo yake Serikali inachukua majukumu mazito sana. Ukiangalia bajeti hii ina fedha ndogo sana lakini hushangai kwa bajeti ndogo kwa sababu dhamira ya kweli ya Serikali ilikuwa ni kusaidia kuhakikisha mazingira mazuri ya biashara katika nchi hii, mazingira mazuri ya uwekezaji katika nchi hii, mazingira mazuri ya uwepo wa viwanda katika nchi hii, lakini ukweli halisi ulioko kwenye utendaji, Serikali inaonesha wananchi kwamba yenyewe ndiyo inataka ifanye kazi ya biashara, ifanye kazi ya kujenga viwanda na vitu vingine kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo inaonekana kwamba wana-discourage sekta binafsi, hawataki kui-encourage sekta binafsi, ndiyo maana kila anayenyanyuka hapa anasema kuna vikwazo vingi sana kwa wafanyabiashara ambao ni ukweli ulio halisi. Leo Wabunge hapa wanalalamika kuhusu hivi vi-regulator vingi ambavyo vimekuwepo vinavyotoza wafanyabiashara. Sasa swali langu najiuliza, kama Serikali wanasikia haya Wabunge wanayolalamika, hao regulators wote kama TFDA, TBS na nyingine nyingi zimewekwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge, kwa nini Waziri asifanye kazi rahisi tu mpaka leo aambiwe ajiuzulu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alete sheria hapa viunganishe hivi vitu, waambiwe Wabunge wabadilishe sheria, kwa sababu hivi tunavyozungumza viko kwa mujibu wa sheria; TFDA wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, TBS kwa mujibu wa sheria, OSHA kwa mujibu wa sheria. Bahati mbaya bado hawajaanza kutufunga, wakianza kutufunga ndiyo tutajua kwamba wapo kwa mujibu wa sheria mlizotunga ninyi wenyewe, sasa hivi bado wanatupiga tu penati, wanatuadhibu, sheria zinaruhusu watufunge, sasa siku wakianza kuwafunga hapa ndiyo tutaona kelele zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo cha msingi, Serikali walete mapendekezo hapa au hoja, Wabunge wajadili, waone namna gani wanawapunguzia wafanyabiashara hizi adha. Vinginevyo watu wa OSHA watalalamikiwa wakati wanaangalia sheria; TRA watalalamikiwa wakati wanaangalia sheria na wengine wote watalalamikiwa wakati sheria mmetunga wenyewe hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TRA wangefanya kazi kwa mujibu wa sheria ilivyo kila mtu huku ndani angekuwa amefungwa kama ni mfanyabiashara. Kwa hiyo watu wanasema TRA ni wabaya sana, lakini ukiniuliza nitakwambia TRA hawajawa wabaya kwa sababu bado hawajafunga watu, bado wanakudai fedha zao ambazo hujalipa, penati kama hujalipa au umechelewa kwa muda, lakini kama unataka kufanya kazi kama ilivyo watafunga hata watu wengine hapa ndani, kila siku watu watafungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nafikiri kwa sababu wanaolalamika ni Wabunge na ndio wanaomwelekeza Mheshimiwa Waziri, ni rahisi tu; alete sheria hapa zibadilishwe ziweze kusaidia nchi yetu iende mbele na tuweze kukuza viwanda vyetu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba kufanya biashara katika Tanzania ni adhabu kubwa sana. Wakati naingia kama Mbunge hapa nilikuwa nafikiri labda Wabunge humu ndani hawajui ugumu huu, lakini baadaye nikagundua viongozi wengi walikataa biashara wakaamua kuwa wakulima na kule kwenye kilimo wamejifichia huko, wana mamilioni ya pesa kibao lakini wamejifichia huko. Sasa mateso yote yako kwa wafanyabiashara, yaani ukiamua kufanya biashara wewe katika nchi hii ni umenunua mateso makubwa sana katika Taifa hili, kwa nini? Kwa sababu siku zote wamekuwa wakiwa