Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kidogo Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa azma yake nzuri ya kutaka kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati lakini pia Tanzania ya viwanda. Kila mtu ana mtazamo wake katika jambo hili. Mimi naona tatizo tulilonalo hapa Tanzania bado Waziri hajawa na usimamizi mzuri, yeye ni baba, kama ni baba anatakiwa alee wafanyabiashara na wenye viwanda wote. Anapopelekewa matatizo ni wajibu wake kuhakikisha anayashughulikia haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini na wala siwezi kukubali kama kuna mtu anataka kuwekeza nchini aje awekeze bila kufanya utafiti kwanza. Kwa hiyo, cha kwanza anachokuja kufanya ni kuhakikisha yale mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kama ni mazuri lakini ataangalia wale walioanzisha viwanda wana changamoto gani ndipo hapo atakapoamua sasa na yeye aje awekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hapa Tanzania tuna changamoto nyingi za viwanda na inaweza ikachukua miaka, Kamati itapita leo itaikuta, itapita mwakani itaikuta, itapita mwaka miwngine itaikuta bado haijatatuliwa. Mimi nashauri sana Serikali mara nyingi wawe karibu na wafanyabiashara na wenye viwanda kuwasikiliza. Kuwasikiliza tu haitoshi, wawatatulie na matatizo yao pale yanapotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeshuhudia mengi katika viwanda lakini mimi nataka niseme jambo moja ambalo linanisikitisha tuna viwanda vingi hapa nchini tayari vina uwezo wa kuzalisha mali inayotosheleza mahitaji ya nchi lakini bado bidhaa zile zinaagizwa kutoka nje. Mimi nafikiri kama tunataka kweli tuwe na viwanda basi tuamue kuwalinda wale ambao tayari wana uwezo wa kuzalisha mali ya kutosheleza nchi hii. Mfano mkubwa ni viwanda vya plastiki, nondo na viwanda vingine. Kuna mwekezaji amewekeza kiwanda hapa cha nondo ametumia dola milioni 30, kiwanda kina uwezo wa kuzalisha metric tone 200,000 lakini leo anazalisha metric tone 15,000 tunategemea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kukuza uchumi cha kwanza tuwalinde wenye viwanda ili kuongeza ajira kwa watu wetu. Tunaponunua bidhaa kutoka nje maana yake tunaongeza ajira kwa wenzetu wenye viwanda vya kule nje. Kwa hiyo, kama tunataka kukuza biashara kwanza tukuze viwanda, hiyo itatusaidia kuongeza wafanyakazi na ajira kwa vijana wetu. Imefika mahali sasa lazima tuamue, tusiogope. Yapo mambo tunaogopa kutatua lakini yapo mambo tunaweza tukayaamua tu na kuaona kama yataleta tija ama la. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mfano huo mmoja wa kiwanda cha nondo lakini bado tuna viwanda vingine vinazalisha mali pia, saruji, mabati na vinginevyo, bado hatujaweka mkakati wa kuhakikisha tunapunguza uingizaji wa bidhaa hizo hapa nchini. Naiomba sana Wizara wahakikishe kama bidhaa zinazoagizwa zipo hapa nchini wapunguze uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengi wamezungumza lakini na mimi nataka niseme moja, TIRDO, SIDO, CAMARTEC na wengine tunawategemea ndio wazalishaji watakaowawezesha wajasiriamali wadogowadogo kule vijijini. Tunasema wao kazi yao ni kukuza teknolojia ili watu kule vijijini waweze kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeshuhudia kabisa wenzetu hawa mashine wanazofanyia ni za toka mimi sijamaliza shule, tukienda na mfumo huo hatutafika. Tunachokiomba Serikali iweke mkazo wa kuongeza bajeti katika Wizara hii hasa katika bajeti ya maendeleo, kuhakikisha wanapewa teknolojia mpya, mashine mpya na wale wakufunzi wanapata mafunzo ya kisasa ili watu waweze kujiletea maendeleo kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata bidhaa zetu kwa mfano, tumekuta trekta pale Arusha, lakini naamini trekta lile pengine limetengenezwa siyo chini ya miezi nane au zaidi, moja tu. Sasa lile si kwamba watu hawana uwezo wa kutengeneza uwezo wanao lakini teknolojia za mashine zetu bado ni mno. Kwa hiyo, tujaribu, yako mambo tunaweza kuyafanya wenyewe na mengine tunaweza tukawatumia wataalam kutoka nje. Naomba sana Serikali ijitahidi katika hili lakini ifike mahali tuamue tufikie mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza ni hii ETS, kila mtu ameizungumzia. Ukiona Mheshimiwa Waziri tunaizungumzia sana maana yake inatuumiza. Inatuumiza kwa sababu mimi siamini, sasa hivi Kiwanda cha Bia TBL kwa hesabu zao za haraka kwa mwaka mmoja watalipa ETS shilingi bilioni saba. Wenyewe wanasema 10% wanayolipa ambayo ni shilingi bilioni 78 lakini mimi naona wala hapajaharibika kitu, Serikali ikae kitako tu, ikae na hawa wenzetu wazungumze wakubaliane na kama itashindikana kama walivyosema wenzangu au ilivyosema hii taarifa yetu, bora tutafute njia mbadala ya kuweza kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hii inayolipwa kwanza haiendi Serikalini, sisi tungefurahi tungesikia ile pesa ya ETS inakwenda Serikalini tungeanza kuzungumza lugha nyingine, lakini pesa hii yote inakwenda kwa mtu. Mtu tu ambaye ameweka kifaa chake pale anakusanya pesa, kwa kweli, hii inatia uchungu sana. Mimi naomba sana Mheshimiwa Waziri suala hili liangalie na ulifanyie kazi kwa sababu wenye viwanda wanalalamika sana kuhusu jambo hili na jambo hili litakwenda kuleta athari kubwa siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli sasa hivi hawajapandisha baadhi ya bei ya bidhaa zao, lakini wakianza kupandisha bei Serikali ijue kwamba itapunguza mapato kwa sababu hata hiyo juice inayoitwa kijoti inayokwenda kuongeza Sh.9 watu watakuwa hawanunui, watakwenda kununua matunda sokoni wakoroge basi. Kwa hiyo, tuone kwamba hapa tutakuja kupoteza siku zijazo. Naiomba sana Serikali iendelee kuangalia hili na ikiwezekana ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalmiko makubwa kule kwa wenzetu wa TRA hasa katika mizigo inayoingia bandarini. Mimi nafikiri inawezekana lipo inawezekana halipo lakini sisi tunatoa tahadhari tu kwa Serikali kama kweli hili lipo linazungumzwa basi ni vizuri wakaanza kufanya mchakato wa kufuatilia na kuona kama ni tatizo gani liko bandarini kwa wenzetu wa TRA. Wanavyolalamika wenzetu hawa kwamba bidhaa zinaingia lakini wakati wa kuzifanyia tathmini inafanywa ndogo, kwa hiyo, zinaingia sokoni zinakuwa na bei rahisi na wengine wanasema wanaghushi risiti, vifaa vinaingia vingi vinalipiwa kidogo. Mambo kama haya ni madogomadogo sana, naomba sana Serikali iyasimamie na hatimaye tuone mafanikio gani tutayapata hapo mbele ili wote tuende kwenye huo uchumi wa viwanda tunaoukusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)