na perception ya kupata kodi, kupata fedha, lakini hawataki kumlea huyo ng’ombe ambaye wanamkamua ili wapate hiyo kodi, hawataki kabisa, yaani Serikali inafikiri kodi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia katika Taifa hili biashara zimefungwa nyingi halafu watu tumekaa kimya na kuna majibu yanakuja kwamba biashara zilizofungwa ni watu ambao wanakwepa kodi, as if hao sio Watanzania. Walishaenda wakaonana nao, wakafahamu kwa nini wamefunga hizo biashara? Kwa nini wafikiri tu kwamba ni kwa sababu wamekwepa kodi, kwa nini wafikiri kitu kimoja tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza kila kukicha biashara zinafungwa. Inawezekana hazijafika milioni, lakini ukweli unabaki kwamba kuna biashara kadhaa zimefungwa katika Taifa hili, zimefungwa kwa nini? Kwa sababu ya mfumo usio rafiki kwa wafanyabiashara wa nchi hii. Je, Waziri na Wizara yake wamewasaidiaje wafanyabiashara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapokaa hapa kama watetezi tusiwafanye wafanyabiashara kama watu wasiotuhusu. Tuna tatizo kubwa la nchi hii kuamini kwamba wafanyabiashara wote ni mabepari, wafanyabiashara wote wanakwepa kodi, which is not true. Kuna wafanyabiashara wanalipa kodi, mfumo wetu wa kodi ndiyo sio mzuri. Sasa tuwasaidie wafanyabiashara hawa na ndiyo kazi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kuwasaidia wafanyabiashara. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri ili aweze kuacha legacy asaidie wafanyabiashara, asimwachie jukumu hili Mheshimiwa Rais peke yake. Rais mpaka aamke, akishaamka na wao ndiyo wanaamka, haiwezekani, hatuwezi kuendesha Serikali ambayo Rais ndio everything. Rais ana wasaidizi wake, Urais ni taasisi, lazima asaidiwe na je, wanamsaidia inavyostahili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tusipoweka dhamira ya kutosha, leo tunazungumzia habari ya viwanda karibu 4,000 na kitu ambavyo vimekua katika nchi hii. Hata kama hivyo viwanda tunasema ni vya vyerehani, ni vya nini, lakini kwa mujibu wa kanuni ni viwanda vidogo. Wajibu wetu, je, tuna mkakati gani wa kuinua hawa wawekezaji wa viwanda wadogowadogo wawe wawekezaji wakubwa wa viwanda; wajibu huo tumejipangaje nao? Kwa sababu leo Wachina tunaozungumza miaka ya 2000 ukienda kwao kule Guangzhou ilikuwa watu wanazalisha bidhaa zao, chaki mtu anazalisha kwenye kibanda cha nyumbani, lakini leo Wachina hao hao wamekuwa ni mabilionea katika nchi zao. Je, sisi tunajiandaa vipi kuwa-empower hawa wafanyabiashara wadogowadogo wawe wafanyabiashara wakubwa ndani ya nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama tunataka kufikia malengo ya kuwa Tanzania ya viwanda, tuna kazi kubwa ya kufanya na tudhamirie, tuwe na viongozi wabunifu, waliodhamiria kulipeleka Taifa hili mbele. Kama viongozi watabaki kuishi maisha yaleyale waliyozoea kumdanganya Rais kwamba wanafanya wakati hawafanyi ili wapate Uwaziri, wapate Naibu Uwaziri, wapate Ukatibu Mkuu, nchi hii hatuendi popote na kila siku tutakuwa na wimbo wa Tanzania ya viwanda ambayo hatutaifikia na itakuja Serikali nyingine na wao wamesema wanataka kutawala miaka mia moja, watatawala miaka mia moja wakiwa wanaishi katika Tanzania ambayo sio ya viwanda wala sio ya kilimo, itakuwa Tanzania… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Japhary.

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hayo ndiyo yalikuwa maombi yangu, naomba kushauri, nashukuru sana. (Makofi